Matendo 8:1-8
Matendo 8:1-8 NENO
Naye Sauli alikua pale, akiridhia kuuawa kwa Stefano. Siku ile kukatukia mateso makuu dhidi ya kanisa huko Yerusalemu, waumini wote isipokuwa mitume wakatawanyika, wakakimbilia Yudea na Samaria. Watu wacha Mungu wakamzika Stefano na kumwomboleza sana. Lakini Sauli alianza kuliangamiza kanisa. Aliingia nyumba kwa nyumba, akiwaburuta wanaume na wanawake, na kuwafunga gerezani. Kwa hiyo wale waliotawanyika wakalihubiri neno la Mungu kila mahali walipoenda. Filipo akaenda mji mmoja wa Samaria akawahubiria habari za Kristo. Watu walipomsikia Filipo na kuona ishara na miujiza alizofanya, wakasikiliza kwa makini yale aliyosema. Pepo wachafu wakawa wakiwatoka watu wengi huku wakipiga kelele, na wengi waliopooza na viwete wakaponywa. Hivyo pakawa na furaha kuu katika mji huo.

