Matendo 8:1-8
Matendo 8:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Saulo naye alikiona kitendo hicho cha kumwua kuwa sawa. Siku hiyo kanisa la Yerusalemu lilianza kuteswa vibaya. Waumini wote, isipokuwa tu wale mitume, walilazimika kutawanyika katika sehemu za mashambani za Yudea na Samaria. Watu wamchao Mungu walimzika Stefano na kumfanyia maombolezo makubwa. Wakati huohuo, Saulo alijaribu kuliangamiza kanisa. Alikwenda katika kila nyumba, akawatoa nje waumini, wanaume kwa wanawake, akawatia gerezani. Wale waumini waliotawanyika, walikwenda kila mahali wakihubiri ule ujumbe. Naye Filipo aliingia katika mji wa Samaria na kumhubiri Kristo kwa wenyeji wa hapo. Watu walijiunga kusikiliza kwa makini ule ujumbe wa Filipo na kuona ile miujiza aliyoifanya. Maana pepo wachafu waliokuwa wamewapagaa watu wengi waliwatoka wakipiga kelele kubwa; na pia watu wengi waliokuwa wamepooza viungo na waliolemaa waliponywa. Kukawa na furaha kubwa katika mji ule.
Matendo 8:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Siku ile kukatokea mateso makuu kwa kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya Yudea na Samaria, isipokuwa hao mitume. Watu watauwa wakamzika Stefano, wakamfanyia maombolezo makuu. Sauli akaliharibu kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani. Lakini wale waliotawanyika wakaenda huku na huko wakilihubiri neno. Filipo akateremka akaingia katika mji wa Samaria, akawahubiria Kristo. Na mkutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule.
Matendo 8:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Siku ile kukatukia adha kuu ya kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya Uyahudi na Samaria, isipokuwa hao mitume. Watu watauwa wakamzika Stefano, wakamfanyia maombolezo makuu. Sauli akaliharibu kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani. Lakini wale waliotawanyika wakaenda huko na huko wakilihubiri neno. Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo. Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule.
Matendo 8:1-8 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Naye Sauli alikua pale, akiridhia kuuawa kwa Stefano. Siku ile kukatukia mateso makuu dhidi ya kanisa huko Yerusalemu, waumini wote isipokuwa mitume wakatawanyika, wakakimbilia Yudea na Samaria. Watu wacha Mungu wakamzika Stefano na kumwomboleza sana. Lakini Sauli alianza kuliangamiza kanisa. Aliingia nyumba kwa nyumba, akiwaburuta wanaume na wanawake, na kuwafunga gerezani. Kwa hiyo wale waliotawanyika wakalihubiri neno la Mungu kila mahali walipoenda. Filipo akaenda mji mmoja wa Samaria akawahubiria habari za Kristo. Watu walipomsikia Filipo na kuona ishara na miujiza alizofanya, wakasikiliza kwa makini yale aliyosema. Pepo wachafu wakawa wakiwatoka watu wengi huku wakipiga kelele, na wengi waliopooza na viwete wakaponywa. Hivyo pakawa na furaha kuu katika mji huo.