Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 20:13-27

Matendo 20:13-27 NENO

Tukatangulia kwenye meli, tukasafiri kwenda Aso ambako tungemchukua Paulo. Alikuwa amefanya utaratibu huu kwa sababu alikuwa akienda huko kwa miguu. Alipotukuta huko Aso, alijiunga nasi kwenye meli, tukasafiri hadi Mitilene. Kutoka huko tuliendelea kwa meli, na kesho yake tukafika mahali panapokabili Kio. Siku iliyofuata tukavuka kwenda Samo, na kesho yake tukawasili Mileto. Paulo alikuwa ameamua tusipitie Efeso ili asitumie muda mwingi huko jimbo la Asia. Alikuwa na haraka ya kufika Yerusalemu kabla ya siku ya Pentekoste kama ingewezekana. Paulo akiwa Mileto, alituma mjumbe kwenda Efeso kuwaita wazee wa kanisa waje wakutane naye. Walipofika akawaambia, “Ninyi wenyewe mnajua jinsi nilivyoishi muda wote nilikuwa nanyi, tangu siku ya kwanza nilipokanyaga hapa jimbo la Asia. Nilimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote na kwa machozi nikivumilia taabu na mapingamizi yaliyonipata kutokana na hila za Wayahudi. Mnajua kwamba sikusita kuhubiri jambo lolote ambalo lingekuwa la kuwafaa ninyi, lakini nilifundisha hadharani na nyumba kwa nyumba. Nimewashuhudia Wayahudi na Wayunani kwamba inawapasa kumgeukia Mungu kwa kutubu dhambi na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo. “Nami sasa nimesukumwa na Roho, ninaenda Yerusalemu wala sijui ni nini kitakachonipata huko. Ila ninachojua tu ni kwamba Roho Mtakatifu amenionya kuwa vifungo na mateso vinaningoja. Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa ya thamani kwangu, kama kuyamaliza mashindano na kukamilisha ile kazi Bwana Yesu aliyonipa, yaani kazi ya kuishuhudia Injili ya neema ya Mungu. “Nami sasa najua kuwa hakuna hata mmoja miongoni mwenu niliowahubiria ufalme wa Mungu atakayeniona tena. Kwa hiyo nawatangazia leo, sina hatia ya damu ya mtu yeyote. Kwa kuwa sikusita kuwatangazia mapenzi yote ya Mungu.

Video ya Matendo 20:13-27