Matendo 20:13-27
Matendo 20:13-27 Biblia Habari Njema (BHN)
Sisi tulipanda meli tukatangulia kwenda Aso ambako tungemchukua Paulo. Ndivyo alivyopanga; maana alitaka kufika huko kwa kupitia nchi kavu. Basi, alitukuta kule Aso, tukampandisha melini, tukaenda Mitulene. Kutoka huko tulisafiri tukafika Kio kesho yake. Siku ya pili, tulitia nanga Samo na kesho yake tukafika Mileto. Paulo alikuwa amekusudia kuendelea na safari kwa meli bila kupitia Efeso ili asikawie zaidi huko Asia. Alikuwa na haraka ya kufika Yerusalemu kwa sikukuu ya Pentekoste kama ingewezekana. Kutoka Mileto Paulo alituma ujumbe kwa wazee wa Efeso wakutane naye. Walipofika kwake aliwaambia, “Mnajua jinsi nilivyokaa nanyi siku zote tangu siku ile ya kwanza nilipofika Asia. Mnajua jinsi nilivyomtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, kwa machozi na matatizo yaliyonipata kutokana na mipango ya hila ya Wayahudi. Mnajua kwamba sikusita hata kidogo kuwahubiria hadharani na nyumbani mwenu na kuwafundisha chochote ambacho kingewasaidieni. Niliwaonya wote – Wayahudi, kadhalika na watu wa mataifa, wamgeukie Mungu na kumwamini Bwana wetu Yesu. Sasa, sikilizeni! Mimi, nikiwa ninamtii Roho, nakwenda Yerusalemu bila kufahamu yatakayonipata huko. Ninachojua tu ni kwamba Roho Mtakatifu ananithibitishia katika kila mji kwamba vifungo na mateso ndivyo vinavyoningojea. Lakini, siuthamini uhai wangu kuwa kitu sana kwangu mradi tu nikamilishe ule utume wangu na ile kazi aliyonipa Bwana Yesu niifanye, yaani nishuhudie Habari Njema ya neema ya Mungu. “Nimepita miongoni mwenu nyote nikiuhubiri ufalme wa Mungu. Sasa lakini, najua hakuna hata mmoja wenu atakayeniona tena. Hivyo, leo hii ninawathibitishieni rasmi kwamba ikijatokea akapotea mmoja wenu, mimi sina lawama yoyote. Kwa maana sikusita hata kidogo kuwatangazieni azimio lote la Mungu.
Matendo 20:13-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini sisi tukatangulia kwenda merikebuni, tukaabiri kwenda Aso, tukikusudia kumpakia Paulo huko; kwa maana ndivyo alivyoagiza, yeye mwenyewe aliazimia kwenda kwa miguu. Alipotufikia huko Aso, tukampakia, kisha tukafika Mitilene. Tukatweka kutoka huko, na siku ya pili tukafika mahali panapokabili Kio; siku ya tatu tukawasili Samo, tukakaa Trogilio, siku ya nne tukafika Mileto. Kwa sababu Paulo alikusudia kusafiri pasipo kupitia Efeso merikebuni, asije akakawia katika Asia; kwa maana alikuwa na haraka, akitaka kuwahi Yerusalemu siku ya Pentekoste, kama ikiwezekana. Toka Mileto Paulo akatuma watu kwenda Efeso, akawaita wazee wa kanisa. Walipofika kwake, akawaambia, Ninyi wenyewe mnajua tangu siku ya kwanza nilipokanyaga hapa Asia, jinsi nilivyokuwa kwenu wakati wote, nikimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, na kwa machozi, na majaribu yaliyonipata kutokana na njama za Wayahudi; ya kuwa sikujiepusha katika kuwatangazia neno lolote liwezalo kuwafaa bali niliwafundisha waziwazi, na nyumba kwa nyumba, nikiwashuhudia Wayahudi na Wagiriki wamtubie Mungu, na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo. Basi sasa, angalieni, nashika njia kwenda Yerusalemu nikiwa nimefungwa rohoni, nisiyajue mambo yatakayonikuta huko; isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki vyaningoja. Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu. Na sasa, tazameni, mimi najua ya kuwa ninyi nyote niliowahubiria ufalme wa Mungu, nikienda huku na huko, hamtaniona uso tena. Kwa hiyo nawashuhudia wote siku hii ya leo, ya kuwa mimi sina hatia kwa damu ya mtu awaye yote. Kwa maana sikujiepusha na kuwahubiria habari ya kusudi lote la Mungu.
Matendo 20:13-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini sisi tukatangulia kwenda merikebuni, tukaabiri kwenda Aso, tukikusudia kumpakia Paulo huko; kwa maana ndivyo alivyoagiza, yeye mwenyewe aliazimu kwenda kwa miguu. Alipotufikia huko Aso, tukampakia, kisha tukafika Mitilene. Tukatweka kutoka huko, na siku ya pili tukafika mahali panapokabili Kio; siku ya tatu tukawasili Samo, tukakaa Trogilio, siku ya nne tukafika Mileto. Kwa sababu Paulo amekusudia kupita Efeso merikebuni, asije akakawia katika Asia; kwa maana alikuwa na haraka, akitaka kuwahi Yerusalemu siku ya Pentekoste, kama ikiwezekana. Toka Mileto Paulo akatuma watu kwenda Efeso, akawaita wazee wa kanisa. Walipofika kwake, akawaambia, Ninyi wenyewe mnajua tangu siku ya kwanza nilipokanyaga hapa Asia, jinsi nilivyokuwa kwenu wakati wote, nikimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, na kwa machozi, na majaribu yaliyonipata kwa hila za Wayahudi; ya kuwa sikujiepusha katika kuwatangazia neno lo lote liwezalo kuwafaa bali naliwafundisha waziwazi, na nyumba kwa nyumba, nikiwashuhudia Wayahudi na Wayunani wamtubie Mungu, na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo. Basi sasa, angalieni, nashika njia kwenda Yerusalemu hali nimefungwa rohoni, nisiyajue mambo yatakayonikuta huko; isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki vyaningoja. Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu. Na sasa, tazameni, mimi najua ya kuwa ninyi nyote niliowahubiria ufalme wa Mungu, nikienda huko na huko, hamtaniona uso tena. Kwa hiyo nawashuhudia wote siku hii ya leo, ya kuwa mimi sina hatia kwa damu ya mtu awaye yote. Kwa maana sikujiepusha na kuwahubiria habari ya kusudi lote la Mungu.
Matendo 20:13-27 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Tukatangulia kwenye meli, tukasafiri kwenda Aso ambako tungemchukua Paulo. Alikuwa amefanya utaratibu huu kwa sababu alikuwa akienda huko kwa miguu. Alipotukuta huko Aso, alijiunga nasi kwenye meli, tukasafiri hadi Mitilene. Kutoka huko tuliendelea kwa meli, na kesho yake tukafika mahali panapokabili Kio. Siku iliyofuata tukavuka kwenda Samo, na kesho yake tukawasili Mileto. Paulo alikuwa ameamua tusipitie Efeso ili asitumie muda mwingi huko jimbo la Asia. Alikuwa na haraka ya kufika Yerusalemu kabla ya siku ya Pentekoste kama ingewezekana. Paulo akiwa Mileto, alituma mjumbe kwenda Efeso kuwaita wazee wa kanisa waje wakutane naye. Walipofika akawaambia, “Ninyi wenyewe mnajua jinsi nilivyoishi muda wote nilikuwa nanyi, tangu siku ya kwanza nilipokanyaga hapa jimbo la Asia. Nilimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote na kwa machozi nikivumilia taabu na mapingamizi yaliyonipata kutokana na hila za Wayahudi. Mnajua kwamba sikusita kuhubiri jambo lolote ambalo lingekuwa la kuwafaa ninyi, lakini nilifundisha hadharani na nyumba kwa nyumba. Nimewashuhudia Wayahudi na Wayunani kwamba inawapasa kumgeukia Mungu kwa kutubu dhambi na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo. “Nami sasa nimesukumwa na Roho, ninaenda Yerusalemu wala sijui ni nini kitakachonipata huko. Ila ninachojua tu ni kwamba Roho Mtakatifu amenionya kuwa vifungo na mateso vinaningoja. Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa ya thamani kwangu, kama kuyamaliza mashindano na kukamilisha ile kazi Bwana Yesu aliyonipa, yaani kazi ya kuishuhudia Injili ya neema ya Mungu. “Nami sasa najua kuwa hakuna hata mmoja miongoni mwenu niliowahubiria ufalme wa Mungu atakayeniona tena. Kwa hiyo nawatangazia leo, sina hatia ya damu ya mtu yeyote. Kwa kuwa sikusita kuwatangazia mapenzi yote ya Mungu.