1 Samweli 14:24-52
1 Samweli 14:24-52 NENO
Basi Waisraeli walikuwa katika dhiki siku ile, kwa sababu Sauli alikuwa amewafunga watu kwa kiapo, akisema, “Alaaniwe mtu yeyote atakayekula chakula kabla ya jioni, kabla sijalipiza kisasi juu ya adui zangu!” Kwa hiyo hakuna mtu yeyote katika jeshi aliyeonja chakula. Jeshi lote liliingia mwituni, na huko kulikuwa na asali juu ya ardhi. Walipoingia mwituni, wakaona asali ikitiririka, hata hivyo hakuna mtu yeyote aliyetia mkono wake kinywani, kwa sababu waliogopa kiapo. Lakini Yonathani alikuwa hajasikia kuwa baba yake alikuwa amewafunga watu kwa kiapo, hivyo akainyoosha ncha ya fimbo iliyokuwa mkononi mwake na kuichovya katika sega la asali. Akainua mkono wake na kuutia kinywani mwake, nayo macho yake yakaangaa. Kisha mmoja wa askari wake akamwambia, “Baba yako alilifunga jeshi kwa kiapo kikali, akisema, ‘Alaaniwe mtu yeyote alaye chakula leo!’ Ndiyo sababu watu wanalegea.” Yonathani akasema, “Baba yangu ameitaabisha nchi. Ona jinsi macho yangu yalipata kuangaa nilipoonja asali hii kidogo. Ingekuwa bora zaidi mara ngapi kama watu wangekula leo baadhi ya nyara walizoteka kutoka kwa adui zao. Je, mauaji ya Wafilisti yasingekuwa makubwa zaidi?” Siku ile baada ya Waisraeli kuwaua Wafilisti kutoka Mikmashi hadi Aiyaloni, walikuwa wamechoka. Watu wakarukia zile nyara, wakichukua kondoo, ngʼombe na ndama, wakawachinja hapo juu ya nchi na kuwala, pamoja na damu. Kisha mtu mmoja akamwambia Sauli, “Tazama, watu wanatenda dhambi dhidi ya BWANA kwa kula nyama yenye damu.” Akasema, “Mmevunja uaminifu. Livingirisheni jiwe kubwa hapa mara moja.” Kisha Sauli akasema, “Nendeni miongoni mwa watu, mwaambie, ‘Kila mmoja wenu aniletee ngʼombe wake na kondoo, mwachinjie hapa na mle. Msitende dhambi dhidi ya BWANA kwa kula nyama ikiwa na damu ndani yake.’ ” Hivyo kila mmoja akaleta ngʼombe wake jioni ile na kumchinja hapo. Ndipo Sauli akamjengea BWANA madhabahu, na ndiyo ilivyokuwa mara yake ya kwanza kujenga madhabahu. Sauli akasema, “Tuteremke tufuatie Wafilisti usiku na kuwateka nyara hadi mapambazuko, nasi tusiache hata mmoja wao hai.” Wakajibu, “Fanya lolote lile uonalo jema zaidi kwako.” Lakini kuhani akasema, “Tuulize kwa Mungu mahali hapa.” Basi Sauli akamuuliza Mungu, akisema, “Je, niteremke kuwafuatia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwa Israeli?” Lakini Mungu hakumjibu siku ile. Kwa hiyo Sauli akasema, “Njooni hapa, ninyi nyote ambao ni viongozi wa jeshi, na tutafute ni dhambi gani imefanywa leo. Kwa hakika kama BWANA aiokoaye Israeli aishivyo, hata kama itakuwa kwa mwana wangu Yonathani, ni lazima afe.” Lakini hakuna mtu yeyote aliyesema neno. Kisha Sauli akawaambia Waisraeli wote, “Ninyi simameni huko; mimi na mwanangu Yonathani tutasimama hapa.” Watu wakajibu, “Fanya lile unaloona jema zaidi kwako.” Kisha Sauli akamwomba BWANA, Mungu wa Israeli, akisema, “Kwa nini hujamjibu mtumishi wako leo? Ikiwa makosa ni yangu au ya mwanangu Yonathani, jibu kwa Urimu. Lakini ikiwa makosa ni ya wanaume wa Israeli, jibu kwa Thumimu.” Yonathani na Sauli wakatolewa kwa kura, nao watu wakawa salama. Sauli akasema, “Pigeni kura kati yangu na mwanangu Yonathani.” Kura ikamwangukia Yonathani. Basi Sauli akamwambia Yonathani, “Niambie ni nini ulichokifanya.” Hivyo Yonathani akamwambia, “Nilionja tu asali kidogo kwa ncha ya fimbo yangu. Je, sasa ni lazima nife?” Sauli akasema, “Mungu na aniadhibu vikali zaidi kama wewe Yonathani hutakufa.” Lakini watu wakamwambia Sauli, “Je, Yonathani atakufa, yeye ambaye ameleta ukombozi huu mkubwa kwa Israeli? Hasha! Hakika kama BWANA aishivyo, hakuna hata unywele wa kichwa chake utakaoanguka juu ya ardhi, kwa kuwa alifanya jambo hili leo kwa msaada wa Mungu.” Basi watu wakamwokoa Yonathani, wala hakuuawa. Kisha Sauli akaacha kuwafuata Wafilisti, nao wakajiondoa na kurudi katika nchi yao. Baada ya Sauli kujitwalia utawala katika Israeli, alipigana dhidi ya adui zake kila upande: Moabu, Waamoni, Edomu, wafalme wa Soba, na Wafilisti. Popote alipogeukia, aliwashinda. Akapigana kishujaa na kuwashinda Waamaleki, akiikomboa Israeli kutoka mikono ya wale waliokuwa wamewateka nyara. Wana wa Sauli walikuwa Yonathani, Ishvi na Malki-Shua. Jina la binti yake mkubwa lilikuwa Merabu, naye mdogo aliitwa Mikali. Jina la mkewe Sauli aliitwa Ahinoamu binti Ahimaasi. Jina la jemadari wa jeshi la Sauli aliitwa Abneri mwana wa Neri, naye Neri alikuwa babaye mdogo Sauli. Babaye Sauli, yaani Kishi, na Neri baba yake Abneri walikuwa wana wa Abieli. Siku zote za utawala wa Sauli zilikuwa za vita vikali dhidi ya Wafilisti, na wakati wowote Sauli alimwona mtu mwenye nguvu au shujaa, alimchukua kwa utumishi wake.