Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samueli 14:24-52

1 Samueli 14:24-52 Biblia Habari Njema (BHN)

Siku ile, Waisraeli walisumbuliwa sana maana Shauli alikuwa amewaapisha watu, “Mtu yeyote atakayekula chakula kabla jua kutua, na kabla sijajilipiza kisasi cha adui zangu, na alaaniwe.” Hivyo, siku yote, hakuna mtu aliyeonja chakula chochote. Watu wote walipofika sehemu yenye msitu, walikuta asali kila mahali. Ingawa watu walipofika msituni na kukuta asali ikidondoka kila mahali hakuna mtu aliyethubutu kula asali hiyo kwa kuogopa kile kiapo walichoapishwa. Lakini Yonathani hakuwa amesikia baba yake alipowaapisha watu. Hivyo akainyosha fimbo aliyokuwa nayo, akaichovya kwenye sega la asali, akala asali hiyo. Hapo akajisikia kuwa na nguvu. Mtu mmoja akamwambia, “Baba yako aliwaapisha watu vikali, akisema, ‘Mtu yeyote atakayekula chakula leo na alaaniwe.’” Nao watu walikuwa hoi kwa njaa. Yonathani akajibu, “Baba yangu anawasumbua watu. Sasa mimi najisikia kuwa na nguvu kwa kuwa nimeonja asali hii kidogo. Kama tu askari wetu wangeweza kula kidogo kutoka nyara walizoteka kutoka kwa adui zao, wengi zaidi wa Wafilisti wangaliuawa.” Siku ile, Waisraeli waliwapiga Wafilisti, tangu Mikmashi mpaka Aiyaloni. Wakati huu Waisraeli walikuwa wamechoka kwa njaa. Basi walikimbilia nyara walizoteka, wakawachukua wanakondoo, fahali na ndama, wakachinja, wakala nyama na damu. Watu wengine wakamwambia Shauli, “Tazama watu wanatenda dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu kwa kula nyama yenye damu.” Shauli akawaambia watu, “Nyinyi ni wahaini. Vingirisheni jiwe kubwa hapa kwangu.” Akawaambia, “Nendeni mkawaambie watu wote walete ng'ombe na kondoo wao hapa, wawachinje na kuwala hapa. Wasitende dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu, kwa kula nyama yenye damu.” Hivyo, usiku ule wote walipeleka ng'ombe wao na kuwachinjia hapo. Basi, Shauli akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu. Hiyo ilikuwa ndiyo madhabahu ya kwanza ambayo Shauli alimjengea Mwenyezi-Mungu. Kisha Shauli akawaambia watu, “Twendeni tukawafuatie Wafilisti usiku, tukawavamie na kupora mali zao mpaka asubuhi; hatutamwacha mtu yeyote hai.” Watu wakamwambia, “Fanya unachoona kuwa chema kwako.” Lakini kuhani akawaambia, “Kwanza tuombe shauri kwa Mwenyezi-Mungu.” Hivyo, Shauli akamwuliza Mungu, “Je, niende kuwashambulia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwa Waisraeli?” Lakini Mungu hakujibu kitu siku hiyo. Shauli akasema, “Njoni hapa enyi viongozi wa watu, tujue ni dhambi gani tumetenda leo. Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai na ambaye huiokoa Israeli, hata kama ni mwanangu Yonathani, lazima auawe.” Lakini hakuna mtu aliyesema neno. Hivyo, Shauli akawaambia, “Nyinyi nyote simameni upande ule, halafu mimi na Yonathani mwanangu tutasimama upande huu.” Wao wakajibu, “Fanya chochote unachoona kinafaa.” Shauli akasema, “Ee Mwenyezi-Mungu wa Israeli, kwa nini hujanijibu mimi mtumishi wako? Ee Mwenyezi-Mungu wa Israeli, ikiwa hatia iko kwangu au kwa Yonathani mwanangu, basi, amua kwa jiwe la kauli ya Urimu. Lakini ikiwa hatia hiyo iko kwa watu wako wa Israeli, amua kwa jiwe la kauli ya Thumimu.” Yonathani na Shauli walipatikana kuwa na hatia, lakini watu walionekana hawana hatia. Shauli akasema, “Pigeni kura kati yangu na mwanangu Yonathani.” Yonathani akapatikana kuwa na hatia. Ndipo Shauli akamwambia Yonathani, “Niambie ulilofanya.” Yonathani akajibu, “Nilikula asali kidogo kwa kutumia fimbo yangu. Niko hapa na niko tayari kufa.” Shauli akasema, “Mungu na anitendee mimi vivyo hivyo na hata na wengine. Yonathani ni lazima utauawa.” Lakini watu wakamwambia Shauli, “Mbona Yonathani aliyeiletea Israeli ushindi huu mkubwa, auawe? Jambo hilo liwe mbali. Twaapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, hata unywele wa kichwa chake hautaanguka chini. Alichokifanya leo, amekifanya kwa msaada wa Mwenyezi-Mungu.” Hivyo, watu walimkomboa Yonathani naye hakuuawa. Kisha Shauli aliacha kuwafuatia Wafilisti, nao Wafilisti wakarudi makwao. Baada ya Shauli kuwa mfalme wa Israeli, alipigana na adui zake kila upande: Wamoabu, Waamoni, Waedomu, wafalme wa Soba, na Wafilisti. Kila alipopigana vita, alishinda. Alipigana kwa uhodari, akawashinda Waamaleki. Aliwaokoa Waisraeli kutoka kwa watu wote waliowashambulia. Watoto wa kiume wa Shauli walikuwa Yonathani, Ishvi na Malki-shua. Binti zake walikuwa wawili; mzaliwa wa kwanza aliitwa Merabu na mdogo aliitwa Mikali. Mkewe Shauli aliitwa Ahinoamu binti Ahimaasi. Kamanda wa jeshi la Shauli aliitwa Abneri, mwana wa Neri, mjomba wa Shauli. Baba wa Shauli alikuwa Kishi na baba wa Abneri alikuwa Neri mwana wa Abieli. Kulikuwa na mapigano makali dhidi ya Wafilisti muda wote Shauli alipokuwa mfalme; na kila mara Shauli alipompata mtu mwenye nguvu au shujaa alimchukua ajiunge na jeshi.

1 Samueli 14:24-52 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Nao watu wa Israeli walisumbuka sana siku ile; lakini Sauli alikuwa amewaapisha watu, akisema, Na alaaniwe mtu awaye yote alaye chakula chochote hadi jioni, nipate kujilipiza kisasi juu ya adui zangu. Basi hakuna mtu miongoni mwao aliyeonja chakula. Nao watu wote wakaingia mwituni; na humo mlikuwa na asali juu ya nchi. Na hapo watu walipoingia mwituni, tazama, hiyo asali ilikuwa ikidondoka; lakini hakuna mtu hata mmoja aliyetia mkono wake kinywani; kwa sababu hao watu walikuwa wakikiogopa kile kiapo. Ila Yonathani hakusikia, hapo babaye alipowaagiza watu kwa kiapo; basi yeye akainyosha ncha ya fimbo iliyokuwa mkononi mwake, na kuichovya katika sega la asali, kisha akatia mkono wake kinywani; na macho yake yakatiwa nuru. Ndipo mmojawapo wa watu akamjibu, akasema, Baba yako aliwaagiza watu sana kwa kiapo, akisema, Na alaaniwe mtu alaye chakula leo. Na hao watu walikuwa wamepungukiwa na nguvu. Ndipo Yonathani akasema, Babangu ameifadhaisha nchi; tafadhali, angalia jinsi macho yangu yalivyotiwa nuru, kwa sababu nilionja asali hii kidogo. Je! Si ingekuwa bora zaidi kama watu wangalikula na kushiba leo katika nyara hizi za adui zao walizoziteka? Kwa maana haukuwa uuaji mkuu sasa katikati ya Wafilisti. Nao wakawapiga watu miongoni mwa Wafilisti siku ile kutoka Mikmashi mpaka Ayaloni; na hao watu walikuwa wamepungukiwa sana na nguvu. Basi watu wakazirukia zile nyara, wakatwaa kondoo, na ng'ombe, na ndama, na kuwachinja papo hapo juu ya nchi, nao wale watu walikuwa wakiwala pamoja na damu. Ndipo wakamwambia Sauli, wakisema, Angalia, watu hao wanakosa juu ya BWANA, kwa jinsi wanavyokula pamoja na damu. Naye akasema, Ninyi mmefanya kwa hiana; vingirisheni kwangu leo jiwe kubwa. Kisha Sauli akasema, Haya! Tawanyikeni katikati ya watu mkawaambie, Nileteeni hapa kila mtu ng'ombe wake, na kila mtu kondoo wake, mkawachinje hapa na kula; wala msikose juu ya BWANA, kwa kula pamoja na damu. Nao watu wote wakaleta kila mtu ng'ombe wake pamoja naye usiku ule, nao wakawachinja hapo. Naye Sauli akamjengea BWANA madhabahu; hiyo ndiyo madhabahu ya kwanza aliyomjengea BWANA. Kisha Sauli akasema, Haya! Na tushuke kuwafuata Wafilisti wakati wa usiku, na kuwateka nyara hata mapambazuko, wala tusiwaache hata mmoja wao. Nao wakamjibu, Fanya lolote uonalo kuwa ni jema. Ndipo yule kuhani akasema, Na tumkaribie Mungu hapa. Basi Sauli akataka shauri kwa Mungu, Je! Nishuke ili kuwafuatia Wafilisti? Je! Utawatia mikononi mwa Israeli? Lakini hakumjibu neno lolote siku ile. Ndipo Sauli akasema, Karibieni hapa, enyi wakuu wote wa watu; mjue na kuona dhambi hii ya leo imekuwa katika kosa gani. Kwa maana, kama aishivyo BWANA, awaokoaye Waisraeli, hata ikiwa iko kwa Yonathani, mwanangu, hakika atakufa. Lakini miongoni mwa watu wote hakuna mtu yeyote aliyemjibu. Ndipo akawaambia Waisraeli wote, Ninyi mtakuwa upande mmoja, na mimi na mwanangu Yonathani tutakuwa upande wa pili. Basi wakamwambia Sauli, Fanya uonayo kuwa ni mema. Kwa hiyo Sauli akamwambia BWANA, Mungu wa Israeli, [Kwa nini usimjibu mtumishi wako leo? Ikiwa dhambi iko ndani yangu, au ndani yake Yonathani mwanangu, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, utoe Urimu; bali ukisema hivi, Dhambi iko katika watu wako Israeli,] utoe Thumimu. Basi Yonathani na Sauli wakatwaliwa, lakini watu wakapona. Basi Sauli akasema, Sasa piga kati ya mimi na mwanangu Yonathani, [yeyote ambaye BWANA atamtwaa, atakufa. Nao watu wakamwambia Sauli, La! Sivyo hivyo; lakini Sauli akawaweza watu. Nao wakapiga kati ya yeye na mwanawe Yonathani,] naye Yonathani akatwaliwa. Ndipo Sauli akamwambia Yonathani, Niambie ulilolifanya. Basi Yonathani akamwambia, akasema, Ni kweli, mimi nilionja asali kidogo kwa ncha ya fimbo ile iliyokuwa mkononi mwangu; na tazama, imenipasa kufa. Naye Sauli akasema, Mungu anifanyie hivi, na kuzidi; kwa kuwa hakika utakufa, Yonathani. Lakini watu wakamwambia Sauli, Je! Atakufa Yonathani, ambaye ndiye aliyeufanya huo wokovu mkuu katika Israeli? Hasha! Kama aishivyo BWANA, hautaanguka chini hata unywele mmoja wa kichwa chake; kwa maana ametenda kazi pamoja na Mungu leo. Hivyo hao watu wakamponya Yonathani, asife. Ndipo Sauli akakwea kuacha kuwafuata Wafilisti; nao Wafilisti wakaenda zao kwao. Basi Sauli alipokwisha kuutwaa ufalme juu ya Israeli, alipigana na adui zake wote pande zote, juu ya Moabu, na juu ya wana wa Amoni, na juu ya Edomu, na juu ya wafalme wa Soba, na juu ya Wafilisti; na popote alipogeukia, akawashinda. Naye kwa ushujaa, akawapiga Waamaleki, na kuwaokoa Waisraeli kutoka kwa mikono ya waliowateka nyara. Basi, wana wa Sauli walikuwa ni hawa, Yonathani, na Ishvi, na Malkishua; na majina ya binti zake wawili yalikuwa haya; jina lake wa kwanza aliitwa Merabu, na jina lake mdogo aliitwa Mikali; na jina lake mkewe Sauli aliitwa Ahinoamu, binti Ahimaasi. Tena, jina la jemadari wa jeshi lake aliitwa Abneri, mwana wa Neri, aliyekuwa baba mdogo wa Sauli. Na Kishi, babaye Sauli, na Neri, babaye Abneri, walikuwa wana wa Abieli. Tena, kulikuwa na vita kali sana juu ya Wafilisti siku zote za Sauli, naye Sauli alipomwona mtu yeyote aliyekuwa hodari, au mtu yeyote aliyekuwa shujaa, humtwaa ili awe pamoja naye.

1 Samueli 14:24-52 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Nao watu wa Israeli walisumbuka sana siku ile; lakini Sauli alikuwa amewaapisha watu, akisema, Na alaaniwe mtu awaye yote alaye chakula cho chote hata jioni, nipate kujilipiza kisasi juu ya adui zangu. Basi hakuna mtu miongoni mwa watu aliyeonja chakula. Nao watu wote wakaingia mwituni; na humo mlikuwa na asali juu ya nchi. Na hapo watu walipokwisha kuingia mwituni, tazama, hiyo asali ilikuwa ikidondoka; walakini hakuna mtu hata mmoja aliyetia mkono wake kinywani; kwa sababu hao watu walikuwa wakikiogopa kile kiapo. Ila Yonathani hakusikia, hapo babaye alipowaagiza watu kwa kiapo; basi yeye akainyosha ncha ya fimbo iliyokuwa mkononi mwake, na kuichovya katika sega la asali, kisha akatia mkono wake kinywani; na macho yake yakatiwa nuru. Ndipo mmojawapo wa watu akamjibu, akasema, Baba yako aliwaagiza watu sana kwa kiapo, akisema, Na alaaniwe mtu alaye chakula leo. Na hao watu walikuwa wamepungukiwa na nguvu. Ndipo Yonathani akasema, Babangu ameifadhaisha nchi; tafadhali, angalia jinsi macho yangu yalivyotiwa nuru, kwa sababu nalionja asali hii kidogo. Je! Si zaidi sana, kama watu wangalikula na kushiba leo katika nyara hizi za adui zao walizoziteka? Kwa maana haukuwa uuaji mkuu sasa katikati ya Wafilisti. Nao wakawapiga watu miongoni mwa Wafilisti siku ile kutoka Mikmashi mpaka Ayaloni; na hao watu walikuwa wamepungukiwa sana na nguvu. Basi watu wakazirukia zile nyara, wakatwaa kondoo, na ng’ombe, na ndama, na kuwachinja papo hapo juu ya nchi, nao wale watu walikuwa wakiwala pamoja na damu. Ndipo wakamwambia Sauli, wakisema, Angalia, watu hao wanakosa juu ya BWANA, kwa jinsi wanavyokula pamoja na damu. Naye akasema, Ninyi mmefanya kwa hiana; vingirisheni kwangu leo jiwe kubwa. Kisha Sauli akasema, Haya! Tawanyikeni katikati ya watu mkawaambie, Nileteeni hapa kila mtu ng’ombe wake, na kila mtu kondoo wake, mkawachinje hapa na kula; wala msikose juu ya BWANA, kwa kula pamoja na damu. Nao watu wote wakaleta kila mtu ng’ombe wake pamoja naye usiku ule, nao wakawachinja hapo. Naye Sauli akamjengea BWANA madhabahu; hiyo ndiyo madhabahu ya kwanza aliyomjengea BWANA. Kisha Sauli akasema, Haya! Na tushuke kuwafuata Wafilisti wakati wa usiku, na kuwateka nyara hata mapambazuko, wala tusiwaache hata mmoja wao. Nao wakamjibu, Fanya yo yote uyaonayo kuwa ni mema. Ndipo yule kuhani akasema, Na tumkaribie Mungu hapa. Basi Sauli akataka shauri kwa Mungu, Je! Nishuke ili kuwafuatia Wafilisti? Je! Utawatia mikononi mwa Israeli? Lakini hakumjibu neno lo lote siku ile. Ndipo Sauli akasema, Karibieni hapa, enyi wakuu wote wa watu; mjue na kuona dhambi hii ya leo imekuwa katika kosa gani. Kwa maana, aishivyo BWANA, awaokoaye Israeli, ijapokuwa i katika Yonathani, mwanangu, kufa atakufa. Lakini miongoni mwa watu wote hakuna mtu ye yote aliyemjibu. Ndipo akawaambia Israeli wote, Ninyi mtakuwa upande mmoja, na mimi na mwanangu Yonathani tutakuwa upande wa pili. Basi wakamwambia Sauli, Fanya uonayo kuwa ni mema. Kwa hiyo Sauli akamwambia BWANA, Mungu wa Israeli, [Kwani usimjibu mtumishi wako leo? Ikiwa dhambi i ndani yangu, au ndani yake Yonathani mwanangu, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, utoe Urimu; bali ukisema hivi, Dhambi i katika watu wako Israeli,] utoe Thumimu. Basi Yonathani na Sauli wakatwaliwa, lakini watu wakapona. Basi Sauli akasema, Sasa piga kati ya mimi na mwanangu Yonathani, [naye awaye yote ambaye BWANA atamtwaa, atakufa. Nao watu wakamwambia Sauli, La! Sivyo hivyo; lakini Sauli akawaweza watu. Nao wakapiga kati ya yeye na mwanawe Yonathani,] naye Yonathani akatwaliwa. Ndipo Sauli akamwambia Yonathani, Niambie ulilolifanya. Basi Yonathani akamwambia, akasema, Ni kweli, mimi nalionja asali kidogo kwa ncha ya fimbo ile iliyokuwa mkononi mwangu; na tazama, imenipasa kufa. Naye Sauli akasema, Mungu anifanyie hivi, na kuzidi; kwa kuwa hakika utakufa, Yonathani. Walakini watu wakamwambia Sauli, Je! Atakufa Yonathani, ambaye ndiye aliyeufanya huo wokovu mkuu katika Israeli? Hasha! Aishivyo BWANA, hautaanguka chini hata unywele mmoja wa kichwa chake; kwa maana ametenda kazi pamoja na Mungu leo. Hivyo hao watu wakamponya Yonathani, asife. Ndipo Sauli akakwea kuacha kuwafuata Wafilisti; nao Wafilisti wakaenda zao kwao. Basi Sauli alipokwisha kuutwaa ufalme juu ya Israeli, alipigana na adui zake zote pande zote, juu ya Moabu, na juu ya wana wa Amoni, na juu ya Edomu, na juu ya wafalme wa Soba, na juu ya Wafilisti; na po pote alipogeukia, akawashinda. Naye akatenda kwa ushujaa, akawapiga Waamaleki, na kuwaokoa Waisraeli katika mikono yao waliowateka nyara. Basi, wana wa Sauli walikuwa ni hawa, Yonathani, na Ishvi, na Malkishua; na majina ya binti zake wawili yalikuwa haya; jina lake wa kwanza aliitwa Merabu, na jina lake mdogo aliitwa Mikali; na jina lake mkewe Sauli aliitwa Ahinoamu, binti Ahimaasi. Tena, jina la jemadari wa jeshi lake aliitwa Abneri, mwana wa Neri, aliyekuwa baba mdogo wa Sauli. Na Kishi, babaye Sauli, na Neri, babaye Abneri, walikuwa wana wa Abieli. Tena, kulikuwa na vita vikali sana juu ya Wafilisti siku zote za Sauli, naye Sauli alipomwona mtu ye yote aliyekuwa hodari, au mtu ye yote aliyekuwa shujaa, humtwaa ili awe pamoja naye.

1 Samueli 14:24-52 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Basi Waisraeli walikuwa katika dhiki siku ile, kwa sababu Sauli alikuwa amewafunga watu kwa kiapo, akisema, “Alaaniwe mtu yeyote atakayekula chakula kabla ya jioni, kabla sijalipiza kisasi juu ya adui zangu!” Kwa hiyo hakuna mtu yeyote katika jeshi aliyeonja chakula. Jeshi lote liliingia mwituni, na huko kulikuwa na asali juu ya ardhi. Walipoingia mwituni, wakaona asali ikitiririka, hata hivyo hakuna mtu yeyote aliyetia mkono wake kinywani, kwa sababu waliogopa kiapo. Lakini Yonathani alikuwa hajasikia kuwa baba yake alikuwa amewafunga watu kwa kiapo, hivyo akainyoosha ncha ya fimbo iliyokuwa mkononi mwake na kuichovya katika sega la asali. Akainua mkono wake na kuutia kinywani mwake, nayo macho yake yakaangaa. Kisha mmoja wa askari wake akamwambia, “Baba yako alilifunga jeshi kwa kiapo kikali, akisema, ‘Alaaniwe mtu yeyote alaye chakula leo!’ Ndiyo sababu watu wanalegea.” Yonathani akasema, “Baba yangu ameitaabisha nchi. Ona jinsi macho yangu yalipata kuangaa nilipoonja asali hii kidogo. Ingekuwa bora zaidi mara ngapi kama watu wangekula leo baadhi ya nyara walizoteka kutoka kwa adui zao. Je, mauaji ya Wafilisti yasingekuwa makubwa zaidi?” Siku ile baada ya Waisraeli kuwaua Wafilisti kutoka Mikmashi hadi Aiyaloni, walikuwa wamechoka. Watu wakarukia zile nyara, wakichukua kondoo, ngʼombe na ndama, wakawachinja hapo juu ya nchi na kuwala, pamoja na damu. Kisha mtu mmoja akamwambia Sauli, “Tazama, watu wanatenda dhambi dhidi ya BWANA kwa kula nyama yenye damu.” Akasema, “Mmevunja uaminifu. Livingirisheni jiwe kubwa hapa mara moja.” Kisha Sauli akasema, “Nendeni miongoni mwa watu, mwaambie, ‘Kila mmoja wenu aniletee ngʼombe wake na kondoo, mwachinjie hapa na mle. Msitende dhambi dhidi ya BWANA kwa kula nyama ikiwa na damu ndani yake.’ ” Hivyo kila mmoja akaleta ngʼombe wake jioni ile na kumchinja hapo. Ndipo Sauli akamjengea BWANA madhabahu, na ndiyo ilivyokuwa mara yake ya kwanza kujenga madhabahu. Sauli akasema, “Tuteremke tufuatie Wafilisti usiku na kuwateka nyara hadi mapambazuko, nasi tusiache hata mmoja wao hai.” Wakajibu, “Fanya lolote lile uonalo jema zaidi kwako.” Lakini kuhani akasema, “Tuulize kwa Mungu mahali hapa.” Basi Sauli akamuuliza Mungu, akisema, “Je, niteremke kuwafuatia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwa Israeli?” Lakini Mungu hakumjibu siku ile. Kwa hiyo Sauli akasema, “Njooni hapa, ninyi nyote ambao ni viongozi wa jeshi, na tutafute ni dhambi gani imefanywa leo. Kwa hakika kama BWANA aiokoaye Israeli aishivyo, hata kama itakuwa kwa mwana wangu Yonathani, ni lazima afe.” Lakini hakuna mtu yeyote aliyesema neno. Kisha Sauli akawaambia Waisraeli wote, “Ninyi simameni huko; mimi na mwanangu Yonathani tutasimama hapa.” Watu wakajibu, “Fanya lile unaloona jema zaidi kwako.” Kisha Sauli akamwomba BWANA, Mungu wa Israeli, akisema, “Kwa nini hujamjibu mtumishi wako leo? Ikiwa makosa ni yangu au ya mwanangu Yonathani, jibu kwa Urimu. Lakini ikiwa makosa ni ya wanaume wa Israeli, jibu kwa Thumimu.” Yonathani na Sauli wakatolewa kwa kura, nao watu wakawa salama. Sauli akasema, “Pigeni kura kati yangu na mwanangu Yonathani.” Kura ikamwangukia Yonathani. Basi Sauli akamwambia Yonathani, “Niambie ni nini ulichokifanya.” Hivyo Yonathani akamwambia, “Nilionja tu asali kidogo kwa ncha ya fimbo yangu. Je, sasa ni lazima nife?” Sauli akasema, “Mungu na aniadhibu vikali zaidi kama wewe Yonathani hutakufa.” Lakini watu wakamwambia Sauli, “Je, Yonathani atakufa, yeye ambaye ameleta ukombozi huu mkubwa kwa Israeli? Hasha! Hakika kama BWANA aishivyo, hakuna hata unywele wa kichwa chake utakaoanguka juu ya ardhi, kwa kuwa alifanya jambo hili leo kwa msaada wa Mungu.” Basi watu wakamwokoa Yonathani, wala hakuuawa. Kisha Sauli akaacha kuwafuata Wafilisti, nao wakajiondoa na kurudi katika nchi yao. Baada ya Sauli kujitwalia utawala katika Israeli, alipigana dhidi ya adui zake kila upande: Moabu, Waamoni, Edomu, wafalme wa Soba, na Wafilisti. Popote alipogeukia, aliwashinda. Akapigana kishujaa na kuwashinda Waamaleki, akiikomboa Israeli kutoka mikono ya wale waliokuwa wamewateka nyara. Wana wa Sauli walikuwa Yonathani, Ishvi na Malki-Shua. Jina la binti yake mkubwa lilikuwa Merabu, naye mdogo aliitwa Mikali. Jina la mkewe Sauli aliitwa Ahinoamu binti Ahimaasi. Jina la jemadari wa jeshi la Sauli aliitwa Abneri mwana wa Neri, naye Neri alikuwa babaye mdogo Sauli. Babaye Sauli, yaani Kishi, na Neri baba yake Abneri walikuwa wana wa Abieli. Siku zote za utawala wa Sauli zilikuwa za vita vikali dhidi ya Wafilisti, na wakati wowote Sauli alimwona mtu mwenye nguvu au shujaa, alimchukua kwa utumishi wake.