YouVersion Logo
Search Icon

Methali 14

14
1Mwanamke mwenye hekima huijenga nyumba yake,
lakini mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.
2Mwenye mwenendo mnyofu humcha Mwenyezi-Mungu,
lakini mpotovu humdharau Mungu.
3Mpumbavu hujiadhibu mwenyewe kwa kuropoka kwake,
lakini mwenye hekima hulindwa na maneno yake.
4Bila ng'ombe wa kulima ghala za mtu ni tupu,
mavuno mengi hupatikana kwa nguvu ya ng'ombe wa kulima.
5Shahidi mwaminifu hasemi uongo,
lakini asiyeaminika hububujika uongo.
6Mwenye dharau hutafuta hekima bure,
lakini mwenye busara hupata maarifa kwa urahisi.
7Ondoka mahali alipo mpumbavu,
maana hapo alipo hamna maneno ya hekima.
8Hekima ya mwenye busara humwonesha njia yake,
lakini upumbavu wa wapumbavu huwadanganya wenyewe.
9Wapumbavu huchekelea dhambi,
bali wanyofu hupata fadhili kwa Mungu.#14:9 aya ya 9 makala ya Kiebrania si dhahiri.
10Moyo waujua uchungu wake wenyewe,
wala mgeni hawezi kushiriki furaha yake.
11Nyumba ya mtu mwovu itabomolewa,
lakini hema ya wanyofu itaimarishwa.
12 # Taz Meth 16:25 Njia unayodhani kuwa ni sawa,
mwishoni yaweza kukuongoza kwenye kifo.
13Huzuni yaweza kufichika katika kicheko;
baada ya furaha huja majonzi.
14Mtu mpotovu atavuna matunda ya mwenendo wake,
naye mtu mwema atapata tuzo la matendo yake.
15Mjinga huamini kila kitu anachoambiwa,
lakini mwenye busara huwa na tahadhari.
16Mwenye hekima ni mwangalifu na huepa uovu,
lakini mpumbavu hajizuii wala hana uangalifu.
17Mwenye kuwaka hasira haraka hutenda kipumbavu,
lakini mwenye busara ana uvumilivu.
18Wajinga hurithi upumbavu,
lakini wenye busara hutuzwa taji ya maarifa.
19Waovu watapiga magoti mbele ya watu wema,
watu wabaya mlangoni mwa waadilifu.
20Maskini huchukiwa hata na jirani yake,
lakini tajiri ana marafiki wengi.
21Anayemdharau jirani yake ni mwenye dhambi,
bali ana heri aliye mwema kwa maskini.
22Anayepanga maovu kweli anakosea!
Wanaopanga kutenda mema hufadhiliwa.
23Bidii katika kila kazi huleta faida,
lakini maneno matupu huleta umaskini.
24Mali ni taji ya fahari ya wenye hekima,
lakini ujinga ni shada la wapumbavu.
25Shahidi wa kweli huokoa maisha,
lakini msema uongo ni msaliti.
26Amchaye Mwenyezi-Mungu ana tumaini imara,
na watoto wake watapata kimbilio salama.
27Kumcha Mwenyezi-Mungu ni chemchemi ya uhai;
humwezesha mtu kuepa mitego ya kifo.
28Fahari ya mfalme ni wingi wa watu wake,
lakini bila watu mtawala huangamia.
29Mtu asiye mwepesi wa hasira ana busara kubwa,
lakini akasirikaye upesi hukuza upumbavu.
30Amani rohoni humpa mtu afya,
lakini tamaa huozesha mifupa.
31Anayemdhulumu maskini anamtukana Muumba wake,
lakini amwoneaye huruma mhitaji anamtukuza Mungu.
32Mwovu huangamizwa kwa matendo yake maovu,
lakini mwadilifu hupata usalama kwa unyofu wake.#14:32 kwa unyofu wake: Kiebrania; katika kifo chake.
33Hekima imo moyoni mwa mtu mwenye busara;
haipatikani kamwe mioyoni mwa wapumbavu.
34Uadilifu hukuza taifa,
lakini dhambi ni balaa kwa taifa lolote.
35Mfalme humfadhili mtumishi atendaye kwa hekima,
lakini hasira yake huwakumba watendao yasiyofaa.

Currently Selected:

Methali 14: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy