Zaburi 89:1-18 BHN

1Ee Mwenyezi-Mungu, nitaimba fadhili zako milele; nitavitangazia vizazi vyote uaminifu wako. 2Natamka kuwa fadhili zako zadumu milele; uaminifu wako ni thabiti kama mbingu. 3Umesema: “Nimefanya agano na mteule wangu, nimemwapia mtumishi wangu Daudi: 4 # Taz Zab 132:11; Mate 2:30 ‘Daima nitamweka mzawa wako kuwa mfalme, tena nitaudumisha ufalme wako milele.’” 5Mbingu na zisifu maajabu yako, ee Mwenyezi-Mungu; uaminifu wako usifiwe katika kusanyiko la watakatifu. 6Nani mbinguni awezaye kulinganishwa nawe ee Mwenyezi-Mungu? Nani aliye sawa nawe kati ya viumbe vya mbinguni? 7Wewe waogopwa katika baraza la watakatifu; wote wanaokuzunguka wanatiwa hofu kuu. 8Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi, ni nani mwenye nguvu kama wewe, ee Mwenyezi-Mungu? Uaminifu umekuzunguka pande zote. 9Wewe watawala machafuko ya bahari; mawimbi yake yakiinuka, wayatuliza. 10Uliliponda joka Rahabu na kuliua; uliwatawanya adui zako kwa nguvu yako. 11Mbingu ni zako na dunia ni yako pia; ulimwengu na vitu vyote vilivyomo wewe uliviumba. 12Wewe uliumba kaskazini na kusini; milima Tabori na Hermoni inakusifu kwa furaha. 13Mkono wako una nguvu, mkono wako una nguvu na umeshinda! 14Uadilifu na haki ni msingi wa utawala wako; fadhili na uaminifu vyakutangulia! 15Heri watu wanaojua kukushangilia, wanaoishi katika mwanga wa wema wako, ee Mwenyezi-Mungu. 16Wanafurahi mchana kutwa kwa sababu yako, na kukusifu kwa ajili ya uadilifu wako. 17Wewe ndiwe fahari na nguvu yao; kwa wema wako twapata ushindi. 18Ee Mwenyezi-Mungu, mlinzi wetu ni wako, mfalme wetu ametoka kwako ewe Mtakatifu wa Israeli.