YouVersion Logo
Search Icon

Methali 13

13
1Mtoto mwenye hekima husikia maagizo ya baba yake,
lakini mwenye dharau hasikilizi maonyo.
2Mtu mwema hupata mema kutokana na maneno yake,
lakini wadanganyifu huishi kwa ukatili.
3Achungaye mdomo wake huyahifadhi maisha yake,
anayeropoka ovyo hujiletea maangamizi.
4Mvivu hutamani lakini hapati chochote,
hali mwenye bidii hujaliwa riziki kwa wingi.
5Mwadilifu huuchukia uongo,
lakini mwovu hutenda kwa aibu na fedheha.
6Uadilifu huwalinda wenye mwenendo mnyofu,
lakini dhambi huwaangusha waovu.
7Baadhi hujidai kuwa matajiri kumbe hawana kitu;
wengine hujiona kuwa maskini hali wana mali tele.
8Fidia ya mtu ni mali yake,
lakini maskini hana cha kutishwa.
9Mwadilifu hungaa kama taa iwakayo vizuri,
lakini waovu ni kama taa inayozimika.
10Kiburi husababisha tu ugomvi,
lakini kwa wanaokubali shauri jema mna hekima.
11Mali ya harakaharaka hutoweka,
lakini akusanyaye kidogokidogo ataiongeza.
12Tumaini la kungojangoja huumiza moyo,
lakini tazamio linalotimia ni mti wa uhai.
13Anayedharau mawaidha anajiletea maangamizi,
lakini anayetii amri atapewa tuzo.
14Mafundisho ya wenye hekima ni chemchemi ya uhai;
humwezesha mtu kuiepa mitego ya kifo.
15Kuwa na akili huleta fadhili,
lakini njia ya waovu ni ya taabu#13:15 aya ya 15 Kiebrania si dhahiri.
16Mwenye busara hutenda kila kitu kwa akili,
lakini mpumbavu hutembeza upumbavu wake.
17Mjumbe mbaya huwatumbukiza watu taabuni,#13:17 huwatumbukiza watu taabuni: Au huanguka taabuni.
lakini mjumbe mwaminifu huleta nafuu.
18Umaskini na fedheha humpata asiyejali mafundisho,
lakini mwenye kusikia maonyo huheshimiwa.
19Inafurahisha upatapo kile unachotaka,
kwa hiyo wapumbavu huchukia kuepa uovu.
20Anayeandamana na wenye hekima hupata hekima,
lakini anayejiunga na wapumbavu atapata madhara.
21Watendao dhambi huandamwa na balaa,
lakini waadilifu watatuzwa mema.
22Mtu mwema huwaachia urithi uzao wake,
lakini mali ya mwenye dhambi imerundikiwa waadilifu.
23Shamba la maskini hutoa mazao mengi,
lakini bila haki hunyakuliwa.#13:23 aya 23 Kiebrania si dhahiri.
24Asiyemwadhibu mtoto wake hampendi;
lakini ampendaye mwanawe humrudi mapema.
25Mwadilifu anacho chakula cha kumtosheleza,
lakini tumbo la waovu hutaabika kwa njaa.

Currently Selected:

Methali 13: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy