YouVersion Logo
Search Icon

Matendo 1

1
1Ndugu Theofilo, Katika kitabu cha kwanza niliandika juu ya mambo yote Yesu aliyotenda na kufundisha tangu mwanzo wa kazi yake 2mpaka siku ile alipochukuliwa mbinguni. Kabla ya kuchukuliwa mbinguni aliwapa maagizo kwa njia ya Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua. 3Kwa muda wa siku arubaini baada ya kifo chake aliwatokea mara nyingi kwa namna ambazo zilithibitisha kabisa kwamba alikuwa hai. Walimwona, naye aliongea nao juu ya ufalme wa Mungu. 4Wakati alipokutana pamoja nao aliwaamuru hivi: “Msiondoke Yerusalemu, bali ngojeni ile zawadi aliyoahidi Baba, ambayo mlikwisha nisikia nikiongea juu yake. 5Kwani Yohane alibatiza kwa maji, lakini baada ya siku chache, nyinyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.”
Yesu anapaa mbinguni
6Basi, mitume walipokutana pamoja na Yesu, walimwuliza, “Je, Bwana, wakati huu ndipo utakaporudisha ule ufalme kwa Israeli?” 7Lakini Yesu akawaambia, “Nyakati na majira ya mambo hayo viko chini ya mamlaka ya Baba yangu, wala si shauri lenu kujua yatakuwa lini. 8Lakini wakati Roho Mtakatifu atakapowashukieni nyinyi, mtapokea nguvu na mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, katika nchi yote ya Yudea na Samaria, na hata miisho ya dunia.” 9Baada ya kusema hayo, wote wakiwa wanamtazama, alichukuliwa mbinguni; wingu likamficha wasimwone tena.
10Walipokuwa bado wanatazama juu angani, akiwa anakwenda zake, mara watu wawili waliokuwa wamevaa nguo nyeupe walisimama karibu nao, 11wakasema, “Enyi wananchi wa Galilaya! Mbona mnasimama mkitazama angani? Yesu huyu ambaye amechukuliwa kutoka kwenu kwenda mbinguni atakuja tena namna hiyohiyo mlivyomwona akienda mbinguni.”
Mathia anachaguliwa ashike nafasi ya Yuda
(Mat. 27:3-10)
12Kisha mitume wakarudi Yerusalemu kutoka ule mlima uitwao Mlima wa Mizeituni ulioko karibu kilomita moja kutoka mjini. 13Walipofika mjini waliingia katika chumba ghorofani ambamo walikuwa wanakaa; nao walikuwa Petro, Yohane, Yakobo, Andrea, Filipo na Thoma, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni Zelote na Yuda mwana wa Yakobo. 14Hawa wote walikusanyika pamoja kusali, pamoja na wanawake kadha wa kadha, na Maria mama yake Yesu, na ndugu zake.
15Siku moja baadaye, Petro alisimama kati ya wale ndugu waumini ambao walikuwa wamekusanyika, wote jumla watu 120, 16akasema, “Ndugu zangu, ilikuwa lazima ile sehemu ya Maandiko Matakatifu itimie, sehemu ambayo Roho Mtakatifu, kwa maneno ya Daudi, alibashiri habari za Yuda ambaye aliwaongoza wale waliomtia Yesu nguvuni. 17Yuda alikuwa mmoja wa kikundi chetu, maana alichaguliwa ashiriki huduma yetu.”
( 18Yeye alinunua shamba kwa zile fedha alizopata kutokana na kitendo chake kiovu, akaanguka chini, akapasuka na matumbo yake yakamwagika nje. 19Kila mtu katika Yerusalemu alisikia habari za tukio hilo na hivyo, kwa lugha yao, wakaliita lile shamba “Akel Dama,” maana yake, “Shamba la Damu.”) 20“Basi, imeandikwa katika kitabu cha Zaburi:
‘Makao yake yabaki mahame;
mtu yeyote asiishi ndani yake.’
Tena imeandikwa:
‘Mtu mwingine achukue nafasi yake ya huduma.’
21Basi, mtu mmoja miongoni mwa wale walioandamana nasi muda wote Bwana Yesu alipokuwa anasafiri pamoja nasi achaguliwe kujiunga nasi. 22Huyo anapaswa kuwa mmoja wa wale walioandamana nasi tangu Yohane alipokuwa anabatiza mpaka siku ile Yesu alipochukuliwa kutoka kwetu kwenda mbinguni. Huyo atashiriki pamoja nasi jukumu la kushuhudia ufufuo wake Yesu.”
23Hapo, wakataja majina ya watu wawili; wa kwanza Yosefu aliyeitwa Barsaba (au pia Yusto), na wa pili Mathia. 24Kisha wakasali: “Bwana, wewe unaijua mioyo ya watu wote. Hivyo, utuoneshe ni yupi kati ya hawa wawili uliyemchagua 25ili achukue nafasi hii ya huduma ya kitume aliyoacha Yuda akaenda mahali pake mwenyewe.” 26Wakapiga kura; kura ikampata Mathia, naye akaongezwa katika idadi ya wale mitume wengine kumi na mmoja.

Currently Selected:

Matendo 1: BHND

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy