YouVersion Logo
Search Icon

Luka 24

24
Kufufuka kwa Yesu
(Mat 28:1-10; Marko 16:1-8; Yoh 20:1-10)
1Jumapili,#24:1 Jumapili: Neno kwa neno: Siku ya kwanza ya juma. alfajiri na mapema, wale wanawake walikwenda kaburini wakichukua yale manukato waliyotayarisha.#24:1-53 Matukio yote ya sura ya 24 yanatendeka siku ileile moja ya Jumapili. Ukilinganisha na ripoti za ufufuo wa Yesu katika Injili nyingine utaona tofauti mbalimbali. Kila mwandishi wa Injili anatumia habari alizozipata mwenyewe kuhabarisha watu juu ya tukio hilo muhimu ambalo bila hilo hakungekuwa na imani ya Kikristo. 2Walikuta lile jiwe limevingirishwa mbali na kaburi. 3Walipoingia ndani, hawakuuona mwili wa Bwana Yesu. 4Walipokuwa bado wanashangaa juu ya jambo hilo, mara watu wawili waliovaa mavazi yenye kung'aa sana, wakasimama karibu nao. 5Hao wanawake wakaingiwa na hofu, wakainama chini. Ndipo wale watu wakawaambia, “Kwa nini mnamtafuta aliye hai kati ya wafu? 6Hayuko hapa; amefufuka. Kumbukeni aliyowaambieni alipokuwa kule Galilaya:#24:6 Baadhi ya hati za mkono za kale hazina maneno: Hayupo hapa; amefufuka (taz Mat 28:6; Marko 16:6). 7‘Ni lazima Mwana wa Mtu atolewe kwa watu waovu, nao watamsulubisha na siku ya tatu atafufuka.’”
8Hapo hao wanawake wakayakumbuka maneno yake, 9wakarudi kutoka kaburini, wakawapa mitume wale kumi na mmoja na wafuasi wengine habari za mambo hayo yote. 10Hao waliotoa habari hizo kwa mitume ni: Maria Magdalene, Yoana na Maria mama wa Yakobo, pamoja na wanawake wengine walioandamana nao. 11Mitume waliyachukua maneno hayo kama yasiyo na msingi, hivyo hawakuamini. 12Lakini Petro alitoka, akaenda mbio hadi kaburini. Alipoinama kuchungulia ndani, akaiona tu ile sanda. Akarudi nyumbani huku akiwa anashangaa juu ya hayo yaliyotokea.#24:12 Baadhi ya hati za mkono za zamani hazina aya 12.
Safari kwenda Emau
(Marko 16:12-13)
13Siku hiyohiyo,#24:13 Wawili kati ya wanafunzi, yaani yamkini wafuasi wa Yesu ambao hawakuwa wa lile kundi la mitume (aya 33). wawili kati ya wafuasi wake Yesu wakawa wanakwenda katika kijiji kimoja kiitwacho Emau,#24:13 Emau: Mahali penyewe hapajulikani dhahiri. Simulizi hili ladhihirisha kwamba kifo na kufufuka kwake Yesu vilikuwa lazima (aya 26 na pia 46) kulingana na nia yake Mungu, na kama ilivyokuwa imetangazwa kabla katika Maandiko Matakatifu (aya 28). umbali wa kilomita kumi na moja kutoka Yerusalemu. 14Wakawa wanazungumza juu ya hayo yote yaliyotukia. 15Walipokuwa wakizungumza na kujadiliana, Yesu mwenyewe akatokea, akatembea pamoja nao. 16Walimwona kwa macho, lakini hawakumtambua.
17Akawauliza, “Mnazungumza nini huku mnatembea?” Nao wakasimama kimya, nyuso zao wamezikunja kwa huzuni. 18Mmoja, aitwaye Kleopa,#24:18 Kleopa: Jina la kiume la Kigiriki; labda si sawa na yule anayetajwa katika Yoh 19:25. akamjibu, “Je, wewe ni mgeni peke yako Yerusalemu ambaye hujui yaliyotukia huko siku hizi?” 19Naye akawajibu, “Mambo gani?” Wao wakamjibu, “Mambo yaliyompata Yesu wa Nazareti. Yeye alikuwa nabii mwenye uwezo wa kutenda na kufundisha mbele ya Mungu na mbele ya watu wote. 20Makuhani na watawala wetu walimtoa ahukumiwe kufa, wakamsulubisha. 21Lakini sisi tulitumaini kwamba yeye ndiye angeikomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu mambo hayo yalipotendeka. 22Tena, wanawake wengine wa kwetu wametushtua. Walikwenda kaburini mapema asubuhi, 23wasiukute mwili wake. Wakarudi wakasema kwamba walitokewa na malaika waliowaambia kwamba alikuwa hai. 24Wengine wetu walikwenda kaburini wakashuhudia yale waliyosema hao wanawake; ila yeye hawakumwona.”
25Kisha Yesu akawaambia, “Mbona mu wapumbavu kiasi hicho na mioyo yenu ni mizito hivyo kusadiki yote yaliyonenwa na manabii? 26Je, haikumpasa Kristo kuteswa, na hivyo aingie katika utukufu wake?” 27Akawafafanulia mambo yote yaliyomhusu yeye katika Maandiko Matakatifu kuanzia Mose hadi manabii wote.#24:27 Maandiko ya A.K. yalijumuisha hasa vitabu vya Mose na vya manabii (tazama maelezo ya Luka 24:44).
28Walipokikaribia kile kijiji walichokuwa wanakiendea, Yesu akafanya kana kwamba anaendelea na safari; 29lakini wao wakamsihi wakisema, “Kaa pamoja nasi, maana kunakuchwa, na usiku unakaribia.” Basi, akaingia kijijini, akakaa pamoja nao. 30Alipoketi kula chakula pamoja nao, akachukua mkate, akaubariki, akaumega, akawapa.#24:30-31 Maneno “kumega mkate” yalitumiwa aghalabu na Kanisa la mwanzoni kwa “Karamu ya Bwana” (Mate 2:42; 20:7; 1Kor 10:16). 31Mara macho yao yakafumbuliwa, wakamtambua; lakini yeye akatoweka kati yao. 32Basi, wakaambiana, “Je, mioyo yetu haikuwa inawaka ndani yetu wakati alipokuwa anatufafanulia Maandiko Matakatifu kule njiani?” 33Wakaondoka saa ileile, wakarudi Yerusalemu; wakawakuta wale mitume kumi na mmoja na wale wengine waliokuwa pamoja nao wamekusanyika 34wakisema, “Hakika Bwana amefufuka, amemtokea Simoni.”#24:34 Habari hii ya Yesu kumtokea Petro haitajwi katika Injili zile nyingine za sunoptiki, lakini Paulo anagusia tukio hilo katika 1Kor 15:5. 35Basi, hao wafuasi wawili wakawajulisha yale yaliyowapata njiani, na jinsi walivyomtambua katika kumega mkate.
Yesu anawatokea wanafunzi wake
(Mat 28:16-20; Marko 16:14-18; Yoh 20:19-23; Mate 1:6-8)
36Walipokuwa wakiwaambia hayo, Yesu mwenyewe akasimama kati yao, akawaambia “Amani iwe nanyi.”#24:36 Amani iwe nanyi: Hayo ni maneno ya salamu ya jadi kwa Wayahudi, maneno ambayo hapa yanachukua maana ya ndani zaidi. 37Wakashtuka na kushikwa na hofu wakidhani wameona mzimu. 38Lakini yeye akawaambia, “Kwa nini mnafadhaika? Mbona mnakuwa na mashaka mioyoni mwenu? 39Angalieni mikono na miguu yangu,#24:39 Mikono na miguu yangu: Yaani waone alama za kusulubiwa; ling pia Yoh 20:20,24-27. Nipapaseni mkaone: ling 1Yoh 1:1. ya kwamba ni mimi mwenyewe. Nipapaseni mkaone, maana mzimu hauna mwili na mifupa kama mnionavyo.”
40Baada ya kusema hayo, akawaonesha mikono na miguu.#24:40 Baadhi ya hati za awali za mkono hazina aya 40. 41Wakiwa bado katika hali ya kutosadiki kwa sababu ya furaha yao, na wakiwa wanastaajabu, akawauliza, “Mnacho chakula chochote hapa?” 42Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa. 43Akakichukua, akala, wote wakimwona. 44Halafu akawaambia, “Hii ndiyo maana ya maneno niliyowaambia nilipokuwa pamoja nanyi: kwamba ilikuwa lazima kukamilisha yote#24:44 Kukamilisha yote: Msemo huu unatupatia malengo ya Injili hii, ambayo ni muhimu na ambayo Luka aliyataja kama utangulizi katika 4:20; linganisha pia Luka 18:31; 22:37. yaliyoandikwa juu yangu katika sheria ya Mose na katika vitabu vya manabii na katika kitabu cha Zaburi.”#24:44 Kitabu cha Zaburi kilikuwa katika sehemu ya kwanza ya mgawo wa Maandiko Matakatifu iliyokuwa kubwa zaidi katika Agano la Kale.
45Kisha, akaziangazia akili zao ili wapate kuelewa Maandiko Matakatifu. 46Akawaambia, “Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu,#24:46 Ling na Isa 53:1-12; Hos 6:2. 47na kwamba ni lazima, kwa jina lake, mataifa yote kuanzia Yerusalemu, yahubiriwe kwamba watu wanapaswa kutubu na kusamehewa dhambi.#24:47 Aya 44-47 kwa kiasi na namna fulani zinatanguliza mahubiri ambayo baadaye mitume watayatoa (ling Mate 2:14-39; 3:17-26; 8:35; 13:16-41; 26:20). 48Nyinyi ni mashahidi wa mambo hayo. 49Nami mwenyewe nitawapelekeeni yule ambaye Baba aliahidi#24:49 Yule ambaye Baba aliahidi: Yaani, Roho Mtakatifu (Mate 1:4; 2:33; ling Yoh 14:16-17,26; 16:7; 20:21-22). kumtuma, lakini ngojeni huku mjini mpaka mtakapopewa ile nguvu itokayo juu.”#24:47-49 Aya hizi zamweka tayari msomaji kwa ajili ya habari za namna hiyo ambazo mwandishi huyo huyo atazitoa mwanzoni mwa kitabu cha Matendo ya Mitume (Ling na Mate 1:1-11; 2:1-4).
Yesu anapaa mbinguni#24:50-53 Kupaa Kwake. Habari hizi zinatolewa kikamilifu zaidi katika kitabu cha Matendo 1:3-11.
(Marko 16:19-20; Mate 1:9-11)
50Kisha akawaongoza nje ya mji hadi Bethania,#24:50 Bethania: Kijiji karibu na Yerusalemu (Mat 21:17). akainua mikono yake juu, akawabariki. 51Alipokuwa anawabariki, akawaacha; akachukuliwa mbinguni. 52Wao wakamwabudu, kisha wakarudi Yerusalemu wakiwa na furaha kubwa: 53wakakaa muda wote hekaluni wakimsifu Mungu.

Currently Selected:

Luka 24: BHNTLK

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy