Mathayo 5
NEN

Mathayo 5

5
Mahubiri Ya Yesu Kwenye Mlima
(Mathayo 5–7)
Sifa Za Aliyebarikiwa
(Luka 6:20-23)
1 # Mk 3:13, 20; Lk 6:20-49 Basi Yesu alipoona makutano, alipanda mlimani akaketi chini, nao wanafunzi wake wakamjia. 2Ndipo akaanza kuwafundisha, akisema:
3 # Mt 5:10, 19; 25:34; Isa 57:15 “Heri walio maskini wa roho,
maana Ufalme wa Mbinguni ni wao.
4 # Isa 61:2-3; Ufu 7:17 Heri wale wanaohuzunika,
maana hao watafarijiwa.
5 # Za 37:11; Rum 4:13 Heri walio wapole,
maana hao watairithi nchi.
6 # Isa 55:1-2 Heri wenye njaa na kiu ya haki,
maana hao watatoshelezwa.
7 # Yak 2:13; Za 41:1; Mt 6:14; Mk 11:24 Heri wenye huruma,
maana hao watapata rehema.
8 # Za 24:3-4; 73:1; 17:15; Ebr 12:14 Heri walio na moyo safi,
maana hao watamwona Mungu.
9 # Mt 5:44, 45; Rum 8:14 Heri walio wapatanishi,
maana hao wataitwa wana wa Mungu.
10 # 1Pet 3:14 Heri wanaoteswa kwa sababu ya haki,
maana Ufalme wa Mbinguni ni wao.
11 # Isa 51:7; 1Pet 4:14 “Heri ninyi watu watakapowashutumu, na kuwatesa na kunena dhidi yenu mabaya ya aina zote kwa uongo kwa ajili yangu. 12#Za 9:2; 2Nya 36:16; 2Kor 6:10Furahini na kushangilia kwa maana thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa kuwa hivyo ndivyo walivyowatesa manabii waliokuwa kabla yenu.
Chumvi Na Nuru
(Marko 9:50; Luka 14:34-35)
13 # Mk 9:50; Lk 14:34-35 “Ninyi ni chumvi ya ulimwengu. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake, yawezaje kurudishiwa ladha yake tena? Haifai tena kwa kitu chochote, ila kutupwa nje ikanyagwe na watu.
14 # Yn 8:12 “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji uliojengwa kilimani hauwezi kufichika. 15#Mk 4:21; Lk 11:33Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa bakuli. Badala yake, huiweka kwenye kinara chake, nayo hutoa mwanga kwa kila mtu aliyemo ndani ya ile nyumba. 16#Efe 5:8-9; 1Pet 2:12Vivyo hivyo, nuru yenu iangaze mbele ya watu, ili wapate kuona matendo yenu mema wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.
Kutimiza Sheria
17 # Rum 3:31; 10:4; Gal 1:24 “Msidhani kwamba nimekuja kufuta Sheria au Manabii; sikuja kuondoa bali kutimiza. 18#Za 119:89; Mk 13:31Kwa maana, amin nawaambia, mpaka mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata herufi moja ndogo wala nukta itakayopotea kwa namna yoyote kutoka kwenye Sheria, mpaka kila kitu kiwe kimetimia. 19#Yak 2:10; 1Kor 15:9Kwa hiyo, yeyote atakayevunja mojawapo ya amri ndogo kuliko zote ya amri hizi, naye akawafundisha wengine kufanya hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika Ufalme wa Mbinguni, lakini yeyote azitendaye na kuzifundisha hizi amri ataitwa mkuu katika Ufalme wa Mbinguni. 20#Rum 9:31; 10:3Kwa maana nawaambia, haki yenu isipozidi haki ya Mafarisayo na walimu wa sheria, kamwe hamtaingia katika Ufalme wa Mbinguni.
Kuhusu Hasira
(Luka 12:57-59)
21 # Kut 21:12; 5:17; Law 24:17 “Mmesikia walivyoambiwa watu wa zamani kwamba, ‘Usiue. Yeyote atakayeua atapaswa hukumu.’ 22#1Yn 3:22; Yn 11:47; Mdo 6:12; Lk 16:24; Yak 3:6Lakini mimi nawaambia kwamba, yeyote atakayemkasirikia ndugu yake, atapaswa hukumu. Tena, yeyote atakayemwambia ndugu yake, ‘Raka,’#5:22 Raka ni neno la Kiaramu ambalo maana yake ni dharau au dhihaka ya hali ya juu. atapaswa kujibu kwa Baraza la Wayahudi.#5:22 Baraza la Wayahudi lilikuwa kundi kuu kabisa la utawala wa Wayahudi lililoundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu. Lakini yeyote atakayesema ‘Wewe mpumbavu!’ atapaswa hukumu ya moto wa jehanamu.
23 # Mt 8:4; 23:19; Mk 11:25 “Kwa hiyo, kama unatoa sadaka yako madhabahuni, ukakumbuka kuwa ndugu yako ana kitu dhidi yako, 24#Ay 42:8; 18:19; 1Tim 2:8; 1Pet 3:7iache sadaka yako hapo mbele ya madhabahu. Enda kwanza ukapatane na ndugu yako; kisha urudi na ukatoe sadaka yako.
25 # Mt 18:35; Lk 12:58-59 “Patana na mshtaki wako upesi wakati uwapo njiani pamoja naye kwenda mahakamani, ili mshtaki wako asije akakutia mikononi mwa hakimu, naye hakimu akakutia mikononi mwa askari, nawe ukatupwa gerezani. 26Amin, nakuambia, hautatoka humo hadi uwe umelipa senti ya mwisho.
Kuhusu Uzinzi
27 # Kut 20:14; Kum 5:18 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Usizini.’ 28#Mit 6:25; 2Pet 2:14Lakini mimi nawaambia kwamba, yeyote amtazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake. 29#Rum 14:21; 1Kor 8:13Jicho lako la kuume likikusababisha kutenda dhambi, lingʼoe ulitupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako mzima ukatupwa jehanamu. 30#Mt 5:29Kama mkono wako wa kuume ukikusababisha kutenda dhambi, ukate, uutupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako mzima utupwe jehanamu.
Kuhusu Talaka
(Mathayo 19:9; Marko 10:11-12; Luka 16:18)
31 # Kum 24:1-4 “Pia ilinenwa kwamba, ‘Mtu yeyote amwachaye mkewe sharti ampe hati ya talaka.’ 32#Lk 16:18Lakini mimi nawaambia, yeyote amwachaye mkewe isipokuwa kwa kosa la uasherati, amfanya mkewe kuwa mzinzi. Na yeyote amwoaye yule mwanamke aliyeachwa, anazini.
Kuhusu Kuapa
33 # Law 19:12; Hes 30:2; Mt 23:16-22 “Tena mmesikia walivyoambiwa watu wa zamani kwamba, ‘Usiape kwa uongo, bali timiza kiapo kile ulichofanya kwa Bwana.’ 34#Yak 5:12; Isa 66:1; Mt 23:22Lakini mimi nawaambia, msiape kabisa: iwe kwa mbingu, kwa kuwa ni kiti cha enzi cha Mungu; 35#Za 48:2au kwa dunia, kwa kuwa ndipo mahali pake pa kuwekea miguu; au kwa Yerusalemu, kwa kuwa ndio mji wa Mfalme Mkuu. 36Nanyi msiape kwa vichwa vyenu, kwa kuwa hamwezi kuufanya hata unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. 37#Yak 5:12; Efe 6:16; 1Yn 3:12‘Ndiyo’ yenu iwe ‘Ndiyo,’ na ‘Hapana’ yenu iwe ‘Hapana.’ Lolote zaidi ya hili latoka kwa yule mwovu.
Kuhusu Kulipiza Kisasi
(Luka 6:29-30)
38 # Law 24:20; Kum 19:21 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Jicho kwa jicho na jino kwa jino.’ 39#1Kor 6:7; 1Pet 3:9Lakini mimi nawaambia, msishindane na mtu mwovu. Lakini kama mtu akikupiga kwenye shavu la kuume, mgeuzie na la pili pia. 40#1Kor 6:7Kama mtu akitaka kukushtaki na kuchukua joho lako, mwachie achukue na koti pia. 41#Mt 27:32; Mk 15:21Kama mtu akikulazimisha kwenda maili moja, nenda naye maili mbili. 42#Kum 15:8; Lk 16:30Mpe yeye akuombaye, wala usimgeuzie kisogo yeye atakaye kukukopa.
Upendo Kwa Adui
(Luka 6:27-28, 32-36)
43 # Law 19:18; Gal 5:14; Kum 23:6; Za 139:21-22 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Mpende jirani yako na umchukie adui yako.’ 44#Yn 15:20; Rum 8:35Lakini ninawaambia: Wapendeni adui zenu na waombeeni wanaowatesa ninyi, 45#Lk 6:35; Rum 8:14; Ay 25:3ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu waovu na watu wema, naye huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. 46#Lk 6:32Kama mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mtapata thawabu gani? Je, hata watoza ushuru hawafanyi hivyo? 47Nanyi kama mkiwasalimu ndugu zenu tu, je, mnafanya nini zaidi ya wengine? Je, hata watu wasiomjua Mungu, hawafanyi hivyo? 48#Law 19:2; 1Pet 1:16Kwa hiyo kuweni wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

Kiswahili Contemporary Version (Neno: Biblia Takatifu)

Copyright ©1984, 1989, 2009, 2015 by Biblica, Inc.® Used by permission.

All Rights Reserved Worldwide Printed.


Learn More About Neno: Bibilia Takatifu 2014

Encouraging and challenging you to seek intimacy with God every day.


YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy.