4
Yesu ajaribiwa nyikani
(Mk 1:12‑13; Lk 4:1‑13)
1 Kisha Yesu akaongozwa na Roho Mtakatifu hadi nyikani ili ajaribiwe na ibilisi. 2Baada ya kufunga siku arobaini usiku na mchana, hatimaye akaona njaa. 3Mjaribu akamjia na kumwambia, “Ikiwa wewe ndiwe Mwana wa Mungu, amuru mawe haya yawe mikate.”
4 Lakini Yesu akajibu, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.’#4:4 Kum 8:3”
5 Ndipo ibilisi akampeleka Yesu hadi mji mtakatifu na kumweka juu ya mnara mrefu wa Hekalu, 6akamwambia, “Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini. Kwa kuwa imeandikwa:
“ ‘Atakuagizia malaika wake,
nao watakuchukua mikononi mwao
ili usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.’#4:6 Za 91:11, 12”
7 Yesu akamjibu, “Pia imeandikwa: ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.’#4:7 Kum 6:16”
8Kwa mara nyingine, ibilisi akampeleka Yesu hadi kwenye kilele cha mlima mrefu na kumwonesha falme zote za dunia na fahari zake, 9kisha akamwambia, “Nitakupa hivi vyote ukinisujudia na kuniabudu.”
10 Yesu akamwambia, “Ondoka mbele yangu, Shetani! Kwa maana imeandikwa, ‘Mwabudu Bwana Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake.’#4:10 Kum 6:13”
11 Ndipo ibilisi akamwacha, nao malaika wakaja na kumhudumia.
Yesu aanza kuhubiri
(Mk 1:14‑15; Lk 4:14‑15)
12 Yesu aliposikia kwamba Yohana Mbatizaji alikuwa amefungwa gerezani, alirudi Galilaya. 13Akaondoka Nazareti akaenda kuishi Kapernaumu, mji ulio karibu na bahari, katika nchi ya Zabuloni na Naftali, 14ili kutimiza neno lililonenwa na nabii Isaya, aliposema:
15 “Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali,
kwenye njia ya bahari,
ngʼambo ya Yordani,
Galilaya ya Mataifa:
16 watu wale waliokaa gizani
wameona nuru kuu;
nao wale walioishi katika nchi ya uvuli wa mauti,
nuru imewazukia.”#4:16 Isa 9:1, 2
17 Tangu wakati huo, Yesu alianza kuhubiri akisema: “Tubuni, kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.”
Wanafunzi wa kwanza wa Yesu
(Mk 1:16‑20; Lk 5:1‑11; Yn 1:35‑51)
18 Yesu alipokuwa akitembea kando ya Bahari ya Galilaya, aliwaona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea ndugu yake. Walikuwa wakizitupa nyavu zao baharini kwa kuwa walikuwa wavuvi. 19Yesu akawaambia, “Njooni, nifuateni nami nitawafanya mwe wavuvi wa watu.” 20Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.
21 Alipoendelea mbele kutoka pale, akawaona ndugu wengine wawili, Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, wakiwa wamekaa kwenye mashua pamoja na baba yao Zebedayo, wakizitengeneza nyavu zao. Yesu akawaita. 22Nao mara moja wakaiacha mashua yao, pamoja na baba yao, wakamfuata.
Yesu afundisha na kuponya wagonjwa
(Lk 6:17‑19)
23 Yesu akazunguka Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, akihubiri habari njema za ufalme, na akiponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi miongoni mwa watu. 24Kwa hiyo sifa zake zikaenea sehemu zote za Siria, nao watu wakamletea wote waliokuwa na magonjwa mbalimbali na maumivu, waliopagawa na pepo wachafu, wenye kifafa na waliopooza, naye akawaponya. 25Makundi makubwa ya watu yakawa yanamjia kutoka Galilaya, Dekapoli#4:25 yaani Miji Kumi, Yerusalemu, Yudea, na kutoka ngʼambo ya Yordani.