Tito 3:1-8
Tito 3:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakumbushe watu kuwastahi watawala na wenye mamlaka, kuwatii na kuwa tayari kwa kila namna kutenda mambo yote mema. Waambie wasimtukane mtu yeyote; bali waishi kwa amani na masikilizano, wawe daima wapole kwa kila mtu. Maana, wakati mmoja sisi tulikuwa wapumbavu, wakaidi na wapotovu. Tulikuwa watumwa wa tamaa na anasa za kila aina. Tuliishi maisha ya uovu na wivu; watu walituchukia nasi tukachukiana. Lakini wakati wema na upendo wa Mungu, Mwokozi wetu ulipofunuliwa, alituokoa si kwa sababu ya jambo lolote jema tulilotenda sisi, bali kwa sababu ya huruma yake, kwa njia ya Roho Mtakatifu anayetujalia tuzaliwe upya na kuwa na maisha mapya kwa kutuosha kwa maji. Mungu alitumiminia Roho Mtakatifu bila kipimo kwa njia ya Yesu Kristo, Mwokozi wetu, ili kwa neema yake tupate kukubaliwa kuwa waadilifu na kuupokea uhai wa milele tunaotumainia. Jambo hili ni kweli. Ninakutaka uyatilie mkazo mambo haya, ili wale wanaomwamini Mungu wawe na hamu ya kuutumia wakati wao katika kutenda mema, yaani mambo mazuri na ya kuwafaa watu.
Tito 3:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Uwakumbushe watu kunyenyekea kwa watawala na wenye mamlaka, na kutii, na kuwa tayari kwa kila kazi njema; wasimtukane mtu yeyote, wasiwe wagomvi, wawe wema, wakiwa wapole sana kwa watu wote. Maana hapo zamani sisi nasi tulikuwa hatuna akili, tulikuwa waasi, tumedanganywa, huku tukitumikia tamaa na anasa za namna nyingi, tukiishi katika uovu na husuda, tukichukiza na kuchukiana. Lakini wema wake Mungu Mwokozi wetu, na upendo wake kwa wanadamu, ulipofunuliwa, alituokoa; si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa mara ya pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu; ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu; ili tukihesabiwa haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu. Ni neno la kuaminiwa; na mambo hayo nataka uyasisitizie sana, ili wale waliomwamini Mungu wakumbuke kudumu katika matendo mema. Mambo hayo ni mazuri sana, tena yana manufaa kwa wanadamu.
Tito 3:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Uwakumbushe watu kunyenyekea kwa wenye uwezo na mamlaka, na kutii, na kuwa tayari kwa kila kazi njema; wasimtukane mtu ye yote, wasiwe wagomvi, wawe wema, wakionyesha upole wote kwa watu wote. Maana hapo zamani sisi nasi tulikuwa hatuna akili, tulikuwa waasi, tumedanganywa, huku tukitumikia tamaa na anasa za namna nyingi, tukiishi katika uovu na husuda, tukichukiza na kuchukiana. Lakini wema wake Mwokozi wetu Mungu, na upendo wake kwa wanadamu, ulipofunuliwa, alituokoa; si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu; ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu; ili tukihesabiwa haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu. Ni neno la kuaminiwa; na mambo hayo nataka uyanene kwa nguvu, ili wale waliomwamini Mungu wakumbuke kudumu katika matendo mema. Hayo ni mazuri, tena yana faida kwa wanadamu.
Tito 3:1-8 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Wakumbushe watu kunyenyekea kwa watawala na kwa wenye mamlaka, na kutii, wakiwa tayari kutenda kila lililo jema, wasimnenee mtu yeyote mabaya, wasiwe wagomvi bali wawe wema, wakiwa wapole kwa watu wote. Maana sisi wenyewe wakati fulani tulikuwa wajinga, wasiotii, tukiwa watumwa wa tamaa mbaya na anasa za kila aina. Tuliishi katika uovu na wivu, tukichukiwa na kuchukiana sisi kwa sisi. Lakini wema na upendo wa Mungu Mwokozi wetu ulipofunuliwa, alituokoa, si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyotenda, bali kwa sababu ya rehema zake. Alituokoa kwa kutuosha kwa kuzaliwa mara ya pili na kwa kufanywa wapya kupitia kwa Roho Mtakatifu, ambaye Mungu alitumiminia kwa wingi kupitia kwa Yesu Kristo Mwokozi wetu, ili, tukiisha kuhesabiwa haki kwa neema yake, tupate kuwa warithi tukiwa na tumaini la uzima wa milele. Hili ni neno la kuaminiwa. Nami nataka uyasisitize mambo haya, ili wale ambao wamemwamini Mungu wapate kuwa waangalifu kujitoa kwa ajili ya kutenda mema wakati wote. Mambo haya ni mazuri tena ya manufaa kwa kila mtu.