Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Tito 2:1-15

Tito 2:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)

Lakini wewe unapaswa kuhubiri mafundisho sahihi. Waambie wanaume wazee kwamba wanapaswa kuwa na kiasi, wawe na busara na wataratibu; wanapaswa kuwa timamu katika imani yao, upendo na uvumilivu. Hali kadhalika waambie wanawake wazee wawe na mwenendo wa uchaji wa Mungu; wasiwe wachongezi au watumwa wa pombe. Wanapaswa kufundisha mambo mema, ili wawazoezeshe kina mama vijana kuwapenda waume zao na watoto, wawe na kiasi na safi, waangalie vizuri mambo ya nyumbani, na wawatii waume zao, ili ujumbe wa Mungu usije ukadharauliwa. Kadhalika, wahimize vijana wawe na kiasi. Katika mambo yote wewe mwenyewe unapaswa kuwa mfano wa matendo mema. Uwe mnyofu na uwe na uzito katika mafundisho yako. Maneno yako yasiwe na hitilafu yoyote ili maadui zako waaibike wasipopata chochote kibaya cha kusema juu yetu. Watumwa wanapaswa kuwatii wakuu wao na kuwapendeza katika mambo yote. Wasibishane nao, au kuiba vitu vyao. Badala yake wanapaswa kuonesha kwamba wao ni wema na waaminifu daima, ili, kwa matendo yao yote, wayapatie sifa njema mafundisho juu ya Mungu, Mwokozi wetu. Maana neema ya Mungu imedhihirishwa kwa ajili ya wokovu wa watu wote. Neema hiyo yatufunza kuachana na uovu wote na tamaa za kidunia; tuwe na kiasi, tuishi maisha adili na ya kumcha Mungu katika ulimwengu huu wa sasa, tukiwa tunangojea siku ile ya heri tunayoitumainia, wakati utakapotokea utukufu wa Mungu Mkuu na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Yeye alijitoa mwenyewe kwa ajili yetu ili atukomboe kutoka katika uovu wote na kutufanya watu safi walio wake yeye mwenyewe, watu walio na hamu ya kutenda mema. Basi, sema mambo hayo na tumia mamlaka yako yote ukiwahimiza na kuwaonya wasikilizaji wako. Mtu yeyote na asikudharau.

Shirikisha
Soma Tito 2

Tito 2:1-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Lakini wewe, nena mambo yanayoambatana na mafundisho mema; ya kwamba wazee wawe wenye kiasi, wastahivu, wenye busara, wazima katika imani na katika upendo na katika subira. Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wanaofundisha yaliyo mema; ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao; na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe. Vivyo hivyo na vijana waume uwaonye kuwa na kiasi; katika mambo yote ukijionesha wewe mwenyewe kuwa kielelezo cha matendo mema, na katika mafundisho yako ukionesha usahihi na ustahivu, na maneno yafaayo yasiyoweza kuhukumiwa makosa, ili yule mwenye kupinga atahayarike, kwa kuwa hana neno baya la kunena juu yetu. Watumwa na wawatii bwana zao, wakiwapendeza katika mambo yote; wasiwe wakaidi, wasiwe wezi; bali wauoneshe uaminifu mwema wote, ili wayapambe mafundisho ya Mungu aliye Mwokozi wetu katika mambo yote. Maana neema ya Mungu iwaokoao wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa; tukilitazamia tumaini lenye baraka na kufunuliwa kwa utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu; ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wake mwenyewe walio na bidii katika matendo mema. Nena mambo hayo, onya na kukaripia kwa mamlaka yote; asikudharau mtu awaye yote.

Shirikisha
Soma Tito 2

Tito 2:1-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Lakini wewe nena mambo yapasayo mafundisho yenye uzima; ya kwamba wazee wawe wenye kiasi, wastahivu, wenye busara, wazima katika imani na katika upendo na katika saburi. Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema; ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao; na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe. Vivyo hivyo na vijana waume uwaonye kuwa na kiasi; katika mambo yote ukijionyesha wewe mwenyewe kuwa kielelezo cha matendo mema, na katika mafundisho yako ukionyesha usahihi na ustahivu, na maneno yenye uzima yasiyoweza kuhukumiwa makosa, ili yule mwenye kupinga atahayarike, kwa kuwa hana neno baya la kunena juu yetu. Watumwa na wawatii bwana zao, wakiwapendeza katika mambo yote; wasiwe wenye kujibu, wasiwe waibaji; bali wauonyeshe uaminifu mwema wote, ili wayapambe mafundisho ya Mwokozi wetu Mungu katika mambo yote. Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa; tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu; ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema. Nena maneno hayo, onya na kukaripia kwa mamlaka yote; asikudharau mtu awaye yote.

Shirikisha
Soma Tito 2

Tito 2:1-15 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Inakupasa kufundisha itikadi sahihi. Wafundishe wazee kuwa na kiasi, wastahivu, wenye busara na wanyofu katika imani, upendo na saburi. Vivyo hivyo, wafundishe wanawake wazee kuwa na mwenendo wa utakatifu, wala wasiwe wasingiziaji au walevi, bali wafundishe yale yaliyo mema, ili waweze kuwafundisha wanawake vijana kuwa na kiasi, wawapende waume zao na kuwapenda watoto wao, wawe waaminifu, watakatifu, wakitunza vyema nyumba zao, wema, watiifu kwa waume zao, ili mtu yeyote asije akalikufuru neno la Mungu. Vivyo hivyo, himiza vijana wawe na kiasi. Katika kila jambo uwe kielelezo kwa kutenda mema. Katika mafundisho yako uonyeshe uadilifu, utaratibu, na usemi sahihi usio na lawama, ili wanaokupinga watahayari, wakose neno lolote baya la kusema juu yetu. Wafundishe watumwa kuwatii mabwana zao katika kila jambo, wakijitahidi kuwapendeza wala wasijibizane nao, wala wasiwaibie, bali waonyeshe kuwa wanaweza kuaminika kabisa, ili kwa kila namna wayafanye mafundisho ya Mungu Mwokozi wetu yawe ya kuvutia. Kwa maana neema ya Mungu ambayo inawaokoa wanadamu wote imefunuliwa. Nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia, ili tupate kuishi maisha ya kiasi, ya haki na ya utaua katika ulimwengu huu wa sasa, huku tukilitazamia tumaini lenye baraka na ufunuo wa utukufu wa Mungu wetu Mkuu, aliye Mwokozi wetu Yesu Kristo. Ndiye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe kutoka uovu wote na kujisafishia watu kuwa mali yake Mwenyewe, yaani, wale walio na juhudi katika kutenda mema. Basi wewe fundisha mambo haya. Onya na kukaripia kwa mamlaka yote. Mtu yeyote asikudharau.

Shirikisha
Soma Tito 2

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha