Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ruthu 1:6-18

Ruthu 1:6-18 Biblia Habari Njema (BHN)

Baadaye, Naomi alipata habari kwamba Mwenyezi-Mungu alikuwa amewabariki watu wake kwa kuwapa chakula. Basi, akaondoka kutoka Moabu kurudi kwao pamoja na wakwe zake. Akaondoka mahali pale alipoishi pamoja na wakwe zake, wakashika njia ya kurudi Yuda. Naye Naomi akawaambia hao wakwe zake wawili, “Rudini kila mmoja nyumbani kwa mama yake. Naomba Mwenyezi-Mungu awe mwema kwenu kama mlivyokuwa wema kwangu na kwa wale watu wangu waliofariki. Mwenyezi-Mungu awajalie, kila mmoja wenu apate mume na nyumba yake.” Kisha Naomi akawaaga kwa kuwabusu. Lakini wao walianza kulia kwa sauti na kumwambia, “La hasha! Tutakwenda pamoja nawe kwa watu wako.” Naye Naomi akawasihi, “Rudini, binti zangu. Kwa nini kunifuata? Je, mnafikiri naweza kupata tena watoto watakaokuwa waume zenu? Rudini nyumbani kwenu binti zangu, kwa maana mimi ni mzee mno, siwezi kuolewa tena. Hata kama ningesema ninalo tumaini, na hata kama ningepata mume usiku huu na kupata watoto, je, mngeweza kungoja mpaka wakue? Je, mngeweza kujizuia msiolewe na waume wengine? Sivyo, binti zangu! Mambo yangu ni magumu mno kwa ajili yenu, maana Mwenyezi-Mungu amenipiga kipigo.” Hapo walipaza sauti wakaanza kulia tena. Ndipo Orpa akamkumbatia mkwewe, akamuaga na kurudi nyumbani; lakini Ruthu, akaandamana naye. Basi Naomi akamwambia, “Ruthu, tazama dada yako amerudi nyumbani kwake na kwa mungu wake; basi, nawe pia urudi, umfuate dada yako.” Lakini Ruthu akamjibu, “Usinisihi nikuache wewe, wala usinizuie kufuatana nawe. Kokote utakakokwenda ndiko nami nitakakokwenda, na ukaapo nitakaa, watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako atakuwa Mungu wangu. Pale utakapofia hapo nitakufa nami, na papo hapo nitazikwa; Mwenyezi-Mungu anipe adhabu kali kama nikitenganishwa nawe isipokuwa tu kwa kifo.” Naomi alipoona kuwa Ruthu ameamua kwenda pamoja naye, aliacha kumshawishi.

Shirikisha
Soma Ruthu 1

Ruthu 1:6-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ndipo alipoondoka, yeye na wakweze, ili kurudi kutoka nchi ya Moabu; maana akiwa katika nchi ya Moabu alipata habari kuwa BWANA alikuwa amewajia watu wake na kuwapa chakula. Basi akatoka pale alipokuwa akiishi, na wakweze wawili pamoja naye; wakashika njia ili kurudi mpaka nchi ya Yuda. Kisha Naomi akawaambia wakweze wawili, Nendeni sasa mkarejee kila mmoja nyumbani kwa mamaye; BWANA na awatendee mema ninyi, kama ninyi mlivyowatendea mema hao waliofariki na mimi pia. BWANA na awajalie kuona raha kila mmoja nyumbani kwa mumewe. Kisha akawabusu; nao wakapaza sauti zao wakalia. Wakamwambia, La, sivyo; lakini tutarudi pamoja nawe kwa watu wako. Naye Naomi akasema, Enyi wanangu, rudini; kwa nini mfuatane nami? Je! Mimi ninao watoto wa kiume tena tumboni mwangu, hata wawe waume zenu? Enyi wanangu, mrejee; nendeni zenu; kwa kuwa mimi ni mzee, siwezi kupata mume tena. Kama ningesema, Natumaini; kama ningepata mume hata usiku huu, na kuzaa watoto wa kiume; je! Mngesubiri hata watakapokuwa watu wazima? Mngejizuia msiwe na waume? La, sivyo, wanangu; maana ni vigumu kwangu kuliko kwenu, kwa sababu mkono wa BWANA umetoka juu yangu. Nao wakapaza sauti zao, wakalia tena, na Orpa akambusu mkwewe, lakini Ruthu akaambatana naye. Naye akasema, Tazama, dada yako amerudi kwa watu wake, na kwa mungu wake; basi urudi nawe ukamfuate dada yako. Naye Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirudi nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu; Pale utakapofia ndipo nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa; BWANA anitende vivyo hivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami. Basi alipomwona kuwa amekata shauri kufuatana naye, aliacha kumshawishi.

Shirikisha
Soma Ruthu 1

Ruthu 1:6-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ndipo alipoondoka, yeye na wakweze, ili kurudi kutoka nchi ya Moabu; maana huko katika nchi ya Moabu amesikia ya kwamba BWANA amewajilia watu wake na kuwapa chakula. Basi akatoka pale alipokuwapo, na wakweze wawili pamoja naye; wakashika njia ili kurudi mpaka nchi ya Yuda. Kisha Naomi akawaambia wakweze wawili, Nendeni sasa mkarejee kila mmoja nyumbani kwa mamaye; BWANA na awatendee mema ninyi, kama ninyi mlivyowatendea mema hao waliofariki na mimi pia. BWANA na awajalie kuona raha kila mmoja nyumbani kwa mumewe. Kisha akawabusu; nao wakapaza sauti zao wakalia. Wakamwambia, La, sivyo; lakini tutarudi pamoja nawe kwa watu wako. Naye Naomi akasema, Enyi wanangu, mrejee; kwani kufuatana na mimi? Je! Mimi ninao watoto wa kiume tena tumboni mwangu, hata wawe waume zenu? Enyi wanangu, mrejee; nendeni zenu; kwa kuwa mimi ni mzee, siwezi kupata mume tena. Kama ningesema, Natumaini; kama ningepata mume hata usiku huu, na kuzaa watoto wa kiume; je! Mngesubiri hata watakapokuwa watu wazima? Mngejizuia msiwe na waume? La, sivyo, wanangu; maana ni vigumu kwangu kuliko kwenu, kwa sababu mkono wa BWANA umetoka juu yangu. Nao wakapaza sauti zao, wakalia tena, na Orpa akambusu mkwewe, lakini Ruthu akaambatana naye. Naye akasema, Tazama, shemeji yako amerejea kwa watu wake, na kwa mungu wake; basi urejee wewe umfuate shemeji yako. Naye Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu; Pale utakapokufa nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa; BWANA anitende vivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami. Basi alipomwona kuwa amekaza nia yake kufuatana naye, aliacha kusema naye.

Shirikisha
Soma Ruthu 1

Ruthu 1:6-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Aliposikia akiwa huko Moabu kwamba BWANA amewasaidia watu wake kwa kuwapa chakula, Naomi na wakwe wake wakajiandaa kurudi nyumbani. Yeye na wakwe wake wawili wakaondoka pale walipokuwa wakiishi na kushika njia kurudi nchi ya Yuda. Ndipo Naomi akawaambia wale wakwe wake wawili, “Rudini, kila mmoja wenu nyumbani mwa mama yake. BWANA na awatendee mema kama mlivyowatendea hao waliofariki, na mimi pia. BWANA na amjalie kila mmoja wenu maisha mema nyumbani mwa mume mwingine.” Kisha akawabusu, nao wakalia kwa sauti kubwa, wakamwambia, “Tutarudi pamoja na wewe kwa watu wako.” Lakini Naomi akasema, “Rudini nyumbani, binti zangu. Kwa nini mnifuate? Je, mimi nitaweza tena kuwa na wana wengine ambao wataweza kuwaoa ninyi? Rudini nyumbani, binti zangu; mimi ni mzee kiasi kwamba siwezi kumpata mume mwingine. Hata kama ningefikiria kuwa bado kuna tumaini kwangu, hata kama ningekuwa na mume usiku huu na kuwazaa wana, je, mngesubiri hadi wakue? Mngebakia bila kuolewa mkiwasubiri? La, hasha, binti zangu. Nimepata uchungu kuliko ninyi, kwa sababu mkono wa BWANA umekuwa kinyume nami!” Kisha wakalia tena kwa sauti. Orpa akambusu mama mkwe wake, akaenda zake, lakini Ruthu akaambatana naye. Naomi akamwambia, “Tazama, mwenzako anarejea kwa watu wake na kwa miungu yake. Rudi pamoja naye.” Lakini Ruthu akajibu, “Usinisihi nikuache au niache kukufuata. Utakakoenda nami nitaenda, na wewe utakapoishi nitaishi. Watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako atakuwa Mungu wangu. Pale utakapofia nami nitafia hapo, na papo hapo nitazikwa. BWANA na aniadhibu vikali, kama kitu kingine chochote kitanitenga nawe isipokuwa kifo.” Naomi alipotambua kwamba Ruthu amenuia kufuatana naye, hakuendelea kumsihi tena.

Shirikisha
Soma Ruthu 1