Ruthu 1:16-21
Ruthu 1:16-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini Ruthu akamjibu, “Usinisihi nikuache wewe, wala usinizuie kufuatana nawe. Kokote utakakokwenda ndiko nami nitakakokwenda, na ukaapo nitakaa, watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako atakuwa Mungu wangu. Pale utakapofia hapo nitakufa nami, na papo hapo nitazikwa; Mwenyezi-Mungu anipe adhabu kali kama nikitenganishwa nawe isipokuwa tu kwa kifo.” Naomi alipoona kuwa Ruthu ameamua kwenda pamoja naye, aliacha kumshawishi. Ndipo wote wawili wakaendelea na safari hadi Bethlehemu. Walipofika huko, watu wote walishangaa, hata wanawake wakaulizana, “Je, huyu ni Naomi?” Naomi akasema, “Msiniite tena Naomi niiteni Mara, kwa maana Mungu mwenye nguvu ameyafanya maisha yangu yawe machungu mno. Nilipoondoka hapa, nilikuwa na vitu vingi, lakini sasa Mwenyezi-Mungu amenirudisha mikono mitupu. Mbona mwaniita Naomi na hali Mwenyezi-Mungu ameniadhibu, naye Mungu Mwenye Nguvu amenitesa.”
Ruthu 1:16-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirudi nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu; Pale utakapofia ndipo nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa; BWANA anitende vivyo hivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami. Basi alipomwona kuwa amekata shauri kufuatana naye, aliacha kumshawishi. Hivyo hao wakaendelea wote wawili hadi walipofika Bethlehemu. Na ikawa walipofika Bethlehemu, mji wote uliwaajabia. Nao wanawake wakasema, Je! Huyu ni Naomi? Akawaambia, Msiniite Naomi, niiteni Mara kwa sababu Mwenyezi Mungu amenitenda mambo machungu sana. Mimi nilitoka nikiwa nimejaa, naye BWANA amenirudisha sina kitu, kwani kuniita Naomi, ikiwa BWANA ameshuhudia juu yangu, na Mwenyezi Mungu amenitesa?
Ruthu 1:16-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu; Pale utakapokufa nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa; BWANA anitende vivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami. Basi alipomwona kuwa amekaza nia yake kufuatana naye, aliacha kusema naye. Hivyo hao wakaendelea wote wawili hata walipofika Bethlehemu. Na ikawa walipofika Bethlehemu, mji wote ulitaharuki kwa habari zao. Nao wanawake wakasema, Je! Huyu ni Naomi? Akawaambia, Msiniite Naomi, niiteni Mara, kwa sababu Mwenyezi Mungu amenitenda mambo machungu sana. Mimi nalitoka hali nimejaa, naye BWANA amenirudisha sina kitu, kwani kuniita Naomi, ikiwa BWANA ameshuhudia juu yangu, na Mwenyezi Mungu amenitesa?
Ruthu 1:16-21 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Lakini Ruthu akajibu, “Usinisihi nikuache au niache kukufuata. Utakakoenda nami nitaenda, na wewe utakapoishi nitaishi. Watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako atakuwa Mungu wangu. Pale utakapofia nami nitafia hapo, na papo hapo nitazikwa. BWANA na aniadhibu vikali, kama kitu kingine chochote kitanitenga nawe isipokuwa kifo.” Naomi alipotambua kwamba Ruthu amenuia kufuatana naye, hakuendelea kumsihi tena. Kwa hiyo hao wanawake wawili wakaondoka, wakafika Bethlehemu. Walipofika Bethlehemu, mji mzima ulitaharuki, wanawake wakashangaa, wakasema, “Huyu aweza kuwa ni Naomi?” Akawaambia, “Msiniite tena Naomi; niiteni Mara, kwa sababu Mwenyezi amenitendea mambo machungu sana. Mimi niliondoka hali nimejaa, lakini BWANA amenirudisha mtupu. Kwa nini kuniita Naomi? BWANA amenitendea mambo machungu; Mwenyezi ameniletea msiba.”