Ruthu 1:14-18
Ruthu 1:14-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Hapo walipaza sauti wakaanza kulia tena. Ndipo Orpa akamkumbatia mkwewe, akamuaga na kurudi nyumbani; lakini Ruthu, akaandamana naye. Basi Naomi akamwambia, “Ruthu, tazama dada yako amerudi nyumbani kwake na kwa mungu wake; basi, nawe pia urudi, umfuate dada yako.” Lakini Ruthu akamjibu, “Usinisihi nikuache wewe, wala usinizuie kufuatana nawe. Kokote utakakokwenda ndiko nami nitakakokwenda, na ukaapo nitakaa, watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako atakuwa Mungu wangu. Pale utakapofia hapo nitakufa nami, na papo hapo nitazikwa; Mwenyezi-Mungu anipe adhabu kali kama nikitenganishwa nawe isipokuwa tu kwa kifo.” Naomi alipoona kuwa Ruthu ameamua kwenda pamoja naye, aliacha kumshawishi.
Ruthu 1:14-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nao wakapaza sauti zao, wakalia tena, na Orpa akambusu mkwewe, lakini Ruthu akaambatana naye. Naye akasema, Tazama, dada yako amerudi kwa watu wake, na kwa mungu wake; basi urudi nawe ukamfuate dada yako. Naye Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirudi nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu; Pale utakapofia ndipo nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa; BWANA anitende vivyo hivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami. Basi alipomwona kuwa amekata shauri kufuatana naye, aliacha kumshawishi.
Ruthu 1:14-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nao wakapaza sauti zao, wakalia tena, na Orpa akambusu mkwewe, lakini Ruthu akaambatana naye. Naye akasema, Tazama, shemeji yako amerejea kwa watu wake, na kwa mungu wake; basi urejee wewe umfuate shemeji yako. Naye Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu; Pale utakapokufa nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa; BWANA anitende vivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami. Basi alipomwona kuwa amekaza nia yake kufuatana naye, aliacha kusema naye.
Ruthu 1:14-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kisha wakalia tena kwa sauti. Orpa akambusu mama mkwe wake, akaenda zake, lakini Ruthu akaambatana naye. Naomi akamwambia, “Tazama, mwenzako anarejea kwa watu wake na kwa miungu yake. Rudi pamoja naye.” Lakini Ruthu akajibu, “Usinisihi nikuache au niache kukufuata. Utakakoenda nami nitaenda, na wewe utakapoishi nitaishi. Watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako atakuwa Mungu wangu. Pale utakapofia nami nitafia hapo, na papo hapo nitazikwa. BWANA na aniadhibu vikali, kama kitu kingine chochote kitanitenga nawe isipokuwa kifo.” Naomi alipotambua kwamba Ruthu amenuia kufuatana naye, hakuendelea kumsihi tena.