Ruthu 1:11-16
Ruthu 1:11-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Naye Naomi akawasihi, “Rudini, binti zangu. Kwa nini kunifuata? Je, mnafikiri naweza kupata tena watoto watakaokuwa waume zenu? Rudini nyumbani kwenu binti zangu, kwa maana mimi ni mzee mno, siwezi kuolewa tena. Hata kama ningesema ninalo tumaini, na hata kama ningepata mume usiku huu na kupata watoto, je, mngeweza kungoja mpaka wakue? Je, mngeweza kujizuia msiolewe na waume wengine? Sivyo, binti zangu! Mambo yangu ni magumu mno kwa ajili yenu, maana Mwenyezi-Mungu amenipiga kipigo.” Hapo walipaza sauti wakaanza kulia tena. Ndipo Orpa akamkumbatia mkwewe, akamuaga na kurudi nyumbani; lakini Ruthu, akaandamana naye. Basi Naomi akamwambia, “Ruthu, tazama dada yako amerudi nyumbani kwake na kwa mungu wake; basi, nawe pia urudi, umfuate dada yako.” Lakini Ruthu akamjibu, “Usinisihi nikuache wewe, wala usinizuie kufuatana nawe. Kokote utakakokwenda ndiko nami nitakakokwenda, na ukaapo nitakaa, watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako atakuwa Mungu wangu.
Ruthu 1:11-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye Naomi akasema, Enyi wanangu, rudini; kwa nini mfuatane nami? Je! Mimi ninao watoto wa kiume tena tumboni mwangu, hata wawe waume zenu? Enyi wanangu, mrejee; nendeni zenu; kwa kuwa mimi ni mzee, siwezi kupata mume tena. Kama ningesema, Natumaini; kama ningepata mume hata usiku huu, na kuzaa watoto wa kiume; je! Mngesubiri hata watakapokuwa watu wazima? Mngejizuia msiwe na waume? La, sivyo, wanangu; maana ni vigumu kwangu kuliko kwenu, kwa sababu mkono wa BWANA umetoka juu yangu. Nao wakapaza sauti zao, wakalia tena, na Orpa akambusu mkwewe, lakini Ruthu akaambatana naye. Naye akasema, Tazama, dada yako amerudi kwa watu wake, na kwa mungu wake; basi urudi nawe ukamfuate dada yako. Naye Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirudi nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu
Ruthu 1:11-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye Naomi akasema, Enyi wanangu, mrejee; kwani kufuatana na mimi? Je! Mimi ninao watoto wa kiume tena tumboni mwangu, hata wawe waume zenu? Enyi wanangu, mrejee; nendeni zenu; kwa kuwa mimi ni mzee, siwezi kupata mume tena. Kama ningesema, Natumaini; kama ningepata mume hata usiku huu, na kuzaa watoto wa kiume; je! Mngesubiri hata watakapokuwa watu wazima? Mngejizuia msiwe na waume? La, sivyo, wanangu; maana ni vigumu kwangu kuliko kwenu, kwa sababu mkono wa BWANA umetoka juu yangu. Nao wakapaza sauti zao, wakalia tena, na Orpa akambusu mkwewe, lakini Ruthu akaambatana naye. Naye akasema, Tazama, shemeji yako amerejea kwa watu wake, na kwa mungu wake; basi urejee wewe umfuate shemeji yako. Naye Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu
Ruthu 1:11-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Lakini Naomi akasema, “Rudini nyumbani, binti zangu. Kwa nini mnifuate? Je, mimi nitaweza tena kuwa na wana wengine ambao wataweza kuwaoa ninyi? Rudini nyumbani, binti zangu; mimi ni mzee kiasi kwamba siwezi kumpata mume mwingine. Hata kama ningefikiria kuwa bado kuna tumaini kwangu, hata kama ningekuwa na mume usiku huu na kuwazaa wana, je, mngesubiri hadi wakue? Mngebakia bila kuolewa mkiwasubiri? La, hasha, binti zangu. Nimepata uchungu kuliko ninyi, kwa sababu mkono wa BWANA umekuwa kinyume nami!” Kisha wakalia tena kwa sauti. Orpa akambusu mama mkwe wake, akaenda zake, lakini Ruthu akaambatana naye. Naomi akamwambia, “Tazama, mwenzako anarejea kwa watu wake na kwa miungu yake. Rudi pamoja naye.” Lakini Ruthu akajibu, “Usinisihi nikuache au niache kukufuata. Utakakoenda nami nitaenda, na wewe utakapoishi nitaishi. Watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako atakuwa Mungu wangu.