Waroma 9:1-33
Waroma 9:1-33 Biblia Habari Njema (BHN)
Nasema ukweli tupu; nimeungana na Kristo nami sisemi uongo. Dhamiri yangu ikiongozwa na Roho Mtakatifu inanithibitishia jambo hili pia. Nataka kusema hivi: Nina huzuni kubwa na maumivu yasiyopimika moyoni mwangu kwa ajili ya ndugu zangu walio wa taifa langu! Kama ingekuwa kwa faida yao, ningekuwa radhi kulaaniwa na kutengwa na Kristo. Hao ndio watu wa Israeli ambao Mungu aliwateua wawe watoto wake, akawashirikisha utukufu wake; alifanya nao maagano, akawapa sheria yake, imani ya kweli na ahadi zake. Wao ni wajukuu wa mababu, naye Kristo, kadiri ya ubinadamu wake, ametoka katika ukoo wao. Mungu atawalaye juu ya yote, na atukuzwe milele! Amina. Sisemi kwamba ahadi ya Mungu imebatilika; maana si watu wote wa Israeli ni wateule wa Mungu. Wala si wazawa wote wa Abrahamu ni watoto wake wa kweli. Ila, kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Wazawa wake watatokana na Isaka.” Ndiyo kusema, si wale waliozaliwa kimaumbile ndio watoto wa Mungu, bali wale waliozaliwa kutokana na ahadi ya Mungu ndio watakaoitwa watoto wake. Maana ahadi yenyewe ni hii: “Wakati maalumu nitarudi, naye Sara atapata mtoto.” Tena si hayo tu, ila pia Rebeka naye alipata mapacha kwa baba mmoja, yaani Isaka, babu yetu. Lakini, ili Mungu aonekane kwamba anao uhuru wa kuchagua, hata kabla wale ndugu hawajazaliwa na kabla hawajaweza kupambanua jema na baya, Rebeka aliambiwa kwamba yule mtoto wa kwanza atamtumikia yule wa nyuma. Hivyo uchaguzi wa Mungu unategemea jinsi anavyoita mwenyewe, na si matendo ya binadamu. Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Yakobo nilimpenda, lakini Esau nilimchukia.” Basi, tuseme nini? Je, Mungu amekosa haki? Hata kidogo! Maana alimwambia Mose: “Nitamhurumia mtu yeyote ninayetaka kumhurumia; nitamwonea huruma mtu yeyote ninayetaka.” Kwa hiyo, yote hutegemea huruma ya Mungu, na si bidii au mapenzi ya mtu. Maana Maandiko Matakatifu yasema hivi kwa Farao: “Nilikufanya mfalme ili kwa njia yako, uwezo wangu ujulikane, na jina langu litangazwe popote duniani.” Ni wazi basi, kwamba Mungu humhurumia yeyote anayetaka kumhurumia, na akipenda kumfanya mtu awe mkaidi, hufanya hivyo. Labda utaniuliza: “Ikiwa mambo yako hivyo, Mungu anawezaje kumlaumu mtu? Nani awezaye kuyapinga mapenzi yake?” Lakini, ewe binadamu, u nani hata uthubutu kumhoji Mungu? Je, chungu chaweza kumwuliza mfinyanzi wake: “Kwa nini umenitengeneza namna hii?” Mfinyanzi anaweza kuutumia udongo apendavyo na kufinyanga vyungu viwili kwa udongo uleule; kimoja kwa matumizi ya heshima, na kingine kwa matumizi ya kawaida. Hivyo ndivyo ilivyo kwa Mungu. Alitaka kuonesha ghadhabu yake na kujulisha uwezo wake. Basi, alikuwa na saburi sana, akiwavumilia wale ambao walikuwa lengo la ghadhabu yake, ambao walistahili kuangamizwa. Alitaka pia kudhihirisha wingi wa utukufu wake ambao alitumiminia sisi tulio lengo la huruma yake; sisi ambao alikwisha kututayarisha kuupokea utukufu wake. Maana sisi ndio hao aliowaita, si kutoka miongoni mwa Wayahudi tu bali pia kutoka kwa watu wa mataifa mengine. Maana ndivyo asemavyo katika kitabu cha Hosea: “Wale waliokuwa ‘Si watu wangu’ nitawaita: ‘Watu wangu!’ Naye ‘Sikupendi’ ataitwa: ‘Mpenzi wangu!’ Na pale walipoambiwa: ‘Nyinyi si wangu’ hapo wataitwa: ‘Watoto wa Mungu aliye hai.’” Naye nabii Isaya, kuhusu Israeli anapaza sauti: “Hata kama wazawa wa Israeli ni wengi kama mchanga wa pwani, ni wachache tu watakaookolewa; maana, Bwana ataitekeleza upesi hukumu yake kamili juu ya ulimwengu wote.” Ni kama Isaya alivyosema hapo awali: “Bwana wa majeshi asingalituachia baadhi ya watoto wa Israeli, tungalikwisha kuwa kama Sodoma, tungalikwisha kuwa kama Gomora.” Basi tuseme nini? Watu wa mataifa ambao hawakutafuta wafanywe waadilifu, wamejaliwa kuwa waadilifu, kwa njia ya imani, hali watu wa Israeli ambao walitafuta sheria ya kuwafanya kuwa waadilifu, hawakuipata. Kwa nini? Kwa sababu walitegemea matendo yao badala ya kutegemea imani. Walijikwaa juu ya jiwe la kujikwaa kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Tazama, nitaweka huko Siyoni jiwe likwazalo, mwamba utakaowafanya watu waanguke. Lakini atakayemwamini hataaibishwa!”
Waroma 9:1-33 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nasema kweli katika Kristo, sisemi uongo, dhamiri yangu ikinishuhudia katika Roho Mtakatifu, ya kwamba nina huzuni nyingi na maumivu yasiyoisha moyoni mwangu. Kwa maana ningeweza kuomba mimi mwenyewe niharimishwe na kutengwa na Kristo kwa ajili ya ndugu zangu, jamaa zangu kwa jinsi ya mwili; ambao ni Waisraeli, wenye kule kufanywa wana, na ule utukufu, na maagano, na kupewa torati, na ibada ya Mungu, na ahadi zake; ambao mababu ni wao, na katika hao alitoka Kristo kwa jinsi ya mwili. Ndiye aliye juu ya mambo yote, Mungu, mwenye kuhimidiwa milele. Amina. Si kana kwamba neno la Mungu limetanguka. Maana hawawi wote Waisraeli walio wa uzao wa Israeli. Wala hawawi wote wana kwa kuwa wazawa wa Abrahamu, bali, Katika Isaka wazawa wako wataitwa; yaani, si watoto wa mwili walio watoto wa Mungu, bali watoto wa ile ahadi wanahesabiwa kuwa wazawa. Kwa maana neno la ahadi ni hili, Panapo wakati huu nitakuja, na Sara atapata mtoto wa kiume. Wala si hivyo tu, lakini Rebeka naye, akiisha kuchukua mimba kwa mume mmoja, naye ni Isaka, baba yetu, (kwa maana kabla hawajazaliwa wale watoto, wala hawajatenda neno jema wala baya, ili lisimame kusudi la Mungu la kuchagua, si kwa sababu ya matendo, bali kwa sababu ya nia yake aitaye), aliambiwa hivi, Mkubwa atamtumikia mdogo. Kama ilivyoandikwa, Nimempenda Yakobo, bali Esau nimemchukia. Tuseme nini basi? Kuna udhalimu kwa Mungu? La hasha! Maana amwambia Musa, Nitamrehemu yeye nimrehemuye, nitamhurumia yeye nimhurumiaye. Basi, kama ni hivyo, si katika uwezo wa yule atakaye, wala wa yule apigaye mbio; bali wa yule arehemuye, yaani, Mungu. Kwa maana Maandiko yasema juu ya Farao, ya kwamba, Nilikusimamisha kwa kusudi hili, ili nioneshe nguvu zangu kwako, jina langu likatangazwe katika nchi yote. Basi, kama ni hivyo, atakaye kumrehemu humrehemu, na atakaye kumfanya mgumu humfanya mgumu. Basi, utaniambia, Mbona angali akilaumu? Kwa maana ni nani ashindanaye na kusudi lake? La! Sivyo, Ee binadamu; wewe u nani umjibuye Mungu? Je! Kitu kilichoumbwa kimwambie yeye aliyekiumba, Kwa nini umeniumba hivi? Au mfinyanzi je! Hana amri juu ya udongo, kwa fungu moja la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima, na kimoja kiwe hakina heshima? Ni nini basi, ikiwa Mungu kwa kutaka kuonesha ghadhabu yake, na kuudhihirisha uweza wake, kwa uvumilivu mwingi, alichukuliana na vile vyombo vya ghadhabu vilivyokuwa karibu kuharibiwa; tena, ili audhihirishe wingi wa utukufu wake katika vile vyombo vya rehema, alivyovitengeneza tangu zamani vipate utukufu; ndio sisi aliotuita, si watu wa Wayahudi tu, ila na watu wa Mataifa pia? Ni kama vile alivyosema katika Hosea, Nitawaita watu wangu wale wasiokuwa watu wangu, Na kumwita mpenzi wangu yeye asiyekuwa mpenzi wangu. Tena itakuwa mahali pale walipoambiwa, Ninyi si watu wangu, Hapo wataitwa wana wa Mungu aliye hai. Isaya naye atoa sauti yake juu ya Israeli, kusema, Hesabu ya wana wa Israeli, ijapokuwa ni kama mchanga wa bahari, ni mabaki yao tu watakaookolewa. Kwa maana Bwana atalitekeleza neno lake juu ya nchi, akilimaliza na kulikata. Tena kama Isaya alivyotangulia kunena, Kama Bwana wa majeshi asingalituachia uzao, Tungalikuwa kama Sodoma, tungalifananishwa na Gomora. Tuseme nini, basi? Ya kwamba watu wa Mataifa, wasioifuata haki, walipata haki; lakini ni ile haki iliyo ya imani; bali Israeli wakiifuata sheria ya haki hawakuifikia ile sheria. Kwa sababu gani? Kwa sababu hawakuifuata kwa njia ya imani, bali kana kwamba kwa njia ya matendo. Wakajikwaa juu ya jiwe lile likwazalo, kama ilivyoandikwa, Tazama, naweka katika Sayuni jiwe likwazalo, na mwamba uangushao; Na kila amwaminiye hatatahayarika.
Waroma 9:1-33 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nasema kweli katika Kristo, sisemi uongo, dhamiri yangu ikinishuhudia katika Roho Mtakatifu, ya kwamba nina huzuni nyingi na maumivu yasiyokoma moyoni mwangu. Kwa maana ningeweza kuomba mimi mwenyewe niharimishwe na kutengwa na Kristo kwa ajili ya ndugu zangu, jamaa zangu kwa jinsi ya mwili; ambao ni Waisraeli, wenye kule kufanywa wana, na ule utukufu, na maagano, na kupewa torati, na ibada ya Mungu, na ahadi zake; ambao mababu ni wao, na katika hao alitoka Kristo kwa jinsi ya mwili. Ndiye aliye juu ya mambo yote, Mungu, mwenye kuhimidiwa milele. Amina. Si kana kwamba neno la Mungu limetanguka. Maana hawawi wote Waisraeli walio wa uzao wa Israeli. Wala hawawi wote wana kwa kuwa wazao wa Ibrahimu, bali, Katika Isaka wazao wako wataitwa; yaani, si watoto wa mwili walio watoto wa Mungu, bali watoto wa ile ahadi wanahesabiwa kuwa wazao. Kwa maana neno la ahadi ni hili, Panapo wakati huu nitakuja, na Sara atakuwa na mwana. Wala si hivyo tu, lakini Rebeka naye, akiisha kuchukua mimba kwa mume mmoja, naye ni Isaka, baba yetu, (kwa maana kabla hawajazaliwa wale watoto, wala hawajatenda neno jema wala baya, ili lisimame kusudi la Mungu la kuchagua, si kwa sababu ya matendo, bali kwa sababu ya nia yake aitaye), aliambiwa hivi, Mkubwa atamtumikia mdogo. Kama ilivyoandikwa, Nimempenda Yakobo, bali Esau nimemchukia. Tuseme nini basi? Kuna udhalimu kwa Mungu? Hasha! Maana amwambia Musa, Nitamrehemu yeye nimrehemuye, nitamhurumia yeye nimhurumiaye. Basi, kama ni hivyo, si katika uwezo wa yule atakaye, wala wa yule apigaye mbio; bali wa yule arehemuye, yaani, Mungu. Kwa maana maandiko yasema juu ya Farao, ya kwamba, Nilikusimamisha kwa kusudi hili, ili nionyeshe nguvu zangu kwako, jina langu likatangazwe katika nchi yote. Basi, kama ni hivyo, atakaye kumrehemu humrehemu, na atakaye kumfanya mgumu humfanya mgumu. Basi, utaniambia, Mbona angali akilaumu? Kwa maana ni nani ashindanaye na kusudi lake? La! Sivyo, Ee binadamu; wewe u nani umjibuye Mungu? Je! Kitu kilichoumbwa kimwambie yeye aliyekiumba, Kwani kuniumba hivi? Au mfinyanzi je! Hana amri juu ya udongo, kwa fungu moja la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima, na kimoja kiwe hakina heshima? Ni nini basi, ikiwa Mungu kwa kutaka kuonyesha ghadhabu yake, na kuudhihirisha uweza wake, kwa uvumilivu mwingi, alichukuliana na vile vyombo vya ghadhabu vilivyofanywa tayari kwa uharibifu; tena, ili audhihirishe wingi wa utukufu wake katika vile vyombo vya rehema, alivyovitengeneza tangu zamani vipate utukufu; ndio sisi aliotuita, si watu wa Wayahudi tu, ila na watu wa Mataifa pia? Ni kama vile alivyosema katika Hosea, Nitawaita watu wangu wale wasiokuwa watu wangu, Na mpenzi wangu yeye asiyekuwa mpenzi wangu. Tena itakuwa mahali pale walipoambiwa, Ninyi si watu wangu, Hapo wataitwa wana wa Mungu aliye hai. Isaya naye atoa sauti yake juu ya Israeli, kusema, Hesabu ya wana wa Israeli, ijapokuwa ni kama mchanga wa bahari, ni mabaki yao tu watakaookolewa. Kwa maana Bwana atalitekeleza neno lake juu ya nchi, akilimaliza na kulikata. Tena kama Isaya alivyotangulia kunena, Kama Bwana wa majeshi asingalituachia uzao, Tungalikuwa kama Sodoma, tungalifananishwa na Gomora. Tuseme nini, basi? Ya kwamba watu wa Mataifa, wasioifuata haki, walipata haki; lakini ni ile haki iliyo ya imani; bali Israeli wakiifuata sheria ya haki hawakuifikilia ile sheria. Kwa sababu gani? Kwa sababu hawakuifuata kwa njia ya imani, bali kana kwamba kwa njia ya matendo. Wakajikwaa juu ya jiwe lile likwazalo, kama ilivyoandikwa, Tazama, naweka katika Sayuni jiwe likwazalo, na mwamba uangushao; Na kila amwaminiye hatatahayarika.
Waroma 9:1-33 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ninasema kweli katika Kristo, wala sisemi uongo, dhamiri yangu inanishuhudia katika Roho Mtakatifu. Nina huzuni kuu na uchungu usiokoma moyoni mwangu. Kwa maana ningetamani hata mimi nilaaniwe na kutengwa na Kristo kwa ajili ya ndugu zangu hasa, wale walio wa kabila langu kwa jinsi ya mwili, yaani watu wa Israeli. Hao ndio wenye kule kufanywa wana, ule utukufu wa Mungu, yale maagano, kule kupokea sheria, ibada ya kwenye Hekalu na zile ahadi. Wao ni wa uzao wa baba zetu wa zamani, ambao kutoka kwao Kristo alikuja kwa jinsi ya mwili kama mwanadamu, yeye ambaye ni Mungu aliye juu ya vyote, mwenye kuhimidiwa milele! Amen. Si kwamba neno la Mungu limeshindwa. Kwa maana si kila Mwisraeli ambaye ni wa uzao utokanao na Israeli ni Mwisraeli halisi. Wala hawawi wazao wa Abrahamu kwa sababu wao ni watoto wake, lakini: “Uzao wako utahesabiwa kupitia kwake Isaka.” Hii ina maana kwamba, si watoto waliozaliwa kimwili walio watoto wa Mungu, bali ni watoto wa ahadi wanaohesabiwa kuwa uzao wa Abrahamu. Kwa maana ahadi yenyewe ilisema, “Nitakurudia tena wakati kama huu, naye Sara atapata mtoto wa kiume.” Wala si hivyo tu, bali pia watoto aliowazaa Rebeka walikuwa na baba huyo huyo mmoja, yaani baba yetu Isaka. Lakini, hata kabla hao mapacha hawajazaliwa au kufanya jambo lolote jema au baya, ili kusudi la Mungu la kuchagua lipate kusimama, si kwa matendo, bali kwa yeye mwenye kuita, Rebeka aliambiwa, “Yule mkubwa atamtumikia yule mdogo.” Kama vile ilivyoandikwa, “Nimempenda Yakobo, lakini nimemchukia Esau.” Tuseme nini basi? Je, Mungu ni dhalimu? La, hasha! Kwa maana Mungu alimwambia Musa, “Nitamrehemu yeye nimrehemuye, na pia nitamhurumia yeye nimhurumiaye.” Kwa hiyo haitegemei kutaka kwa mwanadamu au jitihada, bali hutegemea huruma ya Mungu. Kwa maana Maandiko yamwambia Farao, “Nilikuinua kwa kusudi hili hasa, ili nipate kuonesha uweza wangu juu yako, na ili Jina langu lipate kutangazwa duniani kote.” Kwa hiyo basi, Mungu humhurumia yeye atakaye kumhurumia na humfanya mgumu yeye atakaye kumfanya mgumu. Basi mtaniambia, “Kama ni hivyo, kwa nini basi bado Mungu anatulaumu? Kwa maana ni nani awezaye kupinga mapenzi yake?” Lakini, ewe mwanadamu, u nani wewe ushindane na Mungu? “Je, kilichoumbwa chaweza kumwambia yeye aliyekiumba, ‘Kwa nini umeniumba hivi?’” Je, mfinyanzi hana haki ya kufinyanga kutoka bonge moja vyombo vya udongo, vingine kwa matumizi ya heshima na vingine kwa matumizi ya kawaida? Iweje basi, kama Mungu kwa kutaka kuonesha ghadhabu yake na kufanya uweza wake ujulikane, amevumilia kwa uvumilivu mwingi vile vyombo vya ghadhabu vilivyoandaliwa kwa uharibifu? Iweje basi, kama yeye alitenda hivi ili kufanya wingi wa utukufu wake ujulikane kwa vyombo vya rehema yake, alivyotangulia kuvitengeneza kwa ajili ya utukufu wake? Hivi vyombo ni sisi, ambao pia alituita, sio kutoka kwa Wayahudi peke yao, bali pia kutoka kwa watu wa Mataifa. Kama alivyosema Mungu katika Hosea: “Nitawaita ‘watu wangu’ wale ambao si watu wangu; nami nitamwita ‘mpendwa wangu’ yeye ambaye si mpendwa wangu,” tena, “Itakuwa hasa mahali pale walipoambiwa, ‘Ninyi si watu wangu,’ wao wataitwa ‘wana wa Mungu aliye hai.’ ” Isaya anapaza sauti na kusema kuhusu Israeli kwamba: “Ingawa idadi ya Waisraeli ni wengi kama mchanga wa pwani, ni mabaki yao tu watakaookolewa. Kwa kuwa Bwana ataitekeleza hukumu yake duniani kwa haraka na kwa ukamilifu.” Ni kama vile alivyotabiri Isaya, akisema: “Kama Bwana wa majeshi hakutuachia uzao, tungekuwa kama Sodoma, tungefanana na Gomora.” Kwa hiyo tuseme nini? Kwamba watu wa Mataifa ambao hawakutafuta haki, wamepata haki ile iliyo kupitia kwa imani. Lakini Israeli, ambao walijitahidi kupata haki kupitia kwa sheria, hawakuipata. Kwa nini? Kwa sababu hawakuitafuta kupitia kwa imani bali kupitia kwa matendo. Wakajikwaa kwenye lile “jiwe la kukwaza”. Kama ilivyoandikwa: “Tazama naweka katika Sayuni jiwe la kukwaza watu na mwamba wa kuwaangusha. Yeyote atakayemwamini hataaibika kamwe”.