Waroma 9:1-13
Waroma 9:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Nasema ukweli tupu; nimeungana na Kristo nami sisemi uongo. Dhamiri yangu ikiongozwa na Roho Mtakatifu inanithibitishia jambo hili pia. Nataka kusema hivi: Nina huzuni kubwa na maumivu yasiyopimika moyoni mwangu kwa ajili ya ndugu zangu walio wa taifa langu! Kama ingekuwa kwa faida yao, ningekuwa radhi kulaaniwa na kutengwa na Kristo. Hao ndio watu wa Israeli ambao Mungu aliwateua wawe watoto wake, akawashirikisha utukufu wake; alifanya nao maagano, akawapa sheria yake, imani ya kweli na ahadi zake. Wao ni wajukuu wa mababu, naye Kristo, kadiri ya ubinadamu wake, ametoka katika ukoo wao. Mungu atawalaye juu ya yote, na atukuzwe milele! Amina. Sisemi kwamba ahadi ya Mungu imebatilika; maana si watu wote wa Israeli ni wateule wa Mungu. Wala si wazawa wote wa Abrahamu ni watoto wake wa kweli. Ila, kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Wazawa wake watatokana na Isaka.” Ndiyo kusema, si wale waliozaliwa kimaumbile ndio watoto wa Mungu, bali wale waliozaliwa kutokana na ahadi ya Mungu ndio watakaoitwa watoto wake. Maana ahadi yenyewe ni hii: “Wakati maalumu nitarudi, naye Sara atapata mtoto.” Tena si hayo tu, ila pia Rebeka naye alipata mapacha kwa baba mmoja, yaani Isaka, babu yetu. Lakini, ili Mungu aonekane kwamba anao uhuru wa kuchagua, hata kabla wale ndugu hawajazaliwa na kabla hawajaweza kupambanua jema na baya, Rebeka aliambiwa kwamba yule mtoto wa kwanza atamtumikia yule wa nyuma. Hivyo uchaguzi wa Mungu unategemea jinsi anavyoita mwenyewe, na si matendo ya binadamu. Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Yakobo nilimpenda, lakini Esau nilimchukia.”
Waroma 9:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nasema kweli katika Kristo, sisemi uongo, dhamiri yangu ikinishuhudia katika Roho Mtakatifu, ya kwamba nina huzuni nyingi na maumivu yasiyoisha moyoni mwangu. Kwa maana ningeweza kuomba mimi mwenyewe niharimishwe na kutengwa na Kristo kwa ajili ya ndugu zangu, jamaa zangu kwa jinsi ya mwili; ambao ni Waisraeli, wenye kule kufanywa wana, na ule utukufu, na maagano, na kupewa torati, na ibada ya Mungu, na ahadi zake; ambao mababu ni wao, na katika hao alitoka Kristo kwa jinsi ya mwili. Ndiye aliye juu ya mambo yote, Mungu, mwenye kuhimidiwa milele. Amina. Si kana kwamba neno la Mungu limetanguka. Maana hawawi wote Waisraeli walio wa uzao wa Israeli. Wala hawawi wote wana kwa kuwa wazawa wa Abrahamu, bali, Katika Isaka wazawa wako wataitwa; yaani, si watoto wa mwili walio watoto wa Mungu, bali watoto wa ile ahadi wanahesabiwa kuwa wazawa. Kwa maana neno la ahadi ni hili, Panapo wakati huu nitakuja, na Sara atapata mtoto wa kiume. Wala si hivyo tu, lakini Rebeka naye, akiisha kuchukua mimba kwa mume mmoja, naye ni Isaka, baba yetu, (kwa maana kabla hawajazaliwa wale watoto, wala hawajatenda neno jema wala baya, ili lisimame kusudi la Mungu la kuchagua, si kwa sababu ya matendo, bali kwa sababu ya nia yake aitaye), aliambiwa hivi, Mkubwa atamtumikia mdogo. Kama ilivyoandikwa, Nimempenda Yakobo, bali Esau nimemchukia.
Waroma 9:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nasema kweli katika Kristo, sisemi uongo, dhamiri yangu ikinishuhudia katika Roho Mtakatifu, ya kwamba nina huzuni nyingi na maumivu yasiyokoma moyoni mwangu. Kwa maana ningeweza kuomba mimi mwenyewe niharimishwe na kutengwa na Kristo kwa ajili ya ndugu zangu, jamaa zangu kwa jinsi ya mwili; ambao ni Waisraeli, wenye kule kufanywa wana, na ule utukufu, na maagano, na kupewa torati, na ibada ya Mungu, na ahadi zake; ambao mababu ni wao, na katika hao alitoka Kristo kwa jinsi ya mwili. Ndiye aliye juu ya mambo yote, Mungu, mwenye kuhimidiwa milele. Amina. Si kana kwamba neno la Mungu limetanguka. Maana hawawi wote Waisraeli walio wa uzao wa Israeli. Wala hawawi wote wana kwa kuwa wazao wa Ibrahimu, bali, Katika Isaka wazao wako wataitwa; yaani, si watoto wa mwili walio watoto wa Mungu, bali watoto wa ile ahadi wanahesabiwa kuwa wazao. Kwa maana neno la ahadi ni hili, Panapo wakati huu nitakuja, na Sara atakuwa na mwana. Wala si hivyo tu, lakini Rebeka naye, akiisha kuchukua mimba kwa mume mmoja, naye ni Isaka, baba yetu, (kwa maana kabla hawajazaliwa wale watoto, wala hawajatenda neno jema wala baya, ili lisimame kusudi la Mungu la kuchagua, si kwa sababu ya matendo, bali kwa sababu ya nia yake aitaye), aliambiwa hivi, Mkubwa atamtumikia mdogo. Kama ilivyoandikwa, Nimempenda Yakobo, bali Esau nimemchukia.
Waroma 9:1-13 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ninasema kweli katika Kristo, wala sisemi uongo, dhamiri yangu inanishuhudia katika Roho Mtakatifu. Nina huzuni kuu na uchungu usiokoma moyoni mwangu. Kwa maana ningetamani hata mimi nilaaniwe na kutengwa na Kristo kwa ajili ya ndugu zangu hasa, wale walio wa kabila langu kwa jinsi ya mwili, yaani watu wa Israeli. Hao ndio wenye kule kufanywa wana, ule utukufu wa Mungu, yale maagano, kule kupokea sheria, ibada ya kwenye Hekalu na zile ahadi. Wao ni wa uzao wa baba zetu wa zamani, ambao kutoka kwao Kristo alikuja kwa jinsi ya mwili kama mwanadamu, yeye ambaye ni Mungu aliye juu ya vyote, mwenye kuhimidiwa milele! Amen. Si kwamba neno la Mungu limeshindwa. Kwa maana si kila Mwisraeli ambaye ni wa uzao utokanao na Israeli ni Mwisraeli halisi. Wala hawawi wazao wa Abrahamu kwa sababu wao ni watoto wake, lakini: “Uzao wako utahesabiwa kupitia kwake Isaka.” Hii ina maana kwamba, si watoto waliozaliwa kimwili walio watoto wa Mungu, bali ni watoto wa ahadi wanaohesabiwa kuwa uzao wa Abrahamu. Kwa maana ahadi yenyewe ilisema, “Nitakurudia tena wakati kama huu, naye Sara atapata mtoto wa kiume.” Wala si hivyo tu, bali pia watoto aliowazaa Rebeka walikuwa na baba huyo huyo mmoja, yaani baba yetu Isaka. Lakini, hata kabla hao mapacha hawajazaliwa au kufanya jambo lolote jema au baya, ili kusudi la Mungu la kuchagua lipate kusimama, si kwa matendo, bali kwa yeye mwenye kuita, Rebeka aliambiwa, “Yule mkubwa atamtumikia yule mdogo.” Kama vile ilivyoandikwa, “Nimempenda Yakobo, lakini nimemchukia Esau.”