Waroma 4:7-12
Waroma 4:7-12 Biblia Habari Njema (BHN)
“Heri wale waliosamehewa makosa yao ambao makosa yao yamefutwa. Heri mtu yule ambaye Bwana hataziweka dhambi zake katika kumbukumbu.” Je, hiyo ni kwa wale waliotahiriwa tu, ama pia kwa wale wasiotahiriwa? Ni kwa wale wasiotahiriwa pia. Kwa maana tumekwisha sema: “Abrahamu aliamini, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu.” Je, Abrahamu alikubaliwa kabla ya kutahiriwa, ama baada ya kutahiriwa? Kabla ya kutahiriwa, na si baada ya kutahiriwa. Abrahamu alitahiriwa baadaye, na kutahiriwa huko kulikuwa alama iliyothibitisha kwamba Mungu alimkubali kuwa mwadilifu kwa sababu ya imani yake aliyokuwa nayo kabla ya kutahiriwa. Kwa hiyo, Abrahamu amekuwa baba wa wale wote ambao, ingawa hawakutahiriwa, wamemwamini Mungu, wakafanywa waadilifu. Vilevile yeye ni baba wa wale waliotahiriwa; lakini si kwa kuwa wametahiriwa, bali kwa sababu wanafuata njia ileile ya imani baba yetu Abrahamu aliyofuata kabla ya kutahiriwa.
Waroma 4:7-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Heri waliosamehewa makosa yao, Na waliositiriwa dhambi zao. Heri mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi. Basi je! Heri hiyo ni kwa hao waliotahiriwa, au kwa hao pia wasiotahiriwa? Kwa kuwa tunanena ya kwamba kwake Abrahamu imani yake ilihesabiwa kuwa ni haki. Alihesabiwaje basi? Alipokwisha kutahiriwa, au kabla hajatahiriwa? Si baada ya kutahiriwa, bali kabla ya kutahiriwa. Naye aliipokea dalili hii ya kutahiriwa, mhuri wa ile haki ya imani aliyokuwa nayo kabla hajatahiriwa; apate kuwa baba yao wote waaminio, ijapokuwa hawakutahiriwa, ili na wao pia wahesabiwe haki; tena awe baba ya kutahiriwa, kwa wale ambao si waliotahiriwa tu, bali pia wanazifuata nyayo za imani yake baba yetu Abrahamu aliyokuwa nayo kabla hajatahiriwa.
Waroma 4:7-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Heri waliosamehewa makosa yao, Na waliositiriwa dhambi zao. Heri mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi. Basi je! Uheri huo ni kwa hao waliotahiriwa, au kwa hao pia wasiotahiriwa? Kwa kuwa twanena ya kwamba kwake Ibrahimu imani yake ilihesabiwa kuwa ni haki. Alihesabiwaje basi? Alipokwisha kutahiriwa, au kabla hajatahiriwa? Si baada ya kutahiriwa, bali kabla ya kutahiriwa. Naye aliipokea dalili hii ya kutahiriwa, muhuri ya ile haki ya imani aliyokuwa nayo kabla hajatahiriwa; apate kuwa baba yao wote waaminio, ijapokuwa hawakutahiriwa, ili na wao pia wahesabiwe haki; tena awe baba ya kutahiriwa, kwa wale ambao si waliotahiriwa tu, bali pia wanazifuata nyayo za imani yake baba yetu Ibrahimu aliyokuwa nayo kabla hajatahiriwa.
Waroma 4:7-12 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Wamebarikiwa wale ambao wamesamehewa makosa yao, ambao dhambi zao zimefunikwa. Heri mtu yule Bwana hamhesabii dhambi zake.” Je, huku kubarikiwa ni kwa wale waliotahiriwa peke yao, au pia na kwa wale wasiotahiriwa? Tumesema imani ya Abrahamu ilihesabiwa kwake kuwa haki. Je, ilihesabiwaje kwake kuwa haki? Ni kabla ya kutahiriwa, au baada yake kutahiriwa? Haikuwa baada yake kutahiriwa, bali kabla hajatahiriwa! Alipewa ishara ya tohara kuwa muhuri wa haki aliyokuwa nayo kwa imani hata alipokuwa bado hajatahiriwa. Kusudi lilikuwa kumfanya baba wa wote waaminio pasipo kutahiriwa, ili wahesabiwe kuwa wenye haki. Vivyo hivyo awe baba wa wale waliotahiriwa ambao si kwamba wametahiriwa tu, bali pia wanafuata mfano wa imani ambayo baba yetu Abrahamu alikuwa nayo kabla ya kutahiriwa.