Waroma 14:7-15
Waroma 14:7-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Maana hakuna mtu yeyote miongoni mwetu aishiye kwa ajili yake mwenyewe, wala hakuna anayekufa kwa ajili yake mwenyewe maana tukiishi twaishi kwa ajili ya Bwana; tukifa, tunakufa kwa ajili ya Bwana. Basi, kama tukiishi au tukifa, sisi ni mali yake Bwana. Maana Kristo alikufa, akafufuka ili apate kuwa Bwana wa walio hai na wafu. Kwa nini basi, wewe wamhukumu ndugu yako? Nawe, kwa nini wamdharau ndugu yako? Sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu. Maana Maandiko yanasema: “Kama niishivyo, asema Bwana, kila mtu atanipigia magoti, na kila mmoja atakiri kwamba mimi ni Mungu.” Kwa hiyo, kila mmoja wetu atatoa hoja juu yake mwenyewe mbele ya Mungu. Basi, tuache kuhukumiana, bali tuazimie kutokuwa kamwe kikwazo kwa ndugu au kumsababisha aanguke katika dhambi. Katika kuungana na Bwana Yesu, nina hakika kwamba hakuna kitu chochote kilicho najisi kwa asili yake; lakini, mtu akidhani kwamba kitu fulani ni najisi, basi, kwake huwa najisi. Kama ukimhuzunisha ndugu yako kwa sababu ya chakula unachokula, basi mwenendo wako hauongozwi na upendo. Usikubali hata kidogo chakula chako kiwe sababu ya kupotea kwa mtu mwingine ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake!
Waroma 14:7-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake. Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana. Maana Kristo alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia. Lakini wewe je! Mbona wamhukumu ndugu yako? Au wewe je! Mbona wamdharau ndugu yako? Kwa maana sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu. Kwa kuwa imeandikwa, Kama niishivyo, anena Bwana, kila goti litapigwa mbele zangu; Na kila ulimi utamkiri Mungu. Basi ni hivyo, kila mtu miongoni mwetu atatoa habari zake mwenyewe mbele za Mungu. Basi tusiendelee kuhukumiana, bali amueni kuwa mtu asifanye kitu cha kumkwaza ndugu au cha kumwangusha. Najua, tena nimehakikishwa sana katika Bwana Yesu, ya kuwa hakuna kitu kilicho najisi kwa asili yake, lakini kwake yeye akionaye kitu kuwa najisi, kwake huyo kitu kile ni najisi. Na ndugu yako akichukizwa kwa sababu ya chakula, umeacha kwenda katika upendo. Kwa chakula chako usimharibu mtu yule ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake.
Waroma 14:7-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake. Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana. Maana Kristo alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia. Lakini wewe je! Mbona wamhukumu ndugu yako? Au wewe je! Mbona wamdharau ndugu yako? Kwa maana sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu. Kwa kuwa imeandikwa, Kama niishivyo, anena Bwana, kila goti litapigwa mbele zangu; Na kila ulimi utamkiri Mungu. Basi ni hivyo, kila mtu miongoni mwetu atatoa habari zake mwenyewe mbele za Mungu. Basi tusizidi kuhukumiana, bali afadhali toeni hukumu hii, mtu asitie kitu cha kumkwaza ndugu au cha kumwangusha. Najua, tena nimehakikishwa sana katika Bwana Yesu, ya kuwa hakuna kitu kilicho najisi kwa asili yake, lakini kwake yeye akionaye kitu kuwa najisi, kwake huyo kitu kile ni najisi. Na ndugu yako akiingia huzuni kwa sababu ya chakula, umeacha kwenda katika upendo. Kwa chakula chako usimharibu mtu yule ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake.
Waroma 14:7-15 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa kuwa hakuna hata mmoja wetu anayeishi kwa ajili yake mwenyewe, wala hakuna hata mmoja wetu afaye kwa ajili yake mwenyewe. Kama tunaishi, tunaishi kwa Bwana, nasi pia tukifa tunakufa kwa Bwana. Kwa hiyo basi, kama tukiishi au kama tukifa, sisi ni mali ya Bwana. Kwani kwa sababu hii hasa, Kristo alikufa na akawa hai tena kusudi apate kuwa Bwana wa wote, yaani waliokufa na walio hai. Basi kwa nini wewe wamhukumu ndugu yako? Au kwa nini wewe unamdharau ndugu yako? Kwa kuwa sote tutasimama mbele ya kiti cha Mungu cha hukumu. Kwa kuwa imeandikwa: “ ‘Kama vile niishivyo,’ asema Bwana, ‘kila goti litapigwa mbele zangu, na kila ulimi utakiri kwa Mungu.’ ” Hivyo basi kila mmoja wetu atatoa habari zake mwenyewe kwa Mungu. Kwa hiyo tusiendelee kuhukumiana. Badala yake mtu aamue kutoweka kamwe kikwazo au kizuizi katika njia ya ndugu mwingine. Ninajua tena nimehakikishiwa sana katika Bwana Yesu kwamba hakuna kitu chochote ambacho ni najisi kwa asili yake. Lakini kama mtu anakiona kitu kuwa ni najisi, basi kwake huyo kitu hicho ni najisi. Kama ndugu yako anahuzunishwa kwa sababu ya kile unachokula, basi huenendi tena katika upendo. Usiruhusu kile unachokula kiwe sababu ya kumwangamiza ndugu yako ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake.