Waroma 14:13-23
Waroma 14:13-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, tuache kuhukumiana, bali tuazimie kutokuwa kamwe kikwazo kwa ndugu au kumsababisha aanguke katika dhambi. Katika kuungana na Bwana Yesu, nina hakika kwamba hakuna kitu chochote kilicho najisi kwa asili yake; lakini, mtu akidhani kwamba kitu fulani ni najisi, basi, kwake huwa najisi. Kama ukimhuzunisha ndugu yako kwa sababu ya chakula unachokula, basi mwenendo wako hauongozwi na upendo. Usikubali hata kidogo chakula chako kiwe sababu ya kupotea kwa mtu mwingine ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake! Basi, msikubali kitu mnachokiona kwenu kuwa chema kidharauliwe. Maana ufalme wa Mungu si shauri la kula na kunywa, bali unahusika na kuwa na uadilifu, amani na furaha iletwayo na Roho Mtakatifu. Anayemtumikia Kristo namna hiyo humpendeza Mungu, na kukubaliwa na watu. Kwa hiyo tuyazingatie daima mambo yenye kuleta amani, na yanayotusaidia kujengana. Basi, usiiharibu kazi ya Mungu kwa sababu ya ubishi juu ya chakula. Vyakula vyote ni halali, lakini haifai kula chakula ambacho kitamfanya mtu aanguke katika dhambi. Afadhali kuacha kula nyama, kunywa divai, au kufanya chochote ambacho chaweza kumsababisha ndugu yako aanguke. Basi, shikilia unachoamini kati yako na Mungu wako. Heri mtu yule ambaye, katika kujiamulia la kufanya, haipingi dhamiri yake. Lakini mtu anayeona shaka juu ya chakula anachokula, anahukumiwa kama akila, kwa sababu msimamo wa kitendo chake haumo katika imani. Na, chochote kisicho na msingi wake katika imani ni dhambi.
Waroma 14:13-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi tusiendelee kuhukumiana, bali amueni kuwa mtu asifanye kitu cha kumkwaza ndugu au cha kumwangusha. Najua, tena nimehakikishwa sana katika Bwana Yesu, ya kuwa hakuna kitu kilicho najisi kwa asili yake, lakini kwake yeye akionaye kitu kuwa najisi, kwake huyo kitu kile ni najisi. Na ndugu yako akichukizwa kwa sababu ya chakula, umeacha kwenda katika upendo. Kwa chakula chako usimharibu mtu yule ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake. Basi, huo wema wenu usitajwe kwa ubaya. Maana ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu. Kwa kuwa yeye amtumikiaye Kristo katika mambo hayo humpendeza Mungu, tena hukubaliwa na wanadamu. Basi kama ni hivyo, na mfuate mambo ya amani na mambo yafaayo kwa kujengana. Kwa ajili ya chakula usiiharibu kazi ya Mungu. Kweli, vyote ni safi; bali ni vibaya kwa mtu alaye na kujikwaza. Ni vyema kutokula nyama wala kunywa divai wala kutenda neno lolote ambalo kwa hilo ndugu yako hukwazwa. Ile imani uliyo nayo uwe nayo nafsini mwako mbele za Mungu. Heri mtu yule asiyejihukumu nafsi yake katika neno lile analolikubali. Lakini aliye na mashaka, kama akila, amehukumiwa kuwa ana hatia, kwa maana hakula kwa imani. Na kila tendo lisilotoka katika imani ni dhambi.
Waroma 14:13-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi tusizidi kuhukumiana, bali afadhali toeni hukumu hii, mtu asitie kitu cha kumkwaza ndugu au cha kumwangusha. Najua, tena nimehakikishwa sana katika Bwana Yesu, ya kuwa hakuna kitu kilicho najisi kwa asili yake, lakini kwake yeye akionaye kitu kuwa najisi, kwake huyo kitu kile ni najisi. Na ndugu yako akiingia huzuni kwa sababu ya chakula, umeacha kwenda katika upendo. Kwa chakula chako usimharibu mtu yule ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake. Basi, huo wema wenu usitajwe kwa ubaya. Maana ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu. Kwa kuwa yeye amtumikiaye Kristo katika mambo hayo humpendeza Mungu, tena hukubaliwa na wanadamu. Basi kama ni hivyo, na mfuate mambo ya amani na mambo yafaayo kwa kujengana. Kwa ajili ya chakula usiiharibu kazi ya Mungu. Kweli, vyote ni safi; bali ni vibaya kwa mtu alaye na kujikwaza. Ni vyema kutokula nyama wala kunywa divai wala kutenda neno lo lote ambalo kwa hilo ndugu yako hukwazwa. Ile imani uliyo nayo uwe nayo nafsini mwako mbele za Mungu. Heri mtu yule asiyejihukumu nafsi yake katika neno lile analolikubali. Lakini aliye na shaka, kama akila, amehukumiwa kuwa ana hatia, kwa maana hakula kwa imani. Na kila tendo lisilotoka katika imani ni dhambi.
Waroma 14:13-23 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa hiyo tusiendelee kuhukumiana. Badala yake mtu aamue kutoweka kamwe kikwazo au kizuizi katika njia ya ndugu mwingine. Ninajua tena nimehakikishiwa sana katika Bwana Yesu kwamba hakuna kitu chochote ambacho ni najisi kwa asili yake. Lakini kama mtu anakiona kitu kuwa ni najisi, basi kwake huyo kitu hicho ni najisi. Kama ndugu yako anahuzunishwa kwa sababu ya kile unachokula, basi huenendi tena katika upendo. Usiruhusu kile unachokula kiwe sababu ya kumwangamiza ndugu yako ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake. Usiruhusu kile ambacho unakiona kuwa chema kisemwe kuwa ni kiovu. Kwa maana ufalme wa Mungu si kula na kunywa, bali ni haki, amani na furaha katika Roho Mtakatifu. Kwa sababu mtu yeyote anayemtumikia Kristo kwa jinsi hii, anampendeza Mungu na kukubaliwa na wanadamu. Kwa hiyo na tufanye bidii kutafuta yale yaletayo amani na kujengana sisi kwa sisi. Usiiharibu kazi ya Mungu kwa ajili ya chakula. Hakika vyakula vyote ni safi, lakini ni kosa kula kitu chochote kinachomsababisha ndugu yako ajikwae. Ni afadhali kutokula nyama wala kunywa divai au kufanya jambo lingine lolote litakalomsababisha ndugu yako ajikwae. Je, wewe unayo imani? Ile imani uliyo nayo, uwe nayo nafsini mwako mbele za Mungu. Heri mtu yule asiye na sababu ya kujihukumu nafsi yake kwa ajili ya kile anachokifanya. Lakini kama mtu ana shaka kuhusu kile anachokula, amehukumiwa, kwa sababu hakula kwa imani. Kwa kuwa chochote kinachofanywa pasipo imani ni dhambi.