Waroma 11:17-27
Waroma 11:17-27 Biblia Habari Njema (BHN)
Naam, baadhi ya matawi ya mzeituni bustanini yalikatwa, na mahali pake tawi la mzeituni mwitu likapandikizwa. Nyinyi watu wa mataifa mengine ndio hilo tawi la mzeituni mwitu; na sasa mnashiriki nguvu na utomvu wa mzeituni bustanini. Basi, msiwadharau wale waliokatwa kama matawi! Na, hata kama kuna la kujivunia, kumbukeni kwamba si nyinyi mnaoitegemeza mizizi, bali mizizi ndiyo inayowategemeza nyinyi. Lakini utasema: “Matawi yalikatwa kusudi mimi nipandikizwe mahali pake.” Sawa! Yalikatwa kwa sababu ya kukosa imani, bali wewe unasimama kwa imani yako. Lakini usijivune; ila uwe na tahadhari. Kwa maana, ikiwa Mungu hakuwahurumia Wayahudi ambao ni kama matawi ya asili, je, unadhani atakuhurumia wewe? Ona, basi, jinsi Mungu alivyo mwema na mkali. Yeye ni mkali kwa wale walioanguka, na ni mwema kwako wewe ikiwa utaendelea katika wema wake; la sivyo, nawe pia utakatwa. Nao Wayahudi, hali kadhalika; wakiacha utovu wao wa imani, watapandikizwa tena. Maana Mungu anao uwezo wa kuwapandikiza tena. Nyinyi watu wa mataifa mengine, kwa asili ni kama tawi la mzeituni mwitu, lakini mmeondolewa huko, mkapandikizwa katika mzeituni bustanini mahali ambapo kwa asili si penu. Lakini, Wayahudi kwa asili ni kama mzeituni bustanini, na itakuwa jambo rahisi zaidi kwao kupandikizwa tena katika mti huohuo wao. Ndugu zangu, napenda mjue ukweli huu uliofichika msije mkajiona wenye akili sana. Ukaidi wa Wayahudi ulikuwa ni wa muda tu, mpaka watu wa mataifa mengine watakapokuwa wamemfikia Mungu. Hapo ndipo taifa lote la Israeli litakapookolewa, kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Mkombozi atakuja kutoka Siyoni, atauondoa uovu wa wazawa wa Yakobo. Hili ndilo agano nitakalofanya nao wakati nitakapoziondoa dhambi zao.”
Waroma 11:17-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini iwapo matawi mengine yamekatwa, na wewe mzeituni mwitu ulipandikizwa kati yao, ukawa mshirika wa shina la mzeituni na unono wake, usijisifu juu ya matawi yale; au ikiwa wajisifu, si wewe ulichukuaye shina, bali ni shina likuchukualo wewe. Basi utasema, Matawi yale yalikatwa kusudi ili nipandikizwe mimi. Vema. Yalikatwa kwa kutoamini kwao, na wewe wasimama kwa imani yako. Usijivune, bali uogope. Kwa maana ikiwa Mungu hakuyaachia matawi ya asili, wala hatakuachia wewe. Tazama, basi, wema na ukali wa Mungu; kwa wale walioanguka, ukali, bali kwako wewe wema wa Mungu, ukikaa katika wema huo; kama sivyo, wewe nawe utakatiliwa mbali. Na hao pia, wasipokaa katika kutoamini kwao, watapandikizwa; kwa kuwa Mungu aweza kuwapandikiza tena. Kwa maana ikiwa wewe ulikatwa ukatolewa katika mzeituni, ulio mzeituni mwitu kwa asili yake, kisha ukapandikizwa, kinyume cha asili, katika mzeituni ulio mwema, si zaidi sana wale walio wa asili kuweza kupandikizwa katika mzeituni wao wenyewe? Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili. Hivyo Israeli wote wataokoka; kama ilivyoandikwa, Mwokozi atakuja kutoka Sayuni; Atamtenga Yakobo na maasia yake. Na hili ndilo agano langu nao, Nitakapowaondolea dhambi zao.
Waroma 11:17-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini iwapo matawi mengine yamekatwa, na wewe mzeituni mwitu ulipandikizwa kati yao, ukawa mshirika wa shina la mzeituni na unono wake, usijisifu juu ya matawi yale; au ikiwa wajisifu, si wewe ulichukuaye shina, bali ni shina likuchukualo wewe. Basi utasema, Matawi yale yalikatwa kusudi ili nipandikizwe mimi. Vema. Yalikatwa kwa kutokuamini kwao, na wewe wasimama kwa imani yako. Usijivune, bali uogope. Kwa maana ikiwa Mungu hakuyaachia matawi ya asili, wala hatakuachia wewe. Tazama, basi, wema na ukali wa Mungu; kwa wale walioanguka, ukali, bali kwako wewe wema wa Mungu, ukikaa katika wema huo; kama sivyo, wewe nawe utakatiliwa mbali. Na hao pia, wasipokaa katika kutokuamini kwao, watapandikizwa; kwa kuwa Mungu aweza kuwapandikiza tena. Kwa maana ikiwa wewe ulikatwa ukatolewa katika mzeituni, ulio mzeituni mwitu kwa asili yake, kisha ukapandikizwa, kinyume cha asili, katika mzeituni ulio mwema, si zaidi sana wale walio wa asili kuweza kupandikizwa katika mzeituni wao wenyewe? Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili. Hivyo Israeli wote wataokoka; kama ilivyoandikwa, Mwokozi atakuja kutoka Sayuni; Atamtenga Yakobo na maasia yake. Na hili ndilo agano langu nao, Nitakapowaondolea dhambi zao.
Waroma 11:17-27 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Lakini kama baadhi ya matawi yalikatwa, nawe chipukizi la mzeituni mwitu ukapandikizwa mahali pao ili kushiriki unono pamoja na matawi mengine kutoka shina la mzeituni, basi usijivune juu ya hayo matawi. Lakini ukijivuna, kumbuka jambo hili: Si wewe unayelishikilia shina, bali ni shina linalokushikilia wewe. Basi utasema, “Matawi yale yalikatwa ili nipate kupandikizwa katika hilo shina.” Hii ni kweli. Matawi hayo yalikatwa kwa sababu ya kutokuamini kwake, lakini wewe umesimama tu kwa sababu ya imani. Kwa hiyo usijivune, bali simama kwa kuogopa. Kwa maana kama Mungu hakuyahurumia matawi ya asili, wala hatakuhurumia wewe. Angalia basi wema na ukali wa Mungu: Ukali kwa wale walioanguka, bali wema wa Mungu kwako wewe, kama utadumu katika wema wake. La sivyo, nawe utakatiliwa mbali. Wao nao wasipodumu katika kutokuamini kwao, watapandikizwa tena kwenye shina, kwa maana Mungu anao uwezo wa kuwapandikiza tena kwenye hilo shina. Ikiwa wewe ulikatwa kutoka kile ambacho kwa asili ni mzeituni mwitu, na kupandikizwa kinyume cha asili kwenye mzeituni uliopandwa, si rahisi zaidi matawi haya ya asili kupandikizwa tena kwenye shina lake la mzeituni wao mwenyewe! Ndugu zangu, ili msije mkajidai kuwa wenye hekima kuliko mlivyo, nataka mfahamu siri hii: Ugumu umewapata Israeli kwa sehemu hadi idadi ya watu wa Mataifa watakaoingia itimie. Hivyo Israeli wote wataokolewa. Kama ilivyoandikwa: “Mkombozi atakuja kutoka Sayuni; ataondoa kutokumcha Mungu katika Yakobo. Hili ndilo agano langu nao nitakapoziondoa dhambi zao.”