Waroma 11:1-6
Waroma 11:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, nauliza: Je, Mungu amewakataa watu wake? Hata kidogo! Mimi binafsi ni Mwisraeli, mzawa wa Abrahamu, wa kabila la Benyamini. Mungu hakuwakataa watu wake aliowateua tangu mwanzo. Mnakumbuka yasemavyo Maandiko Matakatifu juu ya Elia wakati alipomnungunikia Mungu kuhusu Israeli: “Bwana, wamewaua manabii wako na kubomoa madhabahu yako. Ni mimi tu peke yangu niliyebaki, nao wanataka kuniua!” Je, Mungu alimjibu nini? Alimwambia: “Nimejiwekea watu 7,000 ambao hawakumwabudu Baali.” Basi, ndivyo ilivyo pia wakati huu wa sasa: Ipo idadi ya waliobaki ambao Mungu aliwateua kwa sababu ya neema yake. Uteuzi wake unatokana na neema yake, na si kwa sababu ya matendo yao. Maana, kama uteuzi wake ungetegemea matendo ya watu, neema yake haingekuwa neema tena.
Waroma 11:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi, nauliza, Je! Mungu aliwasukumia mbali watu wake? La hasha! Kwa kuwa mimi nami ni Mwisraeli, mmoja wa wazawa wa Abrahamu, mtu wa kabila la Benyamini. Mungu hakuwasukumia mbali watu wake aliowajua tokea awali. Au hamjui yale yaliyonenwa na Maandiko juu ya Eliya? Jinsi anavyowashitaki Waisraeli mbele za Mungu, Bwana, wamewaua manabii wako, wamezibomoa madhabahu zako, nami nimebaki peke yangu, nao wananitafuta roho yangu. Lakini lile jibu la Mungu lamwambiaje? Nimejibakizia watu elfu saba wasiopiga goti mbele ya Baali. Basi ni vivi hivi wakati huu wa sasa, yako mabaki waliochaguliwa kwa neema. Lakini ikiwa ni kwa neema, haiwi kwa matendo tena, au hapo neema isingekuwa neema.
Waroma 11:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi, nauliza, Je! Mungu aliwasukumia mbali watu wake? Hasha! Kwa kuwa mimi nami ni Mwisraeli, mmoja wa wazao wa Ibrahimu, mtu wa kabila ya Benyamini. Mungu hakuwasukumia mbali watu wake aliowajua tokea awali. Au hamjui yale yaliyonenwa na maandiko juu ya Eliya? Jinsi anavyowashitaki Waisraeli mbele za Mungu, Bwana, wamewaua manabii wako, wamezibomoa madhabahu zako, nami nimesalia peke yangu, nao wananitafuta roho yangu. Lakini ile jawabu ya Mungu yamwambiaje? Nimejisazia watu elfu saba wasiopiga goti mbele ya Baali. Basi ni vivi hivi wakati huu wa sasa, yako mabaki waliochaguliwa kwa neema. Lakini ikiwa ni kwa neema, haiwi kwa matendo tena, au hapo neema isingekuwa neema.
Waroma 11:1-6 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi nauliza: Je, Mungu amewakataa watu wake? La, hasha! Mimi mwenyewe ni Mwisraeli, tena uzao wa Abrahamu kutoka kabila la Benyamini. Mungu hajawakataa watu wake, ambao yeye aliwajua tangu mwanzo. Je, hamjui yale Maandiko yasemayo kuhusu Eliya, jinsi alivyomlalamikia Mungu kuhusu Israeli? Alisema, “Bwana, wamewaua manabii wako na kuzibomoa madhabahu zako, nimebaki mimi peke yangu, nao wanataka kuniua?” Je, Mungu alimjibuje? “Nimejibakizia watu elfu saba ambao hawajapiga magoti kumwabudu Baali.” Vivyo hivyo pia, sasa wapo mabaki waliochaguliwa kwa neema ya Mungu. Lakini ikiwa wamechaguliwa kwa neema, si tena kwa msingi wa matendo. Kama ingekuwa kwa matendo, neema isingekuwa neema tena.