Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waroma 11:1-32

Waroma 11:1-32 Biblia Habari Njema (BHN)

Basi, nauliza: Je, Mungu amewakataa watu wake? Hata kidogo! Mimi binafsi ni Mwisraeli, mzawa wa Abrahamu, wa kabila la Benyamini. Mungu hakuwakataa watu wake aliowateua tangu mwanzo. Mnakumbuka yasemavyo Maandiko Matakatifu juu ya Elia wakati alipomnungunikia Mungu kuhusu Israeli: “Bwana, wamewaua manabii wako na kubomoa madhabahu yako. Ni mimi tu peke yangu niliyebaki, nao wanataka kuniua!” Je, Mungu alimjibu nini? Alimwambia: “Nimejiwekea watu 7,000 ambao hawakumwabudu Baali.” Basi, ndivyo ilivyo pia wakati huu wa sasa: Ipo idadi ya waliobaki ambao Mungu aliwateua kwa sababu ya neema yake. Uteuzi wake unatokana na neema yake, na si kwa sababu ya matendo yao. Maana, kama uteuzi wake ungetegemea matendo ya watu, neema yake haingekuwa neema tena. Sasa, je? Watu wa Israeli hawakukipata kile walichokuwa wanakitafuta; lakini wote walioteuliwa walikipata. Wengine walipumbazwa, kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Mungu ameifanya mioyo yao kuwa mizito, na mpaka leo hii hawawezi kuona kwa macho yao wala kusikia kwa masikio yao.” Naye Daudi anasema: “Karamu zao na ziwe mtego wa kuwanasa, waanguke na kuadhibiwa. Macho yao yatiwe giza wasiweze kuona. Migongo yao ipindike kwa taabu daima!” Basi, nauliza: Je, Wayahudi wamejikwaa hata wakaangamia kabisa? Hata kidogo! Kutokana na kosa lao ukombozi umewajia watu wa mataifa mengine, ili Wayahudi wapate kuwaonea wivu. Kosa la Wayahudi limesababisha baraka nyingi kwa ulimwengu, na utovu wao wa kiroho umeleta baraka nyingi kwa watu wa mataifa mengine. Basi, ni dhahiri kwamba kuingizwa kwa idadi yao kamili kutakuwa ni baraka zaidi. Basi, sasa nawaambieni nyinyi watu wa mataifa mengine: Maadamu mimi nimekuwa mtume kwa watu wa mataifa mengine, ninajivunia huduma yangu, nipate kuwafanya wananchi wenzangu wawaonee nyinyi wivu, na hivyo nipate kuwaokoa baadhi yao. Maana ikiwa kukataliwa kwao kulisababisha ulimwengu upatanishwe na Mungu, itakuwaje wakati watakapokubaliwa na Mungu? Wafu watafufuka! Ikiwa kipande cha kwanza cha mkate kimewekwa wakfu, mkate wote umewekwa wakfu; mizizi ya mti ikiwa mizuri, na matawi yake huwa mazuri pia. Naam, baadhi ya matawi ya mzeituni bustanini yalikatwa, na mahali pake tawi la mzeituni mwitu likapandikizwa. Nyinyi watu wa mataifa mengine ndio hilo tawi la mzeituni mwitu; na sasa mnashiriki nguvu na utomvu wa mzeituni bustanini. Basi, msiwadharau wale waliokatwa kama matawi! Na, hata kama kuna la kujivunia, kumbukeni kwamba si nyinyi mnaoitegemeza mizizi, bali mizizi ndiyo inayowategemeza nyinyi. Lakini utasema: “Matawi yalikatwa kusudi mimi nipandikizwe mahali pake.” Sawa! Yalikatwa kwa sababu ya kukosa imani, bali wewe unasimama kwa imani yako. Lakini usijivune; ila uwe na tahadhari. Kwa maana, ikiwa Mungu hakuwahurumia Wayahudi ambao ni kama matawi ya asili, je, unadhani atakuhurumia wewe? Ona, basi, jinsi Mungu alivyo mwema na mkali. Yeye ni mkali kwa wale walioanguka, na ni mwema kwako wewe ikiwa utaendelea katika wema wake; la sivyo, nawe pia utakatwa. Nao Wayahudi, hali kadhalika; wakiacha utovu wao wa imani, watapandikizwa tena. Maana Mungu anao uwezo wa kuwapandikiza tena. Nyinyi watu wa mataifa mengine, kwa asili ni kama tawi la mzeituni mwitu, lakini mmeondolewa huko, mkapandikizwa katika mzeituni bustanini mahali ambapo kwa asili si penu. Lakini, Wayahudi kwa asili ni kama mzeituni bustanini, na itakuwa jambo rahisi zaidi kwao kupandikizwa tena katika mti huohuo wao. Ndugu zangu, napenda mjue ukweli huu uliofichika msije mkajiona wenye akili sana. Ukaidi wa Wayahudi ulikuwa ni wa muda tu, mpaka watu wa mataifa mengine watakapokuwa wamemfikia Mungu. Hapo ndipo taifa lote la Israeli litakapookolewa, kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Mkombozi atakuja kutoka Siyoni, atauondoa uovu wa wazawa wa Yakobo. Hili ndilo agano nitakalofanya nao wakati nitakapoziondoa dhambi zao.” Kwa sababu wanaikataa Habari Njema, Wayahudi wamekuwa maadui wa Mungu, lakini kwa faida yenu nyinyi watu wa mataifa. Lakini, kwa kuwa waliteuliwa, bado ni marafiki wa Mungu kwa sababu ya babu zao. Maana Mungu akisha wapa watu zawadi zake na kuwateua, hajuti kwamba amefanya hivyo. Hapo awali nyinyi mlikuwa mmemwasi Mungu, lakini sasa mmepata huruma yake kutokana na kuasi kwao. Hali kadhalika, kutokana na huruma mliyojaliwa nyinyi, Wayahudi wanamwasi Mungu sasa ili nao pia wapokee sasa huruma ya Mungu. Maana Mungu amewafunga watu wote katika uasi wao ili apate kuwahurumia wote.

Shirikisha
Soma Waroma 11

Waroma 11:1-32 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi, nauliza, Je! Mungu aliwasukumia mbali watu wake? La hasha! Kwa kuwa mimi nami ni Mwisraeli, mmoja wa wazawa wa Abrahamu, mtu wa kabila la Benyamini. Mungu hakuwasukumia mbali watu wake aliowajua tokea awali. Au hamjui yale yaliyonenwa na Maandiko juu ya Eliya? Jinsi anavyowashitaki Waisraeli mbele za Mungu, Bwana, wamewaua manabii wako, wamezibomoa madhabahu zako, nami nimebaki peke yangu, nao wananitafuta roho yangu. Lakini lile jibu la Mungu lamwambiaje? Nimejibakizia watu elfu saba wasiopiga goti mbele ya Baali. Basi ni vivi hivi wakati huu wa sasa, yako mabaki waliochaguliwa kwa neema. Lakini ikiwa ni kwa neema, haiwi kwa matendo tena, au hapo neema isingekuwa neema. Imekuwaje basi? Kitu kile ambacho Israeli alikuwa akikitafuta hakukipata; lakini wale waliochaguliwa walikipata, na wengine walitiwa ugumu. Kama ilivyoandikwa, Mungu aliwapa roho ya usingizi, macho hata wasione, na masikio hata wasisikie, hata siku hii ya leo. Na Daudi asema, Meza yao na iwe tanzi na mtego, Na kitu cha kuwakwaza, na malipo kwao; Macho yao yatiwe giza ili wasione, Ukawainamishe mgongo wao siku zote. Basi nasema, Je! Wamejikwaa hata waanguke kabisa? La hasha! Lakini kwa kosa lao wokovu umewafikia Mataifa, ili wao wenyewe watiwe wivu. Basi, ikiwa kosa lao limekuwa utajiri wa ulimwengu, na upungufu wao umekuwa utajiri wa Mataifa, je! Si zaidi sana utimilifu wao? Lakini nasema na ninyi, mlio watu wa Mataifa. Basi, kwa kadiri nilivyo mtume wa watu wa Mataifa, naitukuza huduma iliyo yangu, nipate kuwatia wivu walio damu moja na mimi na kuwaokoa baadhi yao. Maana ikiwa kutupwa kwao kumeleta upatanisho kwa ulimwengu, je! Kukubaliwa kwao kutakuwa nini kama si uhai baada ya kufa? Tena malimbuko yakiwa matakatifu, kadhalika na donge lote; na shina likiwa takatifu, matawi nayo kadhalika. Lakini iwapo matawi mengine yamekatwa, na wewe mzeituni mwitu ulipandikizwa kati yao, ukawa mshirika wa shina la mzeituni na unono wake, usijisifu juu ya matawi yale; au ikiwa wajisifu, si wewe ulichukuaye shina, bali ni shina likuchukualo wewe. Basi utasema, Matawi yale yalikatwa kusudi ili nipandikizwe mimi. Vema. Yalikatwa kwa kutoamini kwao, na wewe wasimama kwa imani yako. Usijivune, bali uogope. Kwa maana ikiwa Mungu hakuyaachia matawi ya asili, wala hatakuachia wewe. Tazama, basi, wema na ukali wa Mungu; kwa wale walioanguka, ukali, bali kwako wewe wema wa Mungu, ukikaa katika wema huo; kama sivyo, wewe nawe utakatiliwa mbali. Na hao pia, wasipokaa katika kutoamini kwao, watapandikizwa; kwa kuwa Mungu aweza kuwapandikiza tena. Kwa maana ikiwa wewe ulikatwa ukatolewa katika mzeituni, ulio mzeituni mwitu kwa asili yake, kisha ukapandikizwa, kinyume cha asili, katika mzeituni ulio mwema, si zaidi sana wale walio wa asili kuweza kupandikizwa katika mzeituni wao wenyewe? Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili. Hivyo Israeli wote wataokoka; kama ilivyoandikwa, Mwokozi atakuja kutoka Sayuni; Atamtenga Yakobo na maasia yake. Na hili ndilo agano langu nao, Nitakapowaondolea dhambi zao. Basi kwa habari ya Injili wamekuwa adui kwa ajili yenu; bali kwa habari ya kule kuchaguliwa wamekuwa wapenzi kwa ajili ya baba zetu. Kwa sababu karama za Mungu hazina majuto, wala mwito wake. Kwa maana kama ninyi zamani mlivyomwasi Mungu, lakini sasa mmepata rehema kwa kuasi kwao; kadhalika na hao wameasi sasa, ili kwa kupata rehema kwenu wao nao wapate rehema. Maana Mungu amewafunga wote pamoja katika kuasi ili awarehemu wote.

Shirikisha
Soma Waroma 11

Waroma 11:1-32 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi, nauliza, Je! Mungu aliwasukumia mbali watu wake? Hasha! Kwa kuwa mimi nami ni Mwisraeli, mmoja wa wazao wa Ibrahimu, mtu wa kabila ya Benyamini. Mungu hakuwasukumia mbali watu wake aliowajua tokea awali. Au hamjui yale yaliyonenwa na maandiko juu ya Eliya? Jinsi anavyowashitaki Waisraeli mbele za Mungu, Bwana, wamewaua manabii wako, wamezibomoa madhabahu zako, nami nimesalia peke yangu, nao wananitafuta roho yangu. Lakini ile jawabu ya Mungu yamwambiaje? Nimejisazia watu elfu saba wasiopiga goti mbele ya Baali. Basi ni vivi hivi wakati huu wa sasa, yako mabaki waliochaguliwa kwa neema. Lakini ikiwa ni kwa neema, haiwi kwa matendo tena, au hapo neema isingekuwa neema. Imekuwaje basi? Kitu kile ambacho Israeli alikuwa akikitafuta hakukipata; lakini wale waliochaguliwa walikipata, na wengine walitiwa uzito. Kama ilivyoandikwa, Mungu aliwapa roho ya usingizi, macho hata wasione, na masikio hata wasisikie, hata siku hii ya leo. Na Daudi asema, Meza yao na iwe tanzi na mtego, Na kitu cha kuwakwaza, na malipo kwao; Macho yao yatiwe giza ili wasione, Ukawainamishe mgongo wao siku zote. Basi nasema, Je! Wamejikwaa hata waanguke kabisa? Hasha! Lakini kwa kosa lao wokovu umewafikilia Mataifa, ili wao wenyewe watiwe wivu. Basi, ikiwa kosa lao limekuwa utajiri wa ulimwengu, na upungufu wao umekuwa utajiri wa Mataifa, je! Si zaidi sana utimilifu wao? Lakini nasema na ninyi, mlio watu wa Mataifa. Basi, kwa kadiri nilivyo mtume wa watu wa Mataifa, naitukuza huduma iliyo yangu, nipate kuwatia wivu walio damu moja na mimi na kuwaokoa baadhi yao. Maana ikiwa kutupwa kwao kumeleta upatanisho kwa ulimwengu, je! Kukubaliwa kwao kutakuwa nini kama si uhai baada ya kufa? Tena malimbuko yakiwa matakatifu, kadhalika na donge lote; na shina likiwa takatifu, matawi nayo kadhalika. Lakini iwapo matawi mengine yamekatwa, na wewe mzeituni mwitu ulipandikizwa kati yao, ukawa mshirika wa shina la mzeituni na unono wake, usijisifu juu ya matawi yale; au ikiwa wajisifu, si wewe ulichukuaye shina, bali ni shina likuchukualo wewe. Basi utasema, Matawi yale yalikatwa kusudi ili nipandikizwe mimi. Vema. Yalikatwa kwa kutokuamini kwao, na wewe wasimama kwa imani yako. Usijivune, bali uogope. Kwa maana ikiwa Mungu hakuyaachia matawi ya asili, wala hatakuachia wewe. Tazama, basi, wema na ukali wa Mungu; kwa wale walioanguka, ukali, bali kwako wewe wema wa Mungu, ukikaa katika wema huo; kama sivyo, wewe nawe utakatiliwa mbali. Na hao pia, wasipokaa katika kutokuamini kwao, watapandikizwa; kwa kuwa Mungu aweza kuwapandikiza tena. Kwa maana ikiwa wewe ulikatwa ukatolewa katika mzeituni, ulio mzeituni mwitu kwa asili yake, kisha ukapandikizwa, kinyume cha asili, katika mzeituni ulio mwema, si zaidi sana wale walio wa asili kuweza kupandikizwa katika mzeituni wao wenyewe? Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili. Hivyo Israeli wote wataokoka; kama ilivyoandikwa, Mwokozi atakuja kutoka Sayuni; Atamtenga Yakobo na maasia yake. Na hili ndilo agano langu nao, Nitakapowaondolea dhambi zao. Basi kwa habari ya Injili wamekuwa adui kwa ajili yenu; bali kwa habari ya kule kuchaguliwa wamekuwa wapenzi kwa ajili ya baba zetu. Kwa sababu karama za Mungu hazina majuto, wala mwito wake. Kwa maana kama ninyi zamani mlivyomwasi Mungu, lakini sasa mmepata rehema kwa kuasi kwao; kadhalika na hao wameasi sasa, ili kwa kupata rehema kwenu wao nao wapate rehema. Maana Mungu amewafunga wote pamoja katika kuasi ili awarehemu wote.

Shirikisha
Soma Waroma 11

Waroma 11:1-32 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Basi nauliza: Je, Mungu amewakataa watu wake? La, hasha! Mimi mwenyewe ni Mwisraeli, tena uzao wa Abrahamu kutoka kabila la Benyamini. Mungu hajawakataa watu wake, ambao yeye aliwajua tangu mwanzo. Je, hamjui yale Maandiko yasemayo kuhusu Eliya, jinsi alivyomlalamikia Mungu kuhusu Israeli? Alisema, “Bwana, wamewaua manabii wako na kuzibomoa madhabahu zako, nimebaki mimi peke yangu, nao wanataka kuniua?” Je, Mungu alimjibuje? “Nimejibakizia watu elfu saba ambao hawajapiga magoti kumwabudu Baali.” Vivyo hivyo pia, sasa wapo mabaki waliochaguliwa kwa neema ya Mungu. Lakini ikiwa wamechaguliwa kwa neema, si tena kwa msingi wa matendo. Kama ingekuwa kwa matendo, neema isingekuwa neema tena. Tuseme nini basi? Kile kitu ambacho Israeli alikitafuta kwa bidii hakukipata. Lakini waliochaguliwa walikipata. Waliobaki walifanywa wagumu, kama ilivyoandikwa: “Mungu aliwapa bumbuazi la mioyo, macho ili wasiweze kuona, na masikio ili wasiweze kusikia, hadi leo.” Naye Daudi anasema: “Karamu zao na ziwe tanzi na mtego wa kuwanasa, kitu cha kuwakwaza waanguke, na adhabu kwao. Macho yao yatiwe giza ili wasiweze kuona, nayo migongo yao iinamishwe daima.” Hivyo nauliza tena: Je, Waisraeli walijikwaa ili waanguke na kuangamia kabisa? La, hasha! Lakini kwa sababu ya makosa yao, wokovu umewafikia watu wa Mataifa, ili kuwafanya Waisraeli waone wivu. Basi ikiwa kukosa kwao kumekuwa utajiri mkubwa kwa ulimwengu, tena kama kuangamia kwao kumeleta utajiri kwa watu wa Mataifa, kurudishwa kwao kutaleta utajiri mkuu zaidi. Sasa ninasema nanyi watu wa Mataifa. Maadamu mimi ni mtume kwa watu wa Mataifa, naitukuza huduma yangu ili kuwafanya watu wangu waone wivu na hivyo kuwaokoa baadhi yao. Kwa kuwa ikiwa kukataliwa kwao ni kupatanishwa kwa ulimwengu, kukubaliwa kwao si kutakuwa ni uhai baada ya kufa? Kama sehemu ya donge la unga uliotolewa kuwa limbuko ni mtakatifu, basi unga wote ni mtakatifu, nalo shina kama ni takatifu, vivyo hivyo na matawi nayo. Lakini kama baadhi ya matawi yalikatwa, nawe chipukizi la mzeituni mwitu ukapandikizwa mahali pao ili kushiriki unono pamoja na matawi mengine kutoka shina la mzeituni, basi usijivune juu ya hayo matawi. Lakini ukijivuna, kumbuka jambo hili: Si wewe unayelishikilia shina, bali ni shina linalokushikilia wewe. Basi utasema, “Matawi yale yalikatwa ili nipate kupandikizwa katika hilo shina.” Hii ni kweli. Matawi hayo yalikatwa kwa sababu ya kutokuamini kwake, lakini wewe umesimama tu kwa sababu ya imani. Kwa hiyo usijivune, bali simama kwa kuogopa. Kwa maana kama Mungu hakuyahurumia matawi ya asili, wala hatakuhurumia wewe. Angalia basi wema na ukali wa Mungu: Ukali kwa wale walioanguka, bali wema wa Mungu kwako wewe, kama utadumu katika wema wake. La sivyo, nawe utakatiliwa mbali. Wao nao wasipodumu katika kutokuamini kwao, watapandikizwa tena kwenye shina, kwa maana Mungu anao uwezo wa kuwapandikiza tena kwenye hilo shina. Ikiwa wewe ulikatwa kutoka kile ambacho kwa asili ni mzeituni mwitu, na kupandikizwa kinyume cha asili kwenye mzeituni uliopandwa, si rahisi zaidi matawi haya ya asili kupandikizwa tena kwenye shina lake la mzeituni wao mwenyewe! Ndugu zangu, ili msije mkajidai kuwa wenye hekima kuliko mlivyo, nataka mfahamu siri hii: Ugumu umewapata Israeli kwa sehemu hadi idadi ya watu wa Mataifa watakaoingia itimie. Hivyo Israeli wote wataokolewa. Kama ilivyoandikwa: “Mkombozi atakuja kutoka Sayuni; ataondoa kutokumcha Mungu katika Yakobo. Hili ndilo agano langu nao nitakapoziondoa dhambi zao.” Kwa habari ya Injili, wao ni adui wa Mungu kwa ajili yenu, lakini kuhusu kule kuteuliwa kwao ni wapendwa, kwa ajili ya baba zao wa zamani; kwa maana akishawapa watu karama, Mungu haziondoi, wala wito wake. Kama vile ninyi wakati fulani mlivyokuwa waasi kwa Mungu lakini sasa mmepata rehema kwa sababu ya kutokutii kwao, hivyo nao Waisraeli wamekuwa waasi ili wao nao sasa waweze kupata rehema kwa ajili ya rehema za Mungu kwenu. Kwa maana Mungu amewafunga wanadamu wote kwenye kuasi ili apate kuwarehemu wote.

Shirikisha
Soma Waroma 11