Ufunuo 6:12-17
Ufunuo 6:12-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha nikatazama, na wakati Mwanakondoo alipouvunja mhuri wa sita, kukawa na tetemeko kubwa la ardhi; jua likawa jeusi kama gunia la manyoya; mwezi wote ukawa mwekundu kama damu; nazo nyota za mbingu zikaanguka juu ya ardhi kama matunda ya mtini yasiyokomaa yaangukavyo wakati mti wake unapotikiswa na upepo mkali. Anga likatoweka kama vile karatasi inavyokunjwakunjwa; milima yote na visima vyote vikaondolewa mahali pake. Kisha, wafalme wa duniani, wakuu, majemadari, matajiri, wenye nguvu, kila mtumwa na mtu huru, wakajificha mapangoni na kwenye miamba milimani. Wakaiambia hiyo milima na hayo majabali, “Tuangukieni, mkatufiche mbali na yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na mbali na ghadhabu ya Mwanakondoo! Maana siku maalumu ya ghadhabu yao imefika. Nani awezaye kuikabili?”
Ufunuo 6:12-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nami nikaona, alipoufungua mhuri wa sita, palikuwa na tetemeko kuu la nchi; jua likawa jeusi kama gunia la singa, mwezi wote ukawa kama damu, na nyota zikaanguka juu ya nchi kama vile mtini upukutishavyo mapooza yake, utikiswapo na upepo mwingi. Mbingu zikaondolewa kama ukurasa ulivyokunjwa, na kila mlima na kisiwa kikahamishwa kutoka mahali pake. Na wafalme wa dunia, na wakuu, na majemadari, na matajiri, na wenye nguvu, na kila mtumwa, na muungwana, wakajificha katika pango na chini ya miamba ya milima, wakiiambia milima na miamba, Tuangukieni, tusitirini, mbele za uso wake yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na kwenye hasira ya Mwana-kondoo. Kwa maana siku iliyo kuu, ya hasira yao, imekuja; naye ni nani awezaye kuistahimili?
Ufunuo 6:12-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nami nikaona, alipoifungua muhuri ya sita, palikuwa na tetemeko kuu la nchi; jua likawa jeusi kama gunia la singa, mwezi wote ukawa kama damu, na nyota zikaanguka juu ya nchi kama vile mtini upukutishavyo mapooza yake, utikiswapo na upepo mwingi. Mbingu zikaondolewa kama ukurasa ulivyokunjwa, na kila mlima na kisiwa kikahamishwa kutoka mahali pake. Na wafalme wa dunia, na wakuu, na majemadari, na matajiri, na wenye nguvu, na kila mtumwa, na mwungwana, wakajificha katika pango na chini ya miamba ya milima, wakiiambia milima na miamba, Tuangukieni, tusitirini, mbele za uso wake yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na hasira ya Mwana-Kondoo. Kwa maana siku iliyo kuu, ya hasira yao, imekuja; naye ni nani awezaye kusimama?
Ufunuo 6:12-17 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Nikatazama alipouvunja ule muhuri wa sita. Pakatokea tetemeko kuu la ardhi, na jua likawa jeusi kama gunia lililotengenezwa kwa singa za mbuzi, na mwezi wote ukawa mwekundu kama damu. Nyota zilizo angani zikaanguka ardhini kama vile matunda ya mtini yasiyokomaa yaangukavyo wakati mti wake unapotikiswa na upepo mkali. Anga ikatoweka kama vile karatasi isokotwavyo, na kila mlima na kila kisiwa kikaondolewa mahali pake. Ndipo wafalme wa dunia, wakuu wote, majemadari, matajiri, wenye nguvu na kila mtu, mtumwa na mtu huru, wakajificha katika mapango na kwenye miamba ya milima. Wakaiita milima na miamba wakisema, “Tuangukieni, mkatufiche na uso wake yeye aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi, na mkatuepushe na ghadhabu ya Mwana-Kondoo! Kwa maana siku ile kuu ya ghadhabu yao imewadia. Je, ni nani awezaye kustahimili?”