Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ufunuo 6:1-17 - Compare All Versions

Ufunuo 6:1-17 BHN (Biblia Habari Njema)

Kisha, nikamwona Mwanakondoo anavunja mhuri mmojawapo wa ile mihuri saba. Nikasikia mmoja wa wale viumbe hai wanne akisema kwa sauti kama ya ngurumo, “Njoo!” Mimi nikatazama, na kumbe palikuwa na farasi mmoja mweupe hapo. Na mpandafarasi wake alikuwa na upinde, akapewa na taji. Basi, akatoka kama mshindi, aendelee kushinda. Kisha, Mwanakondoo akavunja mhuri wa pili. Nikamsikia yule kiumbe hai wa pili akisema, “Njoo!” Nami nikatazama na kumbe palikuwapo farasi mwingine hapo, mwekundu. Mpandafarasi wake alikabidhiwa jukumu la kuondoa amani duniani, watu wauane, naye akapewa upanga mkubwa. Kisha Mwanakondoo akavunja mhuri wa tatu. Nikamsikia yule kiumbe hai wa tatu akisema, “Njoo!” Nikatazama na kumbe palikuwapo farasi mmoja hapo, mweusi. Mpandafarasi wake alikuwa na vipimo viwili vya kupimia uzito mkononi mwake. Nikasikia kitu kama sauti itokayo kwa wale viumbe hai wanne. Nayo ilisema, “Kibaba kimoja cha unga wa ngano kwa kiasi cha fedha denari moja, na vibaba vitatu vya shayiri kwa denari moja. Lakini usiharibu mafuta wala divai!” Kisha, Mwanakondoo akavunja mhuri wa nne. Nikamsikia yule kiumbe hai wa nne akisema, “Njoo!” Nami nikatazama, na kumbe alikuwapo farasi mmoja hapo, rangi yake kijivu. Na jina la mpandafarasi wake lilikuwa Kifo, na Kuzimu alimfuata nyuma. Hao walipewa mamlaka juu ya robo moja ya dunia, wawaue watu kwa upanga, njaa, tauni na kwa wanyama wakali wa dunia. Kisha, Mwanakondoo akavunja mhuri wa tano. Nikaona pale chini ya madhabahu ya kufukizia ubani roho za wale waliouawa kwa sababu ya ujumbe wa Mungu, na kwa sababu ya ushuhuda waliotoa. Basi, wakalia kwa sauti kubwa: “Ee Bwana, uliye mtakatifu na mwaminifu, mpaka lini utakawia kulipiza kisasi kwa wakazi wote wa dunia kwa ajili ya kuuawa kwetu?” Wakapewa kila mmoja vazi refu jeupe, wakaambiwa wazidi kusubiri kwa muda mfupi, mpaka itakapotimia idadi ya watumishi wenzao na ndugu ambao watauawa kama wao wenyewe walivyouawa. Kisha nikatazama, na wakati Mwanakondoo alipouvunja mhuri wa sita, kukawa na tetemeko kubwa la ardhi; jua likawa jeusi kama gunia la manyoya; mwezi wote ukawa mwekundu kama damu; nazo nyota za mbingu zikaanguka juu ya ardhi kama matunda ya mtini yasiyokomaa yaangukavyo wakati mti wake unapotikiswa na upepo mkali. Anga likatoweka kama vile karatasi inavyokunjwakunjwa; milima yote na visima vyote vikaondolewa mahali pake. Kisha, wafalme wa duniani, wakuu, majemadari, matajiri, wenye nguvu, kila mtumwa na mtu huru, wakajificha mapangoni na kwenye miamba milimani. Wakaiambia hiyo milima na hayo majabali, “Tuangukieni, mkatufiche mbali na yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na mbali na ghadhabu ya Mwanakondoo! Maana siku maalumu ya ghadhabu yao imefika. Nani awezaye kuikabili?”

Shirikisha
Ufunuo 6 BHN

Ufunuo 6:1-17 SRUV (Swahili Revised Union Version)

Kisha nikaona Mwana-kondoo alipofungua mojawapo ya ile mihuri saba, nikasikia mmoja wa wale wenye uhai wanne akisema, kama kwa sauti ya ngurumo, Njoo! Nikaona, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda ana uta, akapewa taji, naye akatoka, huku akishinda tena apate kushinda. Na alipoufungua mhuri wa pili, nikamsikia yule mwenye uhai wa pili akisema, Njoo! Akatoka farasi mwingine, mwekundu sana, na yeye aliyempanda aliruhusiwa kuiondoa amani katika nchi, ili watu wauane, naye akapewa upanga mkubwa. Na alipoufungua mhuri wa tatu, nikamsikia yule wa tatu mwenye uhai akisema, Njoo! Nikaona, na tazama, farasi mweusi, na yeye aliyempanda ana mizani mkononi mwake. Nikasikia kama sauti katikati ya hao wenye uhai wanne, ikisema, Kibaba cha ngano kwa nusu rupia, na vibaba vitatu vya shayiri kwa nusu rupia, wala usiyadhuru mafuta wala divai. Na alipoufungua mhuri wa nne, nikasikia sauti ya yule mwenye uhai wa nne akisema, Njoo! Nikaona, na tazama, farasi wa rangi ya kijivujivu, na yeye aliyempanda jina lake ni Mauti, na Kuzimu akafuatana naye. Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue kwa upanga na kwa njaa na kwa tauni na kwa wanyama wa nchi. Na alipoufungua mhuri wa tano, nikaona chini ya madhabahu roho zao waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu, na kwa ajili ya ushuhuda waliokuwa nao. Wakalia kwa sauti kuu, wakisema, Ee Mola, Mtakatifu, na Mkweli, utakawia hadi lini kuhukumu na kuilipa damu yetu kwa hao wakaao juu ya nchi? Nao wakapewa kila mmoja nguo ndefu, nyeupe, wakaambiwa wasubiri bado muda mchache, hadi itakapotimia idadi ya watumishi wenzao na ndugu zao, watakaouawa kama wao walivyouawa. Nami nikaona, alipoufungua mhuri wa sita, palikuwa na tetemeko kuu la nchi; jua likawa jeusi kama gunia la singa, mwezi wote ukawa kama damu, na nyota zikaanguka juu ya nchi kama vile mtini upukutishavyo mapooza yake, utikiswapo na upepo mwingi. Mbingu zikaondolewa kama ukurasa ulivyokunjwa, na kila mlima na kisiwa kikahamishwa kutoka mahali pake. Na wafalme wa dunia, na wakuu, na majemadari, na matajiri, na wenye nguvu, na kila mtumwa, na muungwana, wakajificha katika pango na chini ya miamba ya milima, wakiiambia milima na miamba, Tuangukieni, tusitirini, mbele za uso wake yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na kwenye hasira ya Mwana-kondoo. Kwa maana siku iliyo kuu, ya hasira yao, imekuja; naye ni nani awezaye kuistahimili?

Shirikisha
Ufunuo 6 SRUV

Ufunuo 6:1-17 SUV (Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia)

Kisha nikaona napo Mwana-Kondoo alipofungua moja ya zile muhuri saba, nikasikia mmoja wa wale wenye uhai wanne akisema, kama kwa sauti ya ngurumo, Njoo! Nikaona, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda ana uta, akapewa taji, naye akatoka, ali akishinda tena apate kushinda. Na alipoifungua muhuri ya pili, nikamsikia yule mwenye uhai wa pili akisema, Njoo! Akatoka farasi mwingine, mwekundu sana, na yeye aliyempanda alipewa kuiondoa amani katika nchi, ili watu wauane, naye akapewa upanga mkubwa. Na alipoifungua muhuri ya tatu, nikamsikia yule wa tatu mwenye uhai akisema, Njoo! Nikaona, na tazama, farasi mweusi, na yeye aliyempanda ana mizani mkononi mwake. Nikasikia kama sauti katikati ya hao wenye uhai wanne, ikisema, Kibaba cha ngano kwa nusu rupia, na vibaba vitatu vya shayiri kwa nusu rupia, wala usiyadhuru mafuta wala divai. Na alipoifungua muhuri ya nne, nikasikia sauti ya yule mwenye uhai wa nne akisema, Njoo! Nikaona, na tazama, farasi wa rangi ya kijivujivu, na yeye aliyempanda jina lake ni Mauti, na Kuzimu akafuatana naye. Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue kwa upanga na kwa njaa na kwa tauni na kwa hayawani wa nchi. Na alipoifungua muhuri ya tano, nikaona chini ya madhabahu roho zao waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu, na kwa ajili ya ushuhuda waliokuwa nao. Wakalia kwa sauti kuu, wakisema, Ee Mola, Mtakatifu, Mwenye kweli, hata lini kutokuhukumu, wala kuipatia haki damu yetu kwa hao wakaao juu ya nchi? Nao wakapewa kila mmoja nguo ndefu, nyeupe, wakaambiwa wastarehe bado muda mchache, hata itakapotimia hesabu ya wajoli wao na ndugu zao, watakaouawa vile vile kama wao. Nami nikaona, alipoifungua muhuri ya sita, palikuwa na tetemeko kuu la nchi; jua likawa jeusi kama gunia la singa, mwezi wote ukawa kama damu, na nyota zikaanguka juu ya nchi kama vile mtini upukutishavyo mapooza yake, utikiswapo na upepo mwingi. Mbingu zikaondolewa kama ukurasa ulivyokunjwa, na kila mlima na kisiwa kikahamishwa kutoka mahali pake. Na wafalme wa dunia, na wakuu, na majemadari, na matajiri, na wenye nguvu, na kila mtumwa, na mwungwana, wakajificha katika pango na chini ya miamba ya milima, wakiiambia milima na miamba, Tuangukieni, tusitirini, mbele za uso wake yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na hasira ya Mwana-Kondoo. Kwa maana siku iliyo kuu, ya hasira yao, imekuja; naye ni nani awezaye kusimama?

Shirikisha
Ufunuo 6 SUV

Ufunuo 6:1-17 NEN (Neno)

Nikaangalia Mwana-Kondoo alipofungua ule muhuri wa kwanza miongoni mwa mihuri saba. Ndipo nikasikia mmoja wa wale viumbe wanne wenye uhai akisema kwa sauti kama ya radi: “Njoo!” Nikatazama, na hapo mbele yangu palikuwa na farasi mweupe! Yeye aliyempanda alikuwa na upinde, naye akapewa taji, akampanda akatoka akiwa kama mshindi aelekeaye katika kushinda. Alipouvunja ule muhuri wa pili, nikamsikia yule kiumbe wa pili mwenye uhai akisema, “Njoo!” Ndipo akatokea farasi mwingine mwekundu sana. Yeye aliyempanda akapewa uwezo wa kuondoa amani duniani na kuwafanya watu wauane. Yeye akapewa upanga mkubwa. Mwana-kondoo alipouvunja ule muhuri wa tatu, nikamsikia yule kiumbe wa tatu mwenye uhai akisema, “Njoo!” Nikatazama, na mbele yangu palikuwa na farasi mweusi! Yeye aliyempanda alikuwa na mizani mkononi mwake. Ndipo nikasikia kile kilichokuwa kama sauti katikati ya wale viumbe wanne wenye uhai ikisema, “Kipimo kimoja cha ngano kwa mshahara wa kibarua wa siku moja, na vipimo vitatu vya shayiri kwa mshahara wa kibarua cha siku moja. Lakini usiharibu mafuta wala divai!” Alipouvunja ule muhuri wa nne, nikasikia sauti ya yule kiumbe wa nne mwenye uhai ikisema, “Njoo!” Nikatazama, na hapo mbele yangu palikuwa na farasi mwenye rangi ya kijivujivu! Yeye aliyempanda aliitwa Mauti, naye Kuzimu alikuwa akimfuata nyuma yake kwa karibu. Wakapewa mamlaka juu ya robo ya dunia, kuua kwa upanga, njaa, tauni na kwa wanyama wakali wa dunia. Mwana-kondoo alipouvunja ule muhuri wa tano, nikaona chini ya madhabahu, roho za wale waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu na kwa ajili ya ushuhuda walioutunza. Wakalia kwa sauti kuu, wakasema, “Hata lini, Ee Bwana Mwenyezi, uliye mtakatifu na mwaminifu, hutawahukumu na kulipiza kisasi kwa watu wanaoishi duniani kwa ajili ya damu yetu?” Kisha kila mmoja wao akapewa joho jeupe na wakaambiwa wangoje kwa muda kidogo zaidi, hadi idadi ya ndugu zao na watumishi wenzao watakaouawa kama wao walivyouawa, itakapotimia. Nikatazama alipouvunja ule muhuri wa sita. Pakatokea tetemeko kuu la ardhi, na jua likawa jeusi kama gunia lililotengenezwa kwa singa za mbuzi, na mwezi wote ukawa mwekundu kama damu. Nyota zilizo angani zikaanguka ardhini kama vile matunda ya mtini yasiyokomaa yaangukavyo wakati mti wake unapotikiswa na upepo mkali. Anga ikatoweka kama vile karatasi isokotwavyo, na kila mlima na kila kisiwa kikaondolewa mahali pake. Ndipo wafalme wa dunia, wakuu wote, majemadari, matajiri, wenye nguvu na kila mtu, mtumwa na mtu huru, wakajificha katika mapango na kwenye miamba ya milima. Wakaiita milima na miamba wakisema, “Tuangukieni, mkatufiche na uso wake yeye aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi, na mkatuepushe na ghadhabu ya Mwana-Kondoo! Kwa maana siku ile kuu ya ghadhabu yao imewadia. Je, ni nani awezaye kustahimili?”

Shirikisha
Ufunuo 6 NEN