Zaburi 81:1-16
Zaburi 81:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwimbieni kwa sauti Mungu, nguvu yetu, mshangilieni Mungu wa Yakobo; vumisheni wimbo wa shangwe, pigeni ngoma, chezeni zeze na kinubi cha sauti nzuri. Pigeni tarumbeta kutangaza mwezi mwandamo, na pia mwezi mpevu, wakati wa sikukuu yetu. Hiyo ndiyo kanuni katika Israeli; hilo ndilo agizo la Mungu wa Yakobo. Aliwapa watu wa Israeli agizo hilo, alipoishambulia nchi ya Misri. Nasikia sauti nisiyoitambua ikisema: “Mimi nilikutua mizigo yako mabegani, nilikuondolea matofali uliyochukua mikononi. Ukiwa shidani uliniita, nami nikakuokoa. Nilikujibu nikiwa mafichoni katika ngurumo. Nilikujaribu kwenye maji ya Meriba. Enyi watu wangu, sikieni onyo langu. Laiti ungenisikiliza, ee Israeli! Asiwepo kwako mungu wa kigeni; usiabudu kamwe mungu mwingine. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri. Fumbua kinywa chako, nami nitakulisha. “Lakini watu wangu hawakunisikiliza; Israeli hakunitaka kabisa. Hivyo, nikawaacha wabaki na ukaidi wao; wafuate mashauri yao wenyewe. Laiti watu wangu wangenisikiliza! Laiti Israeli angefuata njia yangu! Ningewashinda maadui zao haraka; ningenyosha mkono dhidi ya wadhalimu wao. Wanichukiao wangenipigia magoti kwa hofu, na adhabu yao ingekuwa ya milele. Lakini wewe ningekulisha kwa ngano bora, ningekushibisha kwa asali ya mwambani.”
Zaburi 81:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mwimbieni Mungu, nguvu zetu, nyimbo za furaha, Mshangilieni Mungu wa Yakobo. Pazeni zaburi, pigeni matari, Kinubi chenye sauti nzuri, na kinanda. Pigeni panda mwandamo wa mwezi, Kukiwa na mbalamwezi, wakati wa sikukuu yetu. Kwa maana ni sheria kwa Israeli, Ni hukumu ya Mungu wa Yakobo. Aliamuru iwe ushuhuda katika Yusufu, Alipoondoka juu ya nchi ya Misri; Maneno yake nisiyemjua niliyasikia. Nimeutua mzigo begani mwake; Mikono yake nikaiondolea kazi nzito. Katika shida uliniita nikakuokoa; Nilikuitikia kutoka maficho yangu ya radi; Nilikujaribu penye maji ya Meriba. Enyi watu wangu, sikieni, nami nitawaonya, Ee Israeli, kama ukitaka kunisikiliza; Usiwe na mungu mgeni ndani yako; Wala usimsujudie mungu mwingine. Mimi ndimi BWANA, Mungu wako, Niliyekupandisha toka nchi ya Misri; Fumbua sana kinywa chako nami nitakijaza. Lakini watu wangu hawakuisikiliza sauti yangu, Wala Israeli hawakunitaka. Nikawaacha wakaenda kwa ukaidi wa mioyo yao, Waenende katika mashauri yao. Laiti watu wangu wangenisikiliza, Na Israeli angeenenda katika njia zangu; Ningewadhili adui zao kwa upesi, Na juu ya watesi wao ningegeuza mkono wangu; Wamchukiao BWANA wangenyenyekea mbele zake, Na maangamizi yao yangedumu milele. Naam, ningewalisha kwa ngano iliyo bora zaidi, Ningewashibisha kwa asali itokayo mwambani.
Zaburi 81:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mwimbieni Mungu, nguvu zetu, nyimbo za furaha, Mshangilieni Mungu wa Yakobo. Pazeni zaburi, pigeni matari, Kinubi chenye sauti nzuri, na kinanda. Pigeni panda mwandamo wa mwezi, Wakati wa mbalamwezi, sikukuu yetu. Kwa maana ni sheria kwa Israeli, Ni hukumu ya Mungu wa Yakobo. Aliamuru iwe ushuhuda katika Yusufu, Alipoondoka juu ya nchi ya Misri; Maneno yake nisiyemjua naliyasikia. Nimelitenga bega lake na mzigo, Mikono yake ikaachana na kikapu. Katika shida uliniita nikakuokoa; Nalikuitikia katika sitara ya radi; Nalikujaribu penye maji ya Meriba. Enyi watu wangu, sikieni, nami nitawaonya, Ee Israeli, kama ukitaka kunisikiliza; Usiwe na mungu mgeni ndani yako; Wala usimsujudie mungu mwingine. Mimi ndimi BWANA, Mungu wako, Niliyekupandisha toka nchi ya Misri; Fumbua sana kinywa chako nami nitakijaza. Lakini watu wangu hawakuisikiliza sauti yangu, Wala Israeli hawakunitaka. Nikawaacha wakaenda kwa ukaidi wa mioyo yao, Waenende katika mashauri yao. Laiti watu wangu wangenisikiliza, Na Israeli angeenenda katika njia zangu; Ningewadhili adui zao kwa upesi, Na juu ya watesi wao ningegeuza mkono wangu; Wamchukiao BWANA wangenyenyekea mbele zake, Bali wakati wao ungedumu milele. Naam, ningewalisha kwa unono wa ngano, Ningewashibisha kwa asali itokayo mwambani.
Zaburi 81:1-16 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mwimbieni kwa furaha, Mungu aliye nguvu yetu; mpigieni kelele za shangwe Mungu wa Yakobo! Anzeni wimbo, pigeni matari, pigeni kinubi na zeze kwa sauti nzuri. Pigeni baragumu za pembe za kondoo dume wakati wa Mwandamo wa Mwezi, na wakati wa mwezi mpevu, katika siku ya Sikukuu yetu; hii ni amri kwa Israeli, agizo la Mungu wa Yakobo. Aliiweka iwe kama sheria kwa Yosefu alipotoka dhidi ya Misri, huko tulikosikia lugha ambayo hatukuielewa. Asema, “Nimeondoa mzigo mabegani mwao; mikono yao iliwekwa huru kutoka kwenye kikapu. Katika shida yako uliniita nami nikakuokoa, nilikujibu katika mawingu yenye ngurumo; nilikujaribu katika maji ya Meriba. “Enyi watu wangu, sikieni, nami nitawaonya: laiti kama mngenisikiliza, ee Israeli! Hamtakuwa na mungu mgeni miongoni mwenu; msimsujudie mungu wa kigeni. Mimi ni BWANA Mungu wako, niliyekutoa nchi ya Misri. Panua sana kinywa chako nami nitakijaza. “Lakini watu wangu hawakutaka kunisikiliza; Israeli hakutaka kunitii. Basi niliwaacha katika ukaidi wa mioyo yao wafuate mashauri yao wenyewe. “Laiti kama watu wangu wangalinisikiliza, kama Israeli wangalifuata njia zangu, ningaliwatiisha adui zao kwa haraka, na kuugeuza mkono wangu dhidi ya watesi wao! Wale wanaomchukia BWANA wangalinyenyekea mbele zake, na adhabu yao ingedumu milele. Bali ninyi mngalilishwa ngano iliyo bora, na kuwatosheleza kwa asali itokayo kwenye mwamba.”