Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 78:1-72

Zaburi 78:1-72 Biblia Habari Njema (BHN)

Sikieni mafundisho yangu, enyi watu wangu; yategeeni sikio maneno ya kinywa changu. Nitasema nanyi kwa mafumbo, nitasema mambo yaliyofichika tangu kale; mambo tuliyoyasikia na kuyajua, mambo ambayo wazee wetu walitusimulia. Hatutawaficha watoto wetu; ila tutakisimulia kizazi kijacho matendo matukufu ya Mwenyezi-Mungu na uwezo wake; tutawaambia maajabu yake aliyotenda. Aliwapa wazawa wa Yakobo masharti, aliweka sheria katika Israeli, ambayo aliwaamuru wazee wetu wawafundishe watoto wao; ili watu wa kizazi kijacho, watoto watakaozaliwa baadaye, wazijue, nao pia wawajulishe watoto wao, ili wamwekee Mungu tumaini lao, wasije wakasahau matendo ya Mungu, bali wazingatie amri zake. Wasiwe kama walivyokuwa wazee wao, watu wakaidi na waasi; kizazi ambacho hakikuwa na msimamo thabiti, ambacho hakikuwa na uaminifu kwa Mungu. Watu wa Efraimu, pinde na mishale mkononi, walirudi nyuma, wakakimbia siku ile ya vita. Hawakulizingatia agano la Mungu; walikataa kufuata sheria yake. Walisahau mambo aliyokuwa ametenda, miujiza aliyokuwa amewaonesha. Alifanya maajabu mbele ya wazee wao, kondeni Soani, nchini Misri. Aliigawa bahari, akawapitisha humo; aliyafanya maji yasimame kama ukuta. Mchana aliwaongoza kwa wingu; usiku kucha kwa mwanga wa moto. Aliipasua miamba kule jangwani, akawanywesha maji kutoka vilindini. Alibubujisha vijito kutoka mwambani, akatiririsha maji kama mito. Hata hivyo waliendelea kumkosea Mungu; walimwasi Mungu Mkuu kule jangwani. Walimjaribu Mungu kwa makusudi; wakidai wapewe chakula walichotaka. Walimkufuru Mungu wakisema: “Je, Mungu aweza kutupa chakula jangwani? Ni kweli, aliupiga mwamba, maji yakabubujika kama mto; lakini, sasa aweza kweli kutupatia mkate, na kuwapatia watu wake nyama?” Mwenyezi-Mungu, aliposikia hayo, alijawa na ghadhabu, moto ukawawakia wazawa wa Yakobo; hasira yake ikawavamia watu wa Israeli, kwa sababu hawakuwa na imani naye, wala hawakuamini nguvu yake ya kuokoa. Hata hivyo aliyaamuru mawingu ya juu, akaifungua milango ya mbingu; akawanyeshea mana wale, akawapa nafaka kutoka mbinguni. Binadamu, wakala chakula cha malaika; naye aliwapelekea chakula cha kutosha. Alivumisha upepo wa mashariki, kwa nguvu yake akachochea pepo za kusini; akawanyeshea watu wake nyama kama vumbi, ndege wengi kama mchanga wa pwani; ndege hao walianguka kambini mwao, kila mahali kuzunguka makao yao. Watu walikula wakashiba; Mungu aliwapa walichotaka. Lakini hata kabla ya kutosheleza hamu yao, chakula kikiwa bado mdomoni mwao, hasira ya Mungu iliwaka juu yao; akawaua wenye nguvu miongoni mwao, na kuwaangusha vijana wa Israeli. Hata hivyo waliendelea kumkosea Mungu; ijapokuwa alitenda maajabu, hawakuamini. Basi, akazikatisha siku zao kama pumzi, miaka yao kwa maafa ya ghafla. Kila alipowaua, waliobaki walimgeukia; walitubu, wakamgeukia Mungu kwa moyo. Walikumbuka kwamba Mungu alikuwa mwamba wao; Mungu Mkuu alikuwa mkombozi wao. Lakini walimdanganya kwa maneno yao; kila walichomwambia kilikuwa uongo. Hawakuambatana naye kwa moyo, hawakuwa waaminifu kwa agano lake. Lakini Mungu mwenye huruma alisamehe uovu wao, na wala hakuwaangamiza. Mara nyingi aliizuia hasira yake, wala hakuiacha ghadhabu yake yote iwake. Alikumbuka kwamba wao ni watu tu; ni kama upepo upitao na kutoweka. Mara ngapi walimwasi kule jangwani, na kumchukiza hukohuko nyikani! Walimjaribu Mungu tena na tena, wakamkasirisha huyo Mtakatifu wa Israeli. Hawakuikumbuka nguvu yake, wala siku ile alipowaokoa na maadui zao, alipotenda maajabu nchini Misri, na miujiza kondeni Soani! Aliigeuza ile mito kuwa damu, Wamisri wasipate maji ya kunywa. Aliwapelekea makundi ya nzi waliowasumbua, na vyura waliowatia hasara. Alituma nzige, wakala mavuno yao, na kuharibu mashamba yao. Aliiharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe, na mitini yao kwa baridi kali. Ngombe wao aliwaua kwa mvua ya mawe, na kondoo wao kwa radi. Aliacha hasira yake kali iwawakie, ghadhabu, chuki na dhiki, na kundi la malaika waangamizi. Aliachilia hasira yake iendelee, wala hakuwaepusha na kifo, bali aliwaangamiza kwa tauni. Aliwaua wazaliwa wa kwanza wote wa Wamisri; naam, chipukizi wa kwanza kambini mwa Hamu. Kisha aliwahamisha watu wake kama kondoo, akawaongoza jangwani kama kundi la mifugo. Aliwaogoza salama, wala hawakuogopa; lakini bahari iliwafunika maadui zao. Aliwaleta katika nchi yake takatifu, katika mlima aliouteka kwa nguvu yake. Aliyafukuza mataifa mbele yao, akazitoa nchi zao ziwe mali ya Israeli, akayakalisha makabila ya Israeli mahemani mwao. Hata hivyo walimjaribu na kumwasi Mungu Mkuu; wala hawakuzingatia masharti yake. Ila waligeuka na kufanya mabaya kama wazee wao; wakayumbayumba kama upinde usio imara. Walimkasirisha kwa madhabahu zao za miungu; wakamchochea aone wivu kwa sanamu zao za kuchonga. Mungu alipoona hayo, akawaka hasira; akamkataa Israeli katakata. Aliyaacha makao yake kule Shilo, makao ambamo alikaa kati ya watu. Aliiacha ishara ya nguvu yake itekwe, utukufu wake utiwe mikononi mwa maadui. Aliwakasirikia watu wake mwenyewe; akawatoa waangamizwe kwa upanga. Moto ukawateketeza vijana wao wa kiume, na wasichana wao wakakosa wachumba. Makuhani wao walikufa kwa upanga, wala wajane wao hawakuomboleza. Kisha Bwana aliamka kama kutoka usingizini, kama shujaa aliyechangamshwa na divai. Akawatimua maadui zake; akawatia aibu ya kudumu milele. Lakini aliikataa jamaa ya Yosefu, wala hakulichagua kabila la Efraimu. Ila alilichagua kabila la Yuda, mlima Siyoni anaoupenda. Alijenga hapo hekalu lake kubwa kama mbingu, kama dunia aliyoiweka imara milele. Alimchagua Daudi, mtumishi wake, akamtoa katika kazi ya kuchunga kondoo. Alimtoa katika kazi ya kuchunga kondoo na wanakondoo, awe na jukumu la kuchunga watu wa Yakobo taifa lake. Achunge Israeli, watu wake Mungu mwenyewe. Daudi akawafunza kwa moyo wake wote, akawaongoza kwa uhodari mkubwa.

Shirikisha
Soma Zaburi 78

Zaburi 78:1-72 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Enyi watu wangu, sikilizeni sheria yangu, Tegeni masikio kwa maneno ya kinywa changu. Nitafumbua kinywa changu kwa mithali, Niyatamke mafumbo ya kale. Mambo tuliyoyasikia na kuyafahamu, Ambayo baba zetu walituambia. Hayo hatutawaficha wana wao, Huku tukiwaambia kizazi kingine, Sifa za BWANA, na nguvu zake, Na mambo yake ya ajabu aliyoyafanya. Maana alikaza ushuhuda katika Yakobo, Na sheria aliiweka katika Israeli. Aliyowaamuru baba zetu Wawajulishe wana wao, Ili kizazi kingine wawe na habari, Ndio hao wana watakaozaliwa. Wasimame na kuwaambia wana wao. Wamwekee Mungu tumaini lao. Wala wasiyasahau matendo ya Mungu, Bali wazishike amri zake. Naam, wasiwe kama baba zao, Kizazi cha ukaidi na uasi. Kizazi kisichojitengeneza moyo, Wala roho yake haikuwa amini kwa Mungu. Wale Waefraimu, wenye silaha, wapiga upinde, Walirudi nyuma siku ya vita. Hawakulishika agano la Mungu; Wakakataa kufuata sheria yake; Wakayasahau matendo yake, Na mambo yake ya ajabu aliyowaonesha. Mbele ya baba zao alifanya mambo ya ajabu, Katika nchi ya Misri, konde la Soani. Aliipasua bahari akawavusha; Aliyafanya maji yasimame kama ukuta. Akawaongoza kwa wingu mchana, Na usiku kucha kwa nuru ya moto. Akapasua miamba jangwani; Akawanywesha maji mengi kama maji ya vilindi. Akafanya vijito vitokeze katika mwamba, Na kufanya maji yatiririke kama mito. Lakini wakazidi kumtenda dhambi, Walipomwasi Aliye Juu katika jangwa. Wakamjaribu Mungu mioyoni mwao Kwa kutaka chakula kwa tamaa zao. Naam, walimwambia Mungu, wakasema, Je! Mungu aweza kuandaa meza jangwani? Tazama, aliupiga mwamba; Maji yakabubujika, ikafurika mito. Pia aweza kutupa chakula? Atawaandalia watu wake nyama? Hivyo BWANA aliposikia akaghadhibika; Moto ukawashwa juu ya Yakobo, Hasira nayo ikapanda juu ya Israeli. Kwa kuwa hawakumwamini Mungu, Wala hawakuutumainia wokovu wake. Lakini aliyaamuru mawingu juu; Akaifungua milango ya mbinguni; Akawanyeshea mana ili wale; Akawapa nafaka ya mbinguni. Mwanadamu akala chakula walacho malaika; Akawapelekea chakula cha kuwashibisha. Aliuelekeza upepo wa mashariki kuvuma toka mbinguni; Na kwa uweza wake akauongoza upepo wa kusini. Akawanyeshea nyama kama mavumbi, Na ndege wenye mbawa, Kama mchanga wa bahari. Akawaangusha kati ya matuo yao, Pande zote za maskani zao. Wakala wakashiba sana; Maana aliwaletea walivyovitamani; Lakini kabla ya kuitosheleza shauku yao, Huku chakula kikiwa bado kinywani mwao, Hasira ya Mungu ikapanda juu yao, Akawaua waliokuwa wanono; Akawaangusha chini vijana wa Israeli. Pamoja na hayo wakazidi kutenda dhambi, Wala hawakuyaamini matendo yake ya ajabu. Kwa hiyo akazikomesha siku zao kama pumzi, Na miaka yao kwa hofu ya kuwastusha. Alipowaua ndipo walipokuwa wakimtafuta; Wakarudi wakamtaka Mungu kwa bidii. Wakakumbuka kuwa Mungu ni mwamba wao, Na Mungu Aliye Juu ni mkombozi wao. Lakini walimdanganya kwa vinywa vyao, Wakamwambia uongo kwa ndimi zao. Kwa maana mioyo yao haikuwa thabiti kwake, Wala hawakuwa waaminifu katika agano lake. Lakini Yeye, kwa kuwa anayo rehema, Husamehe uovu wala haangamizi. Mara nyingi huipishia mbali ghadhabu yake, Wala haiwashi hasira yake yote. Akakumbuka ya kuwa wao ni kiwiliwili, Upepo upitao wala haurudi. Walimwasi jangwani mara ngapi? Na kumhuzunisha nyikani! Wakamjaribu Mungu tena na tena; Na kumkasirisha Mtakatifu wa Israeli. Hawakuukumbuka mkono wake, Wala siku ile alipowakomboa na mtesi. Alivyoziweka ishara zake katika Misri, Na miujiza yake katika uwanda wa Soani. Aligeuza mito yao kuwa damu, Ili wasipate kunywa maji kutoka vijito vyao. Aliwapelekea mainzi wakawala, Na vyura wakawaharibu. Akawapa tunutu mazao yao, Na nzige matunda ya kazi yao. Aliiharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe, Na mikuyu yao kwa mawe ya barafu. Akaacha ng'ombe zao wapigwe kwa mvua ya mawe, Na makundi yao kwa umeme. Akawapelekea ukali wa hasira yake, Ghadhabu, na uchungu, na taabu, Kundi la malaika waletao mabaya. Akaifanyia njia hasira yake; Wala hakuziepusha roho zao kutoka kwa mauti, Bali aliiachia tauni uhai wao; Akampiga kila mzaliwa wa kwanza wa Misri, Malimbuko ya nguvu katika hema za Hamu. Kisha akawaongoza watu wake kama kondoo, Akawachunga kama kundi jangwani. Hao akawachukua salama wala hawakuogopa, Bali bahari iliwafunika adui zao. Akawapeleka hadi mpaka wake mtakatifu, Mlima alioununua kwa mkono wake wa kulia. Akawafukuza mataifa mbele yao, Akawapimia urithi kwa kamba, Na kuwakalisha makabila ya Israeli katika hema zao. Lakini walimjaribu Mungu Aliye Juu, wakamwasi, Wala hawakuzishika shuhuda zake. Bali walirudi nyuma, wakahaini kama baba zao; Wakayumba kama upinde usiofaa. Wakamkasirisha kwa mahali pao pa juu, Wakamtia wivu kwa sanamu zao. Mungu alisikia, akaghadhibika, Akamkataa Israeli kabisa. Akaiacha maskani ya Shilo, Hema aliyoiweka katikati ya wanadamu; Akaziacha nguvu zake kutekwa, Na fahari yake mkononi mwa mtesi. Akawatoa watu wake wapigwe kwa upanga; Akaughadhibikia urithi wake. Moto ukawala vijana wao, Wanawali wao hawakuimbiwa nyimbo za arusi, Makuhani wao walianguka kwa upanga, Wala wajane wao hawakuomboleza. Ndipo Bwana alipoamka kama aliyelala usingizi, Kama shujaa apigaye kelele kwa sababu ya mvinyo; Akawapiga watesi wake akawarudisha nyuma, Akawatia aibu ya milele. Ila akaikataa hema ya Yusufu; Wala hakuichagua kabila la Efraimu. Bali aliichagua kabila la Yuda, Mlima Sayuni alioupenda. Akajenga patakatifu pake kama vilele, Kama dunia aliyoiweka imara milele. Akamchagua Daudi, mtumishi wake, Akamwondoa katika mazizi ya kondoo. Nyuma ya kondoo wanyonyeshao alimwondoa, Awachunge Yakobo watu wake, na Israeli urithi wake. Akawahudumia kwa ukamilifu wa moyo wake, Na kuwaongoza kwa busara ya mikono yake.

Shirikisha
Soma Zaburi 78

Zaburi 78:1-72 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Enyi watu wangu, sikilizeni sheria yangu, Tegeni masikio kwa maneno ya kinywa changu. Na nifunue kinywa changu kwa mithali, Niyatamke mafumbo ya kale. Mambo tuliyoyasikia na kuyafahamu, Ambayo baba zetu walituambia. Hayo hatutawaficha wana wao, Huku tukiwaambia kizazi kingine, Sifa za BWANA, na nguvu zake, Na mambo yake ya ajabu aliyoyafanya. Maana alikaza ushuhuda katika Yakobo, Na sheria aliiweka katika Israeli. Aliyowaamuru baba zetu Wawajulishe wana wao, Ili kizazi kingine wawe na habari, Ndio hao wana watakaozaliwa. Wasimame na kuwaambia wana wao Wamwekee Mungu tumaini lao. Wala wasiyasahau matendo ya Mungu, Bali wazishike amri zake. Naam, wasiwe kama baba zao, Kizazi cha ukaidi na uasi. Kizazi kisichojitengeneza moyo, Wala roho yake haikuwa amini kwa Mungu. Wale Waefraimu, wenye silaha, wapiga upinde, Walirudi nyuma siku ya vita. Hawakulishika agano la Mungu; Wakakataa kuenenda katika sheria yake; Wakayasahau matendo yake, Na mambo yake ya ajabu aliyowaonyesha. Mbele ya baba zao alifanya mambo ya ajabu, Katika nchi ya Misri, konde la Soani. Aliipasua bahari akawavusha; Aliyasimamisha maji mfano wa chungu. Akawaongoza kwa wingu mchana, Na usiku kucha kwa nuru ya moto. Akapasua miamba jangwani; Akawanywesha maji mengi kama maji ya vilindi. Akatokeza na vijito gengeni, Akatelemsha maji kama mito. Lakini wakazidi kumtenda dhambi, Walipomwasi Aliye juu katika nchi ya kiu. Wakamjaribu Mungu mioyoni mwao Kwa kutaka chakula kwa tamaa zao. Naam, walimwamba Mungu, wakasema, Je! Mungu aweza kuandika meza jangwani? Tazama, aliupiga mwamba; Maji yakabubujika, ikafurika mito. Pia aweza kutupa chakula? Atawaandalia watu wake nyama? Hivyo BWANA aliposikia akaghadhibika; Moto ukawashwa juu ya Yakobo, Hasira nayo ikapanda juu ya Israeli. Kwa kuwa hawakumwamini Mungu, Wala hawakuutumainia wokovu wake. Lakini aliyaamuru mawingu juu; Akaifungua milango ya mbinguni; Akawanyeshea mana ili wale; Akawapa nafaka ya mbinguni. Mwanadamu akala chakula cha mashujaa; Aliwapelekea chakula cha kuwashibisha. Aliuelekeza upepo wa mashariki mbinguni; Akaiongoza kusi kwa uweza wake. Akawanyeshea nyama kama mavumbi, Na ndege wenye mbawa, Kama mchanga wa bahari. Akawaangusha kati ya matuo yao, Pande zote za maskani zao. Wakala wakashiba sana; Maana aliwaletea walivyovitamani; Hawakuachana na matakwa yao. Ila chakula chao kikali ki vinywani mwao Hasira ya Mungu ikapanda juu yao, Akawaua waliokuwa wanono; Akawaangusha chini vijana wa Israeli. Pamoja na hayo wakazidi kutenda dhambi, Wala hawakuyaamini matendo yake ya ajabu. Kwa hiyo akazikomesha siku zao kama pumzi, Na miaka yao kwa hofu ya kuwasitusha. Alipowaua ndipo walipokuwa wakimtafuta; Wakarudi wakamtaka Mungu kwa bidii. Wakakumbuka kuwa Mungu ni mwamba wao, Na Mungu Aliye juu ni mkombozi wao. Lakini walimdanganya kwa vinywa vyao, Wakamwambia uongo kwa ndimi zao. Kwa maana mioyo yao haikuwa thabiti kwake, Wala hawakuwa waaminifu katika agano lake. Lakini Yeye, kwa kuwa anayo rehema, Husamehe uovu wala haangamizi. Mara nyingi huipishia mbali ghadhabu yake, Wala haiwashi hasira yake yote. Akakumbuka ya kuwa wao ni kiwiliwili, Upepo upitao wala haurudi. Walimwasi jangwani mara ngapi? Na kumhuzunisha nyikani! Wakarudi nyuma wakamjaribu Mungu; Wakampa mpaka Mtakatifu wa Israeli. Hawakuukumbuka mkono wake, Wala siku ile alipowakomboa na mtesi. Alivyoziweka ishara zake katika Misri, Na miujiza yake katika konde la Soani. Aligeuza damu mito yao, Na vijito wasipate kunywa. Aliwapelekea mainzi wakawala, Na vyura wakawaharibu. Akawapa tunutu mazao yao, Na nzige kazi yao. Aliiharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe, Na mikuyu yao kwa mawe ya barafu. Akaacha ng’ombe zao wapigwe kwa mvua ya mawe, Na makundi yao kwa umeme. Akawapelekea ukali wa hasira yake, Ghadhabu, na uchungu, na taabu, Kundi la malaika waletao mabaya. Akiifanyizia njia hasira yake; Wala hakuziepusha roho zao na mauti, Bali aliiachia tauni uhai wao; Akampiga kila mzaliwa wa kwanza wa Misri, Malimbuko ya nguvu katika hema za Hamu. Bali aliwaongoza watu wake kama kondoo, Akawachunga kama kundi jangwani. Hao akawachukua salama wala hawakuogopa, Bali bahari iliwafunikiza adui zao. Akawapeleka hadi mpaka wake mtakatifu, Mlima alioununua kwa mkono wake wa kuume. Akawafukuza mataifa mbele yao, Akawapimia urithi kwa kamba, Na kuwakalisha kabila za Israeli katika hema zao. Lakini walimjaribu Mungu Aliye juu, wakamwasi, Wala hawakuzishika shuhuda zake. Bali walirudi nyuma, wakahaini kama baba zao; Wakaepea kama upinde usiofaa. Wakamkasirisha kwa mahali pao pa juu, Wakamtia wivu kwa sanamu zao. Mungu akasikia, akaghadhibika, Akamkataa Israeli kabisa. Akaiacha maskani ya Shilo, Hema aliyoiweka katikati ya wanadamu; Akaziacha nguvu zake kutekwa, Na fahari yake mkononi mwa mtesi. Akawatoa watu wake wapigwe kwa upanga; Akaughadhibikia urithi wake. Moto ukawala vijana wao, Wanawali wao hawakuimbiwa nyimbo za arusi, Makuhani wao walianguka kwa upanga, Wala wajane wao hawakuomboleza. Ndipo Bwana alipoamka kama aliyelala usingizi, Kama shujaa apigaye kelele sababu ya mvinyo; Akawapiga watesi wake akawarudisha nyuma, Akawatia aibu ya milele. Ila akaikataa hema ya Yusufu; Wala hakuichagua kabila ya Efraimu. Bali aliichagua kabila ya Yuda, Mlima Sayuni alioupenda. Akajenga patakatifu pake kama vilele, Kama dunia aliyoiweka imara milele. Akamchagua Daudi, mtumishi wake, Akamwondoa katika mazizi ya kondoo. Nyuma ya kondoo wanyonyeshao alimwondoa, Awachunge Yakobo watu wake, na Israeli urithi wake. Akawalisha kwa ukamilifu wa moyo wake, Na kuwaongoza kwa busara ya mikono yake.

Shirikisha
Soma Zaburi 78

Zaburi 78:1-72 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Enyi watu wangu, sikieni mafundisho yangu, sikilizeni maneno ya kinywa changu. Nitafungua kinywa changu kwa mafumbo, nitazungumza mambo yaliyofichika, mambo ya kale: yale ambayo tuliyasikia na kuyajua, yale ambayo baba zetu walituambia. Hatutayaficha kwa watoto wao; tutakiambia kizazi kijacho matendo yastahiliyo sifa ya BWANA, uweza wake, na maajabu aliyoyafanya. Aliagiza amri kwa Yakobo na akaweka sheria katika Israeli, ambazo aliwaamuru baba zetu wawafundishe watoto wao, ili kizazi kijacho kizijue, pamoja na watoto ambao watazaliwa, nao pia wapate kuwaeleza watoto wao. Ndipo wangeweka tumaini lao kwa Mungu, nao hawangesahau matendo yake, bali wangezishika amri zake. Hawangefanana na baba zao, waliokuwa kizazi cha ukaidi na uasi, ambao roho zao hazikuwa na uaminifu kwa Mungu, ambao roho zao hazikumwamini. Watu wa Efraimu, ingawa walijifunga pinde, walikimbia siku ya vita. Hawakulishika agano la Mungu, na walikataa kuishi kwa sheria yake. Walisahau aliyokuwa ameyatenda, maajabu aliyokuwa amewaonesha. Alitenda miujiza machoni mwa baba zao, huko Soani, katika nchi ya Misri. Aliigawanya bahari akawapitisha, alifanya maji yasimame imara kama ukuta. Aliwaongoza kwa wingu mchana, na kwa nuru ya moto usiku kucha. Alipasua miamba jangwani na akawapa maji tele kama bahari, alitoa vijito kutoka jabali lililochongoka, akayafanya maji yatiririke kama mito. Lakini waliendelea kutenda dhambi dhidi yake, wakiasi jangwani dhidi ya Aliye Juu Sana. Kwa makusudi walimjaribu Mungu, wakidai vyakula walivyovitamani. Walinena dhidi ya Mungu, wakisema, “Je, Mungu aweza kuandaa meza jangwani? Alipopiga mwamba, maji yalitoka kwa nguvu, vijito vikatiririka maji mengi. Lakini je, aweza kutupatia chakula pia? Je, anaweza kuwapatia watu wake nyama?” BWANA alipowasikia, alikasirika sana, moto wake ukawa dhidi ya Yakobo, na ghadhabu yake ikawaka dhidi ya Israeli, kwa kuwa hawakumwamini Mungu, wala kuutumainia ukombozi wake. Hata hivyo alitoa amri kwa anga zilizo juu na kufungua milango ya mbingu, akawanyeshea mana ili watu wale; aliwapa nafaka ya mbinguni. Watu walikula mkate wa malaika, akawatumia chakula chote ambacho wangeweza kula. Aliachia upepo wa mashariki kutoka mbingu na kuuongoza upepo wa kusini kwa uwezo wake. Aliwanyeshea nyama kama mavumbi, ndege warukao kama mchanga wa pwani. Aliwafanya washuke ndani ya kambi yao, kuzunguka mahema yao yote. Walikula na kusaza, kwa maana alikuwa amewapa kile walichotamani. Kabla hawajamaliza kula walichokitamani, hata kilipokuwa kingali bado vinywani mwao, hasira ya Mungu ikawaka juu yao, akawaua wale waliokuwa na nguvu zaidi miongoni mwao, akiwaangusha vijana wa Israeli. Licha ya haya yote, waliendelea kutenda dhambi, licha ya maajabu yake, hawakuamini. Kwa hiyo akamaliza siku zao katika ubatili na miaka yao katika vitisho. Kila mara Mungu alipowaua baadhi yao, waliosalia walimtafuta, walimgeukia tena kwa shauku. Walikumbuka kwamba Mungu alikuwa Mwamba wao, kwamba Mungu Aliye Juu Sana alikuwa Mkombozi wao. Lakini walimdanganya kwa vinywa vyao, wakisema uongo kwa ndimi zao, mioyo yao haikuwa thabiti kwake, wala hawakuwa waaminifu katika agano lake. Hata hivyo alikuwa na huruma, alisamehe maovu yao na hakuwaangamiza. Mara kwa mara alizuia hasira yake, wala hakuchochea ghadhabu yake yote. Alikumbuka kwamba wao walikuwa nyama tu, upepo upitao ambao haurudi. Mara ngapi walimwasi jangwani na kumhuzunisha nyikani! Walimjaribu Mungu mara kwa mara, wakamkasirisha yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli. Hawakukumbuka uwezo wake, siku aliyowakomboa kutoka kwa mtesi, siku aliyoonesha ishara zake za ajabu huko Misri, maajabu yake huko Soani. Aligeuza mito yao kuwa damu, hawakuweza kunywa maji kutoka vijito vyao. Aliwapelekea makundi ya inzi wakawala, na vyura wakawaharibu. Aliruhusu tunutu kuharibu mimea yao, mazao yao kwa nzige. Aliharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe na mikuyu yao kwa mvua iliyochangamana na theluji. Aliwaachia mifugo yao mvua ya mawe, akayapiga makundi ya wanyama wao kwa radi. Aliwafungulia hasira yake kali, ghadhabu yake, hasira na uadui, na kundi la malaika wa kuharibu. Aliitengenezea njia hasira yake, hakuwaepusha na kifo, bali aliwaachia tauni. Aliwapiga wazaliwa wote wa kwanza wa Misri, matunda ya kwanza ya ujana katika mahema ya Hamu. Lakini aliwatoa watu wake kama kundi, akawaongoza kama kondoo kupitia jangwani. Aliwaongoza salama, wala hawakuogopa, bali bahari iliwameza adui zao. Hivyo akawaleta hadi kwenye mpaka wa nchi yake takatifu, hadi nchi ya vilima ambayo mkono wake wa kuume ulikuwa umeitwaa. Aliyafukuza mataifa mbele yao, na kuwagawia nchi zao kama urithi, aliwakalisha makabila ya Israeli katika makao yao. Lakini wao walimjaribu Mungu, na kuasi dhidi ya Yeye Aliye Juu Sana, wala hawakuzishika sheria zake. Kama baba zao, hawakuwa thabiti wala waaminifu, wakawa wasioweza kutegemewa kama upinde wenye kasoro. Wakamkasirisha Mungu kwa mahali pao pa juu pa kuabudia, wakachochea wivu wake kwa sanamu zao. Mungu alipowasikia, alikasirika sana, akamkataa Israeli kabisa. Akaiacha maskani ya Shilo, hema alilokuwa ameliweka katikati ya wanadamu. Akalipeleka Sanduku la nguvu zake utumwani, utukufu wake mikononi mwa adui. Aliachia watu wake wauawe kwa upanga, akaukasirikia sana urithi wake. Moto uliwaangamiza vijana wao, na wanawali wao hawakuimbiwa nyimbo za arusi, makuhani wao waliuawa kwa upanga, wala wajane wao hawakuweza kulia. Ndipo Bwana alipoamka kama kuamka usingizini, kama shujaa anavyoamka kutoka bumbuazi la mvinyo. Aliwapiga na kuwashinda adui zake, akawatia katika aibu ya milele. Ndipo alipoyakataa mahema ya Yusufu, hakulichagua kabila la Efraimu, lakini alilichagua kabila la Yuda, Mlima Sayuni, ambao aliupenda. Alijenga patakatifu pake kama vilele, kama dunia ambayo aliimarisha milele. Akamchagua Daudi mtumishi wake na kumtoa kwenye mazizi ya kondoo. Kutoka kuchunga kondoo alimleta kuwa mchungaji wa watu wake Yakobo, wa Israeli urithi wake. Naye Daudi aliwachunga kwa uadilifu wa moyo, kwa mikono ya ustadi aliwaongoza.

Shirikisha
Soma Zaburi 78