Zaburi 73:3-11
Zaburi 73:3-11 Biblia Habari Njema (BHN)
maana niliwaonea wivu wenye kiburi, nilipoona wakosefu wakifanikiwa. Maana hao hawapatwi na mateso; miili yao ina afya na wana nguvu. Taabu za binadamu haziwapati hao; hawapati mateso kama watu wengine. Kiburi kimekuwa mkufu wao shingoni, uhasama ni kama nguo yao. Macho yao hufura kwa uovu; mioyo yao hububujika mipango mibaya. Huwadhihaki wengine na kusema mabaya; hujivuna na kupanga kufanya uhasama. Kwa vinywa vyao hutukana mbingu; kwa ndimi zao hujitapa duniani. Hata watu wa Mungu wanawafuata, hawaoni kwao chochote kibaya na kusadiki kila wanachosema. Wanasema: “Mungu hawezi kujua! Mungu Mkuu hataweza kugundua!”
Zaburi 73:3-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Maana niliwaonea wivu wenye kujivuna, Nilipoiona hali ya amani ya wasio haki. Maana hawana maumivu katika kufa kwao, Na miili yao ina nguvu. Hawana taabu kama watu wengine, Wala hawapati mapigo kama wanadamu wenzao. Hivyo kiburi kimekuwa mkufu shingoni mwao, Udhalimu huwavika kama nguo. Macho yao hutokeza kwa kunenepa, Wameipita kadiri ya mawazo ya mioyo yao. Hudhihaki, husimulia mabaya, Husimulia udhalimu kana kwamba wako juu. Wameweka kinywa chao mbinguni, Na ulimi wao hutangatanga duniani. Kwa hiyo watu wake hugeuka huko, Na maji yaliyojaa humezwa nao. Nao husema, Mungu ajuaje? Yako maarifa kwake aliye juu?
Zaburi 73:3-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Maana naliwaonea wivu wenye kujivuna, Nilipoiona hali ya amani ya wasio haki. Maana hawana maumivu katika kufa kwao, Na mwili wao una nguvu. Katika taabu ya watu hawamo, Wala hawapati mapigo pamoja na wanadamu. Hivyo kiburi kimekuwa mkufu shingoni mwao, Jeuri huwavika kama nguo. Macho yao hutokeza kwa kunenepa, Wameipita kadiri ya mawazo ya mioyo yao. Hudhihaki, husimulia mabaya, Husimulia udhalimu kana kwamba wako juu. Wameweka kinywa chao mbinguni, Na ulimi wao hutanga-tanga duniani. Kwa hiyo watu wake hugeuka huko, Na maji yaliyojaa humezwa nao. Nao husema, Mungu ajuaje? Yako maarifa kwake aliye juu?
Zaburi 73:3-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa maana niliwaonea wivu wenye kujivuna nilipoona kufanikiwa kwa waovu. Wao hawana taabu; miili yao ina afya na nguvu. Hawapati shida zinazowataabisha watu wengine, wala hawapati mapigo kama wanadamu wengine. Kwa hiyo kiburi ni mkufu wao, wamejivika jeuri. Uovu hutoka katika mioyo yao iliyokufa ganzi, majivuno maovu kutoka mioyoni mwao hayana kikomo. Hudhihaki na kusema kwa ukorofi, katika majivuno yao wanatishia kutesa. Vinywa vyao huweka madai hata kwa mbingu, nazo ndimi zao humiliki duniani. Kwa hiyo watu wao huwageukia na kunywa maji tele. Wanasema, “Mungu awezaje kujua? Je, Yeye Aliye Juu Sana anayo maarifa?”