Zaburi 41:1-13
Zaburi 41:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Heri mtu anayewajali maskini; Mwenyezi-Mungu atamwokoa wakati wa shida. Mwenyezi-Mungu atamlinda na kumweka hai, naye atafanikiwa katika nchi; Mungu hatamwacha makuchani mwa maadui zake. Mwenyezi-Mungu atamsaidia awapo mgonjwa, atamponya maradhi yake yote. Nami nilisema: “Unifadhili, ee Mwenyezi-Mungu, unihurumie maana nimekukosea wewe.” Madui zangu husema vibaya juu yangu: “Atakufa lini na jina lake litoweke!” Wanitembeleapo husema maneno matupu; wanakusanya mabaya juu yangu, na wafikapo nje huwatangazia wengine. Wote wanichukiao hunongonezana juu yangu; wananiwazia mabaya ya kunidhuru. Husema: “Maradhi haya yatamuua; hatatoka tena kitandani mwake!” Hata rafiki yangu wa moyoni niliyemwamini, rafiki ambaye alishiriki chakula changu, amegeuka kunishambulia! Ee Mwenyezi-Mungu, unionee huruma! Unipe nafuu, nami nitawalipiza. Hivyo nitajua kwamba unapendezwa nami, maadui zangu wasipopata fahari juu yangu. Wewe umenitegemeza kwani natenda mema; waniweka mbele yako milele. Asifiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, tangu milele na hata milele! Amina! Amina!
Zaburi 41:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Heri amkumbukaye mnyonge; BWANA atamwokoa siku ya taabu. BWANA atamlinda na kumhifadhi hai, Naye atafanikiwa katika nchi; Wala usimtie katika hali wamtakiayo adui zake. BWANA atamtegemeza alipo mgonjwa kitandani. Katika ugonjwa wake unamponya maradhi yake yote. Nami nilisema, BWANA, unifadhili, Uniponye roho yangu maana nimekutenda dhambi. Adui zangu wananitaja kwa maneno mabaya, Atakufa lini, jina lake lipotee? Na mmoja wao akija kunitazama asema uongo, Moyo wake hujikusanyia maovu, Naye atokapo nje huyanena. Wote wanaonichukia wananong'onezana juu yangu, Wananiwazia yaliyo mabaya zaidi. Wanafikiri pigo liualo limemshika, Akalala asiweze kusimama tena. Hata rafiki yangu mwandani niliyemtumaini, Aliyekula pamoja nami, Ameniinulia kisigino chake. Lakini Wewe, BWANA, unifadhili, Uniinue nipate kuwalipa. Kwa neno hili nimejua ya kuwa wapendezwa nami, Kwa kuwa adui yangu hajivunii kunishinda. Nami katika ukamilifu wangu umenitegemeza, Umeniweka mbele za uso wako milele. Na atukuzwe BWANA, Mungu wa Israeli, Tangu milele hata milele. Amina na Amina.
Zaburi 41:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Heri amkumbukaye mnyonge; BWANA atamwokoa siku ya taabu. BWANA atamlinda na kumhifadhi hai, Naye atafanikiwa katika nchi; Wala usimtie katika hali wamtakiayo adui zake. BWANA atamtegemeza alipo mgonjwa kitandani. Katika ugonjwa wake umemtandikia. Nami nalisema, BWANA, unifadhili, Uniponye roho yangu maana nimekutenda dhambi. Adui zangu wananitaja kwa maneno mabaya, Atakufa lini, jina lake likapotea? Na mmoja wao akija kunitazama asema uongo, Moyo wake hujikusanyia maovu, Naye atokapo nje huyanena. Wote wanaonichukia wananinong’ona, Wananiwazia mabaya. Neno la kisirani limemgandama, Na iwapo amelala hatasimama tena. Msiri wangu tena niliyemtumaini, Aliyekula chakula changu, Ameniinulia kisigino chake. Lakini Wewe, BWANA, unifadhili, Uniinue nipate kuwalipa. Kwa neno hili nimejua ya kuwa wapendezwa nami, Kwa kuwa adui yangu hasimangi kwa kunishinda. Nami katika ukamilifu wangu umenitegemeza, Umeniweka mbele za uso wako milele. Na atukuzwe BWANA, Mungu wa Israeli, Tangu milele hata milele. Amina na Amina.
Zaburi 41:1-13 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Heri mtu yule anayemjali mnyonge, BWANA atamwokoa wakati wa shida. BWANA atamlinda na kuyahifadhi maisha yake, atambariki katika nchi na hatamwacha katika tamaa ya adui zake. BWANA atamtegemeza akiwa mgonjwa kitandani, na atamwinua kutoka kitandani mwake. Nilisema, “Ee BWANA nihurumie, niponye, maana nimekutenda dhambi wewe.” Adui zangu wanasema kwa hila, “Lini atakufa, na jina lake litokomee kabisa.” Kila anapokuja mtu kunitazama, huzungumza uongo, huku moyo wake ukikusanya masingizio; kisha huondoka na kuyasambaza. Adui zangu wote hunongʼonezana dhidi yangu, hao huniwazia mabaya sana, wakisema, “Ugonjwa mbaya sana umempata, kamwe hatainuka tena kitandani mwake.” Hata rafiki yangu wa karibu niliyemwamini, yule aliyekula chakula changu ameniinulia kisigino chake. Lakini wewe, Ee BWANA, nihurumie, ukaniinue tena, ili niweze kuwalipiza kisasi. Najua kwamba wapendezwa nami, kwa kuwa adui yangu hanishindi. Katika uadilifu wangu unanitegemeza na kuniweka kwenye uwepo wako milele. Mtukuzeni BWANA, Mungu wa Israeli, tangu milele na hata milele. Amen na Amen.