Zaburi 29:1-11
Zaburi 29:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Mpeni Mwenyezi-Mungu heshima enyi viumbe vya mbinguni, semeni Mwenyezi-Mungu ni mtukufu na mwenye nguvu. Semeni jina la Mwenyezi-Mungu ni tukufu. Mwabuduni katika mahali pake patakatifu. Sauti ya Mwenyezi-Mungu yasikika juu ya maji; Mungu mtukufu angurumisha radi, sauti ya Mwenyezi-Mungu yasikika juu ya bahari! Sauti ya Mwenyezi-Mungu ina nguvu, sauti ya Mwenyezi-Mungu imejaa fahari. Sauti ya Mwenyezi-Mungu huvunja mierezi; Mwenyezi-Mungu avunja mierezi ya Lebanoni. Huirusha milima ya Lebanoni kama ndama, milima ya Sirioni kama mwananyati. Sauti ya Mwenyezi-Mungu hutoa miali ya moto. Sauti ya Mwenyezi-Mungu hutetemesha jangwa, Mwenyezi-Mungu hutetemesha jangwa la Kadeshi. Sauti ya Mwenyezi-Mungu huitikisa mivule, hukwanyua majani ya miti msituni, na hekaluni mwake wote wasema: “Utukufu kwa Mungu!” Mwenyezi-Mungu ameketi juu ya gharika; Mwenyezi-Mungu ni mfalme atawalaye milele. Mwenyezi-Mungu na awape watu wake nguvu! Mwenyezi-Mungu na awabariki watu wake kwa amani!
Zaburi 29:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mpeni BWANA, enyi wana wa Mungu, Mpeni BWANA utukufu na nguvu; Mpeni BWANA utukufu wa jina lake; Mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu. Sauti ya BWANA inasikika juu ya maji; Mungu wa utukufu apiga radi; BWANA yu juu ya maji mengi. Sauti ya BWANA ina nguvu; Sauti ya BWANA ina utukufu; Sauti ya BWANA yaivunja mierezi; Naam, BWANA aivunjavunja mierezi ya Lebanoni; Airusharusha Lebanoni kama ndama wa ng'ombe; Lebanoni na Sirioni kama mwananyati. Sauti ya BWANA inatoa miale paa ya moto; Sauti ya BWANA yalitetemesha jangwa; BWANA alitetemesha jangwa la Kadeshi. Sauti ya BWANA yawazalisha ayala, Na kuiacha misitu wazi; Na ndani ya hekalu lake Wanasema, Utukufu! BWANA aketi juu ya Gharika; Naam, BWANA ameshika hatamu ya ufalme milele. BWANA na awape watu wake nguvu; BWANA na awabariki watu wake kwa amani.
Zaburi 29:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mpeni BWANA, enyi wana wa Mungu, Mpeni BWANA utukufu na nguvu; Mpeni BWANA utukufu wa jina lake; Mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu. Sauti ya BWANA i juu ya maji; Mungu wa utukufu alipiga radi; BWANA yu juu ya maji mengi. Sauti ya BWANA ina nguvu; Sauti ya BWANA ina adhama; Sauti ya BWANA yaivunja mierezi; Naam, BWANA aivunja-vunja mierezi ya Lebanoni; Airusha-rusha kama ndama wa ng’ombe; Lebanoni na Sirioni kama mwana-nyati. Sauti ya BWANA yaipasua miali ya moto; Sauti ya BWANA yalitetemesha jangwa; BWANA alitetemesha jangwa la Kadeshi. Sauti ya BWANA yawazalisha ayala, Na kuifichua misitu; Na ndani ya hekalu lake Wanasema wote, Utukufu. BWANA aliketi juu ya Gharika; Naam, BWANA ameketi hali ya mfalme milele. BWANA atawapa watu wake nguvu; BWANA atawabariki watu wake kwa amani.
Zaburi 29:1-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mpeni BWANA, enyi mashujaa, mpeni BWANA utukufu na nguvu. Mpeni BWANA utukufu unaostahili jina lake; mwabuduni BWANA katika uzuri wa utakatifu wake. Sauti ya BWANA iko juu ya maji; Mungu wa utukufu hupiga radi, BWANA hupiga radi juu ya maji makuu. Sauti ya BWANA ina nguvu; sauti ya BWANA ni tukufu. Sauti ya BWANA huvunja mierezi; BWANA huvunja vipande vipande mierezi ya Lebanoni. Hufanya Lebanoni irukaruke kama ndama, Sirioni urukaruke kama mwana nyati. Sauti ya BWANA hupiga kwa miali ya radi. Sauti ya BWANA hutikisa jangwa; BWANA hutikisa Jangwa la Kadeshi. Sauti ya BWANA huzalisha ayala, na huuacha msitu wazi. Hekaluni mwake wote wasema, “Utukufu!” BWANA huketi akiwa ametawazwa juu ya gharika; BWANA ametawazwa kuwa Mfalme milele. BWANA huwapa watu wake nguvu; BWANA huwabariki watu wake kwa kuwapa amani.