Zaburi 19:1-9
Zaburi 19:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Mbingu zatangaza utukufu wa Mungu; anga ladhihirisha kazi ya mikono yake. Mchana waupasha habari mchana ufuatao, usiku waufahamisha usiku ufuatao. Hamna msemo au maneno yanayotumika; wala hakuna sauti inayosikika; hata hivyo, sauti yao yaenea duniani kote, na maneno yao yafika kingo za ulimwengu. Mungu ameliwekea jua makao yake angani; nalo hutoka kama bwana arusi chumbani mwake, lafurahi kama shujaa aliye tayari kushindana. Lachomoza toka upande mmoja, na kuzunguka hadi upande mwingine; hakuna kiwezacho kuliepa joto lake. Sheria ya Mwenyezi-Mungu ni kamilifu, humpa mtu uhai mpya; masharti ya Mwenyezi-Mungu ni thabiti, huwapa hekima wasio na makuu. Kanuni za Mwenyezi-Mungu ni sawa, huufurahisha moyo; amri ya Mwenyezi-Mungu ni safi, humwelimisha mtu. Kumcha Mwenyezi-Mungu ni jambo jema, na la kudumu milele; maagizo ya Mwenyezi-Mungu ni sawa, yote ni ya haki kabisa.
Zaburi 19:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu, Na anga laitangaza kazi ya mikono yake. Mchana husemezana na mchana, Usiku hutolea usiku maarifa. Hakuna usemi wala maneno, Sauti yao haisikilikani. Sauti yao imeenea duniani kote, Na maneno yao hadi miisho ya ulimwengu. Katika hizo ameliwekea jua hema, Nalo hutokeza kama bwana arusi akitoka chumbani mwake, Lafurahi kama mtu aliye hodari Kwenda mbio katika njia yake. Kuchomoza kwake ni katika mwisho wa mbingu, Na kuzunguka kwake ni hadi miisho ya mbingu, Wala hakuna kitu Kisichofikiwa na joto lake. Sheria ya BWANA ni kamilifu, Huiburudisha nafsi. Ushuhuda wa BWANA ni amini, Humtia hekima mtu asiye nayo. Maagizo ya BWANA ni ya adili, Huufurahisha moyo. Amri ya BWANA ni safi, Huyatia macho nuru. Kicho cha BWANA ni kitakatifu, Kinadumu milele. Hukumu za BWANA ni kweli, Zina haki kabisa.
Zaburi 19:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu, Na anga laitangaza kazi ya mikono yake. Mchana husemezana na mchana, Usiku hutolea usiku maarifa. Hakuna lugha wala maneno, Sauti yao haisikilikani. Sauti yao imeenea duniani mwote, Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu. Katika hizo ameliwekea jua hema, Kama bwana arusi akitoka chumbani mwake, Lafurahi kama mtu aliye hodari Kwenda mbio katika njia yake. Kutoka kwake lautoka mwisho wa mbingu, Na kuzunguka kwake hata miisho yake, Wala kwa hari yake Hakuna kitu kilichositirika. Sheria ya BWANA ni kamilifu, Huiburudisha nafsi. Ushuhuda wa BWANA ni amini, Humtia mjinga hekima. Maagizo ya BWANA ni ya adili, Huufurahisha moyo. Amri ya BWANA ni safi, Huyatia macho nuru. Kicho cha BWANA ni kitakatifu, Kinadumu milele. Hukumu za BWANA ni kweli, Zina haki kabisa.
Zaburi 19:1-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mbingu zinatangaza utukufu wa Mungu, anga zahubiri kazi ya mikono yake. Siku baada ya siku zinatoa habari, usiku baada ya usiku zinatangaza maarifa. Hakuna msemo wala lugha, ambapo sauti zao hazisikiki. Sauti yao imeenea duniani pote, nayo maneno yao yameenea hadi miisho ya ulimwengu. Katika mbingu amepiga hema kwa ajili ya jua, linafanana na bwana arusi akitoka chumbani mwake, kama shujaa anavyofurahia kukamilisha kushindana kwake. Huchomoza upande mmoja wa mbingu, na kufanya mzunguko wake hadi upande mwingine. Hakuna kilichojificha joto lake. Sheria ya BWANA ni kamilifu, ikihuisha nafsi. Shuhuda za BWANA ni za kuaminika, zikimpa mjinga hekima. Maagizo ya BWANA ni kamili, nayo hufurahisha moyo. Amri za BWANA huangaza, zatia nuru machoni. Kumcha BWANA ni utakatifu, nako kwadumu milele. Amri za BWANA ni za hakika, nazo zina haki.