Zaburi 148:1-14
Zaburi 148:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Msifuni Mwenyezi-Mungu! Msifuni Mwenyezi-Mungu kutoka mbinguni, msifuni kutoka huko juu mbinguni. Msifuni, enyi malaika wake wote, msifuni, enyi majeshi yake yote. Msifuni, enyi jua na mwezi, msifuni, enyi nyota zote zingaazo. Msifuni, enyi mbingu za juu, na maji yaliyo juu ya mbingu. Vyote vilisifu jina la Mwenyezi-Mungu, maana yeye aliamuru, na vyote vikawa. Yeye aliviweka mahali pao daima, kwa amri ambayo haiwezi kubatilishwa. Msifuni Mwenyezi-Mungu kutoka duniani; enyi majoka ya baharini na vilindini, msifuni. Msifuni enyi moto, mvua ya mawe na theluji, upepo wa tufani unaotimiza amri yake! Msifuni enyi milima na vilima, miti ya matunda na misitu! Msifuni enyi wanyama wa porini na wafugwao, viumbe vitambaavyo na ndege wote! Msifuni enyi wafalme na mataifa yote; viongozi na watawala wote duniani! Msifuni enyi wavulana na wasichana; wazee wote na watoto pia! Nyote lisifuni jina la Mwenyezi-Mungu, maana jina lake peke yake latukuka; utukufu wake wapita dunia na mbingu. Amewapa watu wake nguvu; heshima kwa watu wote waaminifu, watu wa Israeli wapenzi wake. Msifuni Mwenyezi-Mungu!
Zaburi 148:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Haleluya. Msifuni BWANA kutoka mbinguni; Msifuni katika mahali palipo juu. Msifuni, enyi malaika wake wote; Msifuni, majeshi yake yote. Msifuni, jua na mwezi; Msifuni, nyota zote zenye mwanga. Msifuni, enyi mbingu za mbingu, Nanyi maji mlioko juu ya mbingu. Na vilisifu jina la BWANA, Kwa maana aliamuru, vikaumbwa. Amevithibitisha hata milele na milele, Ametoa amri wala haitapita. Msifuni BWANA kutoka nchi, Enyi nyangumi na vilindi vyote. Moto na mvua ya mawe, theluji na mvuke, Upepo wa dhoruba utimizao neno lake. Milima na vilima vyote, Miti yenye matunda na mierezi yote. Hayawani, na wanyama wafugwao, Vitambaavyo, na ndege wenye mbawa. Wafalme wa dunia, na watu wote, Wakuu, na watawala wote wa dunia. Vijana wa kiume, na wanawali, Wazee, na watoto; Na walisifu jina la BWANA, Maana jina lake peke yake limetukuka; Adhama yake i juu ya nchi na mbingu. Naye amewainulia watu wake pembe, Sifa za watauwa wake wote; Wana wa Israeli, watu walio karibu naye. Haleluya.
Zaburi 148:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Haleluya. Msifuni BWANA kutoka mbinguni; Msifuni katika mahali palipo juu. Msifuni, enyi malaika wake wote; Msifuni, majeshi yake yote. Msifuni, jua na mwezi; Msifuni, nyota zote zenye mwanga. Msifuni, enyi mbingu za mbingu, Nanyi maji mlioko juu ya mbingu. Na vilisifu jina la BWANA, Kwa maana aliamuru, vikaumbwa. Amevithibitisha hata milele na milele, Ametoa amri wala haitapita. Msifuni BWANA kutoka nchi, Enyi nyangumi na vilindi vyote. Moto na mvua ya mawe, theluji na mvuke, Upepo wa dhoruba ulitendao neno lake. Milima na vilima vyote, Miti yenye matunda na mierezi yote. Hayawani, na wanyama wafugwao, Vitambaavyo, na ndege wenye mbawa. Wafalme wa dunia, na watu wote, Wakuu, na makadhi wote wa dunia. Vijana waume, na wanawali, Wazee, na watoto; Na walisifu jina la BWANA, Maana jina lake peke yake limetukuka; Adhama yake i juu ya nchi na mbingu. Naye amewainulia watu wake pembe, Sifa za watauwa wake wote; Wana wa Israeli, watu walio karibu naye. Haleluya.
Zaburi 148:1-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Msifuni BWANA. Msifuni BWANA kutoka mbinguni, msifuni juu vileleni. Msifuni, enyi malaika wake wote, msifuni yeye, enyi jeshi lake lote la mbinguni. Msifuni yeye, enyi jua na mwezi, msifuni yeye, enyi nyota zote zingʼaazo. Msifuni yeye, enyi mbingu zilizo juu sana, na ninyi maji juu ya anga. Vilisifu jina la BWANA kwa maana aliamuru navyo vikaumbwa. Aliviweka mahali pake milele na milele, alitoa amri ambayo haibadiliki milele. Mtukuzeni BWANA kutoka duniani, ninyi viumbe vikubwa vya baharini na vilindi vyote vya bahari, umeme wa radi na mvua ya mawe, theluji na mawingu, pepo za dhoruba zinazofanya amri zake, ninyi milima na vilima vyote, miti ya matunda na mierezi yote, wanyama wa mwituni na mifugo yote, viumbe vidogo na ndege warukao, wafalme wa dunia na mataifa yote, ninyi wakuu na watawala wote wa dunia, wanaume vijana na wanawali, wazee na watoto. Wote na walisifu jina la BWANA, kwa maana jina lake pekee limetukuka, utukufu wake uko juu ya nchi na mbingu. Amewainulia watu wake pembe, sifa ya watakatifu wake wote, ya Israeli, watu walio karibu na moyo wake.