Zaburi 119:73-80
Zaburi 119:73-80 Biblia Habari Njema (BHN)
Mikono yako iliniumba na kuniunda; unijalie akili nijifunze amri zako. Wakuchao wataniona na kufurahi, maana tumaini langu liko katika neno lako. Najua hukumu zako ni adili, ee Mwenyezi-Mungu, na kwamba umeniadhibu kwani wewe ni mwaminifu. Fadhili zako na zinipe faraja, kama ulivyoniahidi mimi mtumishi wako. Unionee huruma nipate kuishi, maana sheria yako ni furaha yangu. Wenye kiburi waaibike kwa maana wamenifanyia hila, lakini mimi nitazitafakari kanuni zako. Wote wakuchao na waje kwangu, wapate kuyajua maamuzi yako. Moyo wangu na uzingatie masharti yako, nisije nikaaibishwa.
Zaburi 119:73-80 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mikono yako iliniumba na kunidhibiti, Unifahamishe nikajifunze amri zako. Wakuchao na wanione na kufurahi, Kwa sababu nimelitumainia neno lako. Najua ya kuwa hukumu zako ni za haki, Ee BWANA, na kwa uaminifu umenitesa. Nakuomba, fadhili zako ziwe faraja kwangu, Kulingana na ahadi yako kwa mtumishi wako. Rehema zako zinijie nipate kuishi, Maana sheria yako ni furaha yangu. Wenye kiburi waaibike, maana wamenidhulumu kwa uongo, Mimi nitayatafakari mausia yako. Wakuchao na wanirudie, Nao watazijua shuhuda zako. Moyo wangu na uwe mkamilifu katika amri zako, Nisije mimi nikaaibika.
Zaburi 119:73-80 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mikono yako ilinifanya ikanitengeneza, Unifahamishe nikajifunze maagizo yako. Wakuchao na wanione na kufurahi, Kwa sababu nimelingojea neno lako. Najua ya kuwa hukumu zako ni za haki, Ee BWANA, na kwa uaminifu umenitesa. Nakuomba, fadhili zako ziwe faraja kwangu, Sawasawa na ahadi yako kwa mtumishi wako. Rehema zako zinijie nipate kuishi, Maana sheria yako ni furaha yangu. Wenye kiburi waaibike, maana wamenidhulumu kwa uongo, Mimi nitayatafakari mausia yako. Wakuchao na wanirudie, Nao watazijua shuhuda zako. Moyo wangu na uwe mkamilifu katika amri zako, Nisije mimi nikaaibika.
Zaburi 119:73-80 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mikono yako ilinifanya na kuniumba, nipe ufahamu niweze kujifunza amri zako. Wakuchao wafurahie wanaponiona, kwa kuwa nimeweka tumaini langu katika neno lako. Ee BWANA, ninajua kwamba sheria zako ni za haki, katika uaminifu wako umeniadhibu. Upendo wako usiokoma uwe faraja yangu, sawasawa na ahadi yako kwa mtumishi wako. Huruma yako na inijie ili nipate kuishi, kwa kuwa naifurahia sheria yako. Wenye majivuno na waaibishwe kwa kunikosea mimi bila sababu, lakini mimi nitatafakari juu ya mausia yako. Wale wakuchao na wanigeukie mimi, hao ambao wanazielewa sheria zako. Moyo wangu usiwe na lawama katika kutii maagizo yako, ili nisiaibishwe.