Zaburi 119:57-64
Zaburi 119:57-64 Biblia Habari Njema (BHN)
Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, ndiwe riziki yangu kuu; naahidi kushika maneno yako. Naomba radhi yako kwa moyo wangu wote; unionee huruma kama ulivyoahidi! Nimeufikiria mwenendo wangu, na nimerudi nifuate maamuzi yako. Bila kukawia nafanya haraka kuzishika amri zako. Waovu wametega mitego waninase, lakini mimi sisahau sheria yako. Usiku wa manane naamka kukusifu, kwa sababu ya maagizo yako maadilifu. Mimi ni rafiki ya wote wakuchao, rafiki yao wanaozitii kanuni zako. Dunia imejaa fadhili zako, ee Mwenyezi-Mungu, unifundishe masharti yako.
Zaburi 119:57-64 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA ndiye aliye fungu langu, Ninaahidi kuyatii maneno yake. Nimekuomba radhi kwa moyo wangu wote, Unifadhili kulingana na ahadi yako. Ninapozitafakari njia zako, Naielekeza miguu yangu kwa shuhuda zako. Nilifanya haraka wala sikukawia, Kuyatii maagizo yako. Japo kamba za wasio haki zimenifunga, Siisahau sheria yako. Usiku wa manane nitaamka nikushukuru, Kwa sababu ya hukumu zako za haki. Mimi ni mwenzi wa watu wote wakuchao, Na wale wayatiio mausia yako. BWANA, dunia imejaa fadhili zako, Unifundishe amri zako.
Zaburi 119:57-64 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA ndiye aliye fungu langu, Nimesema kwamba nitayatii maneno yake. Nimekuomba radhi kwa moyo wangu wote, Unifadhili sawasawa na ahadi yako. Nalizitafakari njia zangu, Na miguu yangu nalizielekezea shuhuda zako. Nalifanya haraka wala sikukawia, Kuyatii maagizo yako. Kamba za wasio haki zimenifunga, Sikuisahau sheria yako. Katikati ya usiku nitaamka nikushukuru, Kwa sababu ya hukumu zako za haki. Mimi ni mwenzao watu wote wakuchao, Na wale wayatiio mausia yako. BWANA, dunia imejaa fadhili zako, Unifundishe amri zako.
Zaburi 119:57-64 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ee BWANA, wewe ni fungu langu, nimeahidi kuyatii maneno yako. Nimetafuta uso wako kwa moyo wangu wote, nihurumie sawasawa na ahadi yako. Nimezifikiri njia zangu na nimeelekeza hatua zangu katika mausia yako. Nitafanya haraka bila kuchelewa kuzitii amri zako. Hata waovu wanifunge kwa kamba, sitasahau sheria yako. Usiku wa manane ninaamka kukushukuru kwa sababu ya sheria zako za haki. Mimi ni rafiki kwa wale wote wakuchao, kwa wote wanaofuata mausia yako. Ee BWANA, dunia imejaa upendo wako, nifundishe maagizo yako.