Zaburi 115:1-11
Zaburi 115:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Sio sisi, ee Mwenyezi-Mungu, sio sisi; bali wewe peke yako utukuzwe, kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako. Kwa nini mataifa yaseme: “Mungu wenu yuko wapi?” Mungu wetu yuko mbinguni; yeye hufanya yote anayotaka. Miungu yao ni ya fedha na dhahabu; imetengenezwa kwa mikono ya wanadamu. Ina vinywa, lakini haisemi. Ina macho, lakini haioni. Ina masikio, lakini haisikii. Ina pua, lakini hainusi. Ina mikono, lakini haipapasi. Ina miguu, lakini haitembei. Haiwezi kamwe kutoa sauti. Wote wanaoitengeneza wanafanana nayo, kadhalika na wote wanaoitumainia. Enyi Waisraeli, mtumainieni Mwenyezi-Mungu; yeye ndiye msaada wenu na ngao yenu. Enyi wazawa wa Aroni, mtumainieni Mwenyezi-Mungu; yeye ndiye msaada wenu na ngao yenu. Enyi mnaomcha Mwenyezi-Mungu, mtumainini, yeye ndiye msaada wenu na ngao yenu.
Zaburi 115:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ee BWANA, kutukuza usitutukuze sisi, Bali ulitukuze jina lako, Kwa ajili ya fadhili zako, Kwa ajili ya uaminifu wako. Kwa nini mataifa kusema, Yuko wapi Mungu wao? Lakini Mungu wetu yuko mbinguni, Alitakalo lote amelitenda. Sanamu zao ni fedha na dhahabu, Kazi ya mikono ya wanadamu. Zina vinywa lakini hazisemi, Zina macho lakini hazioni, Zina masikio lakini hazisikii, Zina pua lakini hazinusi harufu, Mikono lakini hazishiki, miguu lakini haziendi, Wala hazitoi sauti kwa koo zake. Wazitengenezao watafanana nazo, Sawa na wote wanaozitumainia. Enyi Israeli, mtumainini BWANA; Yeye ni msaada wao na ngao yao. Enyi mlango wa Haruni, mtumainini BWANA; Yeye ni msaada wao na ngao yao. Enyi mmchao BWANA, mtumainini BWANA; Yeye ni msaada wao na ngao yao.
Zaburi 115:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ee BWANA, kutukuza usitutukuze sisi, Bali ulitukuze jina lako, Kwa ajili ya fadhili zako, Kwa ajili ya uaminifu wako. Kwa nini mataifa kusema, Yuko wapi Mungu wao? Lakini Mungu wetu yuko mbinguni, Alitakalo lote amelitenda. Sanamu zao ni fedha na dhahabu, Kazi ya mikono ya wanadamu. Zina vinywa lakini hazisemi, Zina macho lakini hazioni, Zina masikio lakini hazisikii, Zina pua lakini hazisikii harufu, Mikono lakini hazishiki, miguu lakini haziendi, Wala hazitoi sauti kwa koo zake. Wazifanyao watafanana nazo, Kila mmoja anayezitumainia. Enyi Israeli, mtumainini BWANA; Yeye ni msaada wao na ngao yao. Enyi mlango wa Haruni, mtumainini BWANA; Yeye ni msaada wao na ngao yao. Enyi mmchao BWANA, mtumainini BWANA; Yeye ni msaada wao na ngao yao.
Zaburi 115:1-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Sio kwetu sisi, Ee BWANA, sio kwetu sisi, bali utukufu ni kwa jina lako, kwa sababu ya upendo na uaminifu wako. Kwa nini mataifa waseme, “Yuko wapi Mungu wao?” Mungu wetu yuko mbinguni, naye hufanya lolote limpendezalo. Lakini sanamu zao ni za fedha na dhahabu, zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu. Zina vinywa, lakini haziwezi kusema, zina macho, lakini haziwezi kuona; zina masikio, lakini haziwezi kusikia, zina pua, lakini haziwezi kunusa; zina mikono, lakini haziwezi kupapasa, zina miguu, lakini haziwezi kutembea; wala koo zao haziwezi kutoa sauti. Wale wanaozitengeneza watafanana nazo, vivyo hivyo wale wote wanaozitumainia. Ee nyumba ya Israeli, mtumainini BWANA, yeye ni msaada na ngao yao. Ee nyumba ya Haruni, mtumainini BWANA, yeye ni msaada na ngao yao. Ninyi mnaomcha, mtumainini BWANA, yeye ni msaada na ngao yao.