Zaburi 108:1-13
Zaburi 108:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Niko thabiti moyoni, ee Mungu, naam, niko thabiti moyoni; nitaimba na kukushangilia! Amka, ee nafsi yangu! Amkeni enyi kinubi na zeze! Nitayaamsha mapambazuko! Ee Mwenyezi-Mungu, nitakushukuru kati ya mataifa; nitakuimbia sifa kati ya mataifa. Fadhili zako ni kubwa kuliko mbingu; uaminifu wako waenea hata mawinguni. Utukuzwe, ee Mungu juu ya mbingu! Utukufu wako uenee duniani kote! Watu hao uwapendao na wasalimishwe; utusaidie kwa mkono wako na kutusikiliza. Mungu amesema kutoka patakatifu pake: “Sasa nitaigawa Shekemu kwa shangwe, bonde la Sukothi nitalipima sehemusehemu. Gileadi ni yangu, na Manase ni yangu; Efraimu ni kofia yangu ya chuma, na Yuda ni fimbo yangu ya enzi. Moabu ni kama bakuli langu la kunawia; kiatu changu nitaitupia Edomu kuimiliki. Nitapiga kelele ya ushindi juu ya Filistia!” Ni nani, atakayenipeleka kwenye mji wa ngome? Ni nani atakayeniongoza mpaka Edomu? Je, umetuacha kabisa, ee Mungu? Wewe huendi tena na majeshi yetu! Utupatie msaada dhidi ya maadui zetu, maana msaada wa binadamu haufai kitu. Mungu akiwa upande wetu tutashinda, yeye atawaponda maadui zetu.
Zaburi 108:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ee Mungu, moyo wangu u thabiti, Nitaimba, nitaimba zaburi, Naam, kwa utukufu wangu. Amka, kinanda na kinubi, Nitaamka alfajiri. Ee BWANA, nitakushukuru kati ya watu, Nitakuimbia sifa kati ya mataifa. Maana fadhili zako ni kubwa kuliko mbingu, Na uaminifu wako unafika hata mawinguni. Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu, Na juu ya nchi yote uwe utukufu wako. Ili watu uwapendao waokolewe, 2 Unipe ushindi kwa mkono wako wa kulia, na uniitikie. Mungu amenena kwa utakatifu wake, Nami nitashangilia. Nitaigawanya Shekemu, Nitalipima bonde la Sukothi. Gileadi ni yangu, na Manase ni yangu, Na Efraimu ni nguvu ya kichwa changu. Yuda ni fimbo yangu ya kifalme, Moabu ni bakuli langu la kunawia. Nitamtupia Edomu kiatu changu, Na kumpigia Filisti kelele za vita. Ni nani atakayenipeleka hadi mji wenye boma? Ni nani atakayeniongoza hadi Edomu? Ee Mungu, si Wewe uliyetutupa? Wala, Ee Mungu, huendi na majeshi yetu? Utuletee msaada juu ya mtesi, Maana wokovu wa binadamu haufai. Kwa msaada wa Mungu tutatenda makuu, Maana Yeye atawakanyaga watesi wetu.
Zaburi 108:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ee Mungu, moyo wangu u thabiti, Nitaimba, nitaimba zaburi, Naam, kwa utukufu wangu. Amka, kinanda na kinubi, Nitaamka alfajiri. Ee BWANA, nitakushukuru kati ya watu, Nitakuimbia zaburi kati ya mataifa. Maana fadhili zako ni kubwa hata mbinguni, Na uaminifu wako hata mawinguni. Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu, Na juu ya nchi yote uwe utukufu wako. Ili wapenzi wako waopolewe, Uokoe kwa mkono wako wa kuume, uniitikie. Mungu amenena kwa utakatifu wake, Nami nitashangilia. Nitaigawanya Shekemu, Nitalipima bonde la Sukothi. Gileadi ni yangu, na Manase ni yangu, Na Efraimu ni nguvu ya kichwa changu. Yuda ni fimbo yangu ya kifalme, Moabu ni bakuli langu la kunawia. Nitamtupia Edomu kiatu changu, Na kumpigia Filisti kelele za vita. Ni nani atakayenipeleka hata mji wenye boma? Ni nani atakayeniongoza hata Edomu? Ee Mungu, si Wewe uliyetutupa? Wala, Ee Mungu, hutoki na majeshi yetu? Utuletee msaada juu ya mtesi, Maana wokovu wa binadamu haufai. Kwa msaada wa Mungu tutatenda makuu, Maana Yeye atawakanyaga watesi wetu.
Zaburi 108:1-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ee Mungu, moyo wangu ni thabiti; nitaimba na kusifu kwa moyo wangu wote. Amka, kinubi na zeze! Nitayaamsha mapambazuko. Nitakusifu wewe, Ee BWANA, katikati ya mataifa; nitaimba habari zako, katikati ya jamaa za watu. Kwa maana upendo wako ni mkuu, ni juu kuliko mbingu; uaminifu wako unazifikia anga. Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu, utukufu wako na uenee duniani kote. Tuokoe na utusaidie kwa mkono wako wa kuume, ili wale uwapendao wapate kuokolewa. Mungu amenena kutoka patakatifu pake: “Nitaigawa Shekemu kwa ushindi na kulipima Bonde la Sukothi. Gileadi ni yangu, Manase ni yangu, Efraimu ni kofia yangu ya chuma, nayo Yuda ni fimbo yangu ya utawala. Moabu ni sinia langu la kunawia, juu ya Edomu natupa kiatu changu; nashangilia kwa kushindwa kwa Ufilisti.” Ni nani atakayenipeleka hadi mji wenye ngome? Ni nani atakayeniongoza hadi nifike Edomu? Ee Mungu, si ni wewe uliyetukataa sisi, na hutoki tena na majeshi yetu? Tuletee msaada dhidi ya adui, kwa maana msaada wa mwanadamu haufai kitu. Kwa msaada wa Mungu tutapata ushindi, naye atawaponda adui zetu.