Zaburi 107:33-43
Zaburi 107:33-43 Biblia Habari Njema (BHN)
Mungu aliigeuza mito kuwa jangwa, chemchemi akazikausha kabisa. Ardhi yenye rutuba akaifanya udongo wa chumvi, kwa sababu ya uovu wa wakazi wake. Aligeuza majangwa kuwa mabwawa ya maji, na nchi kame kuwa chemchemi za maji. Akawahamishia huko wenye njaa, nao wakajenga mji wa kukalika. Walilima mashamba na kupanda mizabibu, wakavuna mazao kwa wingi. Aliwabariki watu wake, wakaongezeka; na idadi ya wanyama wao akaizidisha. Kisha walipopungua na kuwa wanyonge, kwa kukandamizwa, kuteswa na huzuni, aliwadharau wakuu waliowatesa, akawazungusha jangwani kusiko na njia. Lakini aliwaokoa wahitaji katika taabu zao, akaongeza jamaa zao kama kundi la kondoo. Waadilifu waonapo jambo hilo wanafurahi, lakini waovu wote wananyamazishwa. Wenye hekima na wayafikirie mambo haya, wazitambue fadhili zake Mwenyezi-Mungu.
Zaburi 107:33-43 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Amegeuza mito ikawa jangwa, Na chemchemi za maji zikawa nchi kavu. Nchi ya matunda mengi ikawa uwanda wa chumvi, Kwa sababu ya uovu wa wakazi wake. Amegeuza jangwa ikawa ziwa la maji, Na nchi kavu ikawa chemchemi za maji. Maana amewakalisha huko wenye njaa, Nao wamejenga mji wa kukaa. Wakapanda mbegu katika mashamba, Na kutia mizabibu iliyotoa matunda yake. Naye aliwabariki wakaongezeka sana, Wala hawapunguzi mifugo wao. Walipopungua na kudhilika, Kwa kuonewa na dhiki na huzuni. Aliwamwagia wakuu dharau, Na kuwazungusha katika nyika isiyo na njia. Lakini alimwinua mhitaji juu mbali na mateso, Na kuwaongeza jamaa zao kama kundi la kondoo. Wanyofu wa moyo wanaona na kufurahi, Na waovu wote wananyamazishwa. Aliye na hekima na ayaangalie hayo; Na wazitafakari fadhili za BWANA.
Zaburi 107:33-43 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Amegeuza mito ikawa jangwa, Na chemchemi za maji zikawa nchi ya kiu. Nchi ya matunda mengi ikawa uwanda wa chumvi, Kwa sababu ya ubaya wao walioikaa. Amegeuza jangwa ikawa ziwa la maji, Na nchi kavu ikawa chemchemi za maji. Maana amewakalisha huko wenye njaa, Nao wametengeneza mji wa kukaa. Wakapanda mbegu katika mashamba, Na kutia mizabibu iliyotoa matunda yake. Naye huwabariki wakaongezeka sana, Wala hayapunguzi makundi yao. Kisha wakapungua na kudhilika, Kwa kuonewa na mabaya na huzuni. Akawamwagia wakuu dharau, Na kuwazungusha katika nyika isiyo na njia. Akamweka mhitaji juu mbali na mateso, Akamfanyia jamaa kama kundi la kondoo. Wanyofu wa moyo wataona na kufurahi, Na uovu wa kila namna utajifumba kinywa. Aliye na hekima na ayaangalie hayo; Na wazitafakari fadhili za BWANA.
Zaburi 107:33-43 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Yeye aligeuza mito kuwa jangwa, chemchemi za maji zinazotiririka kuwa ardhi yenye kiu, nchi inayozaa ikawa ya chumvi isiyofaa, kwa sababu ya uovu wa wale walioishi humo. Aligeuza jangwa likawa madimbwi ya maji, nayo ardhi kame kuwa chemchemi za maji zinazotiririka; aliwaleta wenye njaa wakaishi humo, nao wakajenga mji wangeweza kuishi. Walilima mashamba na kupanda mizabibu, nayo ikazaa matunda mengi, Mungu aliwabariki, hesabu yao ikaongezeka sana, wala hakuruhusu mifugo yao kupungua. Kisha hesabu yao ilipungua, na walinyenyekeshwa kwa kuonewa, maafa na huzuni. Yeye ambaye huwamwagia dharau wakuu, aliwafanya watangetange nyikani isiyo na njia. Lakini yeye aliwainua wahitaji katika taabu zao, na kuongeza jamaa zao kama makundi ya kondoo. Wanyofu wataona na kufurahi, lakini waovu wote watafunga vinywa vyao. Yeyote aliye na hekima, ayasikie mambo haya, na atafakari upendo mkuu wa BWANA.