Zaburi 107:33-43
Zaburi 107:33-43 SRUV
Amegeuza mito ikawa jangwa, Na chemchemi za maji zikawa nchi kavu. Nchi ya matunda mengi ikawa uwanda wa chumvi, Kwa sababu ya uovu wa wakazi wake. Amegeuza jangwa ikawa ziwa la maji, Na nchi kavu ikawa chemchemi za maji. Maana amewakalisha huko wenye njaa, Nao wamejenga mji wa kukaa. Wakapanda mbegu katika mashamba, Na kutia mizabibu iliyotoa matunda yake. Naye aliwabariki wakaongezeka sana, Wala hawapunguzi mifugo wao. Walipopungua na kudhilika, Kwa kuonewa na dhiki na huzuni. Aliwamwagia wakuu dharau, Na kuwazungusha katika nyika isiyo na njia. Lakini alimwinua mhitaji juu mbali na mateso, Na kuwaongeza jamaa zao kama kundi la kondoo. Wanyofu wa moyo wanaona na kufurahi, Na waovu wote wananyamazishwa. Aliye na hekima na ayaangalie hayo; Na wazitafakari fadhili za BWANA.