Methali 3:1-12
Methali 3:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwanangu, usiyasahau mafundisho yangu, bali kwa moyo wako uzishike amri zangu. Maana yatakupa wingi wa siku, maisha marefu na fanaka kwa wingi. Utii na uaminifu visitengane nawe. Vifunge shingoni mwako; viandike moyoni mwako. Hivyo utakubalika na kusifika, mbele ya Mungu na mbele ya wanadamu. Mtumaini Mwenyezi-Mungu kwa moyo wako wote, wala usitegemee akili zako mwenyewe. Umtambue Mungu katika kila ufanyalo, naye atazinyosha njia zako. Usijione wewe mwenyewe kuwa mwenye hekima; mche Mwenyezi-Mungu na kujiepusha na uovu. Hiyo itakuwa dawa mwilini mwako, na kiburudisho mifupani mwako. Mheshimu Mwenyezi-Mungu kwa mali yako, na kwa malimbuko ya mazao yako yote. Hapo ghala zako zitajaa nafaka, na mapipa yako yatafurika divai mpya. Mwanangu, usidharau adhabu ya Mwenyezi-Mungu, wala usiudhike kwa maonyo yake; maana Mwenyezi-Mungu humwonya yule ampendaye, kama baba amwonyavyo mwanawe mpenzi.
Methali 3:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mwanangu, usiisahau sheria yangu, Bali moyo wako uzishike amri zangu. Maana zitakuongezea wingi wa siku. Na miaka ya uzima, na amani. Rehema na kweli zisiachane nawe; Zifunge shingoni mwako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako. Ndivyo utakavyopata kibali na akili nzuri, Mbele za Mungu na mbele ya mwanadamu. Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako. Usiwe na hekima machoni pako; Mche BWANA, ukajiepushe na uovu. Itakuwa afya mwilini pako, Na mafuta mifupani mwako. Mheshimu BWANA kwa mali yako, Na kwa malimbuko ya mazao yako yote. Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi, Na vyombo vyako vitafurika divai mpya. Mwanangu, usidharau kuadhibiwa na BWANA, Wala usione ni taabu kurudiwa naye. Kwa kuwa BWANA ampendaye humrudi, Kama vile baba mwanawe ampendezaye.
Methali 3:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mwanangu, usiisahau sheria yangu, Bali moyo wako uzishike amri zangu. Maana zitakuongezea wingi wa siku. Na miaka ya uzima, na amani. Rehema na kweli zisifarakane nawe; Zifunge shingoni mwako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako. Ndivyo utakavyopata kibali na akili nzuri, Mbele za Mungu na mbele ya mwanadamu. Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako. Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche BWANA, ukajiepushe na uovu. Itakuwa afya mwilini pako, Na mafuta mifupani mwako. Mheshimu BWANA kwa mali yako, Na kwa malimbuko ya mazao yako yote. Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi, Na mashinikizo yako yatafurika divai mpya. Mwanangu, usidharau kuadhibiwa na BWANA, Wala usione ni taabu kurudiwa naye. Kwa kuwa BWANA ampendaye humrudi, Kama vile baba mwanawe ampendezaye.
Methali 3:1-12 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mwanangu, usisahau mafundisho yangu, bali zitunze amri zangu moyoni mwako, kwa kuwa zitakuongezea miaka mingi ya maisha yako na kukuletea mafanikio. Usiache kamwe upendo na uaminifu vitengane nawe; vifunge shingoni mwako, viandike katika ubao wa moyo wako. Ndipo utapata kibali na jina zuri mbele za Mungu na mwanadamu. Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote wala usizitegemee akili zako mwenyewe; katika njia zako zote mkiri yeye, naye atayanyoosha mapito yako. Usiwe mwenye hekima machoni pako mwenyewe; mche BWANA ukajiepushe na uovu. Hii itakuletea afya mwilini mwako, na lishe kwenye mifupa yako. Mheshimu BWANA kwa mali yako na kwa malimbuko ya mazao yako yote; ndipo ghala zako zitakapojaa hadi kufurika, viriba vyako vitafurika kwa mvinyo mpya. Mwanangu, usidharau adhabu ya BWANA na usichukie maonyo yake, kwa sababu BWANA huwaadibisha wale anaowapenda, kama vile baba afanyavyo kwa mwana apendezwaye naye.