Wafilipi 4:10-20
Wafilipi 4:10-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Katika kuungana na Bwana nimepata furaha kubwa kwamba mwishoni mlipata tena fursa ya kuonesha kwamba mnanikumbuka. Kusema kweli mmekuwa mkinikumbuka daima ila tu hamkupata nafasi ya kuonesha jambo hilo. Sisemi hivyo sasa kwa sababu nahitaji kitu; maana nimejifunza kuridhika na vitu nilivyo navyo. Najua hali ya kutokuwa na vitu na hali ya kuwa na vingi. Nimejizoeza kuridhika katika kila hali na mahali; niwe nina cha kutosha au nina njaa; iwe nina ziada au nimepungukiwa. Naweza kuikabili kila hali kwani Kristo hunipa nguvu. Hata hivyo, nyinyi mlifanya vema kwa kushirikiana nami katika taabu zangu. Nyinyi Wafilipi mwafahamu wenyewe kwamba mwanzoni mwa kuhubiri Habari Njema, nilipokuwa naondoka Makedonia, nyinyi peke yenu ndio kanisa lililonisaidia; nyinyi peke yenu ndio mlioshirikiana nami katika kupokea na kuwapa wengine mahitaji. Nilipokuwa nahitaji msaada kule Thesalonike mliniletea, tena zaidi ya mara moja. Sio kwamba napenda tu kupokea zawadi; ninachotaka ni faida iongezwe katika hazina yenu. Basi, nimekwisha pokea vitu vyote mlivyonipa, tena ni zaidi kuliko nilivyohitaji. Nina kila kitu kwa vile sasa Epafrodito amekwisha niletea zawadi zenu. Zawadi hizi ni kama tambiko yenye harufu nzuri, sadaka inayokubaliwa na kumpendeza Mungu. Basi, Mungu wangu, kwa utajiri wake mkuu kwa njia ya Kristo, atawapeni mahitaji yenu yote. Utukufu uwe kwa Mungu wetu na Baba yetu, milele na milele. Amina.
Wafilipi 4:10-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nilifurahi sana katika Bwana, kwa kuwa sasa mwisho mmehuisha tena fikira zenu kwa ajili yangu, kama vile mlivyokuwa mkinifikiri hali yangu lakini hamkupata nafasi. Si kwamba nasema haya kwa kuwa nina mahitaji; maana nimejifunza kuwa radhi na hali yoyote niliyo nayo. Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yoyote, na katika mambo yoyote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa. Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu. Lakini mlifanya vema, mliposhiriki nami katika dhiki yangu. Nanyi pia, ninyi wenyewe mnajua, enyi Wafilipi, ya kuwa katika mwanzo wa Injili, nilipotoka Makedonia, hakuna kanisa lingine lililoshirikiana nami katika habari hii ya kutoa na kupokea, ila ninyi peke yenu. Kwa kuwa hata huko Thesalonike mliniletea msaada kwa mahitaji yangu, wala si mara moja. Si kwamba nakitamani kile kipawa, bali nayatamani mazao yanayozidi kuwa mengi, katika hesabu yenu. Lakini ninavyo vitu vyote na kuzidi, tena nimejaa tele; nimepokea kwa mkono wa Epafrodito vitu vile vilivyotoka kwenu, harufu ya manukato, sadaka yenye kibali, impendezayo Mungu. Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu. Sasa atukuzwe Mungu, Baba yetu, milele na milele. Amina.
Wafilipi 4:10-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nalifurahi sana katika Bwana, kwa kuwa sasa mwisho mmehuisha tena fikira zenu kwa ajili yangu, kama vile mlivyokuwa mkinifikiri hali yangu lakini hamkupata nafasi. Si kwamba nasema haya kwa kuwa nina mahitaji; maana nimejifunza kuwa radhi na hali yo yote niliyo nayo. Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa. Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu. Lakini mlifanya vema, mliposhiriki nami katika dhiki yangu. Nanyi pia, ninyi wenyewe mnajua, enyi Wafilipi, ya kuwa katika mwanzo wa Injili, nilipotoka Makedonia, hakuna kanisa lingine lililoshirikiana nami katika habari hii ya kutoa na kupokea, ila ninyi peke yenu. Kwa kuwa hata huko Thesalonike mliniletea msaada kwa mahitaji yangu, wala si mara moja. Si kwamba nakitamani kile kipawa, bali nayatamani mazao yanayozidi kuwa mengi, katika hesabu yenu. Lakini ninavyo vitu vyote na kuzidi, tena nimejaa tele; nimepokea kwa mkono wa Epafrodito vitu vile vilivyotoka kwenu, harufu ya manukato, sadaka yenye kibali, impendezayo Mungu. Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu. Sasa atukuzwe Mungu, Baba yetu, milele na milele. Amina.
Wafilipi 4:10-20 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Nina furaha kubwa katika Bwana Isa kwamba hatimaye mmeanza upya kushughulika tena na maisha yangu. Kweli mmekuwa mkinifikiria lakini mlikuwa hamjapata nafasi ya kufanya hivyo. Sisemi hivyo kwa vile nina mahitaji, la! Kwa maana nimejifunza kuridhika katika hali yoyote. Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa. Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu. Lakini, mlifanya vyema kushiriki nami katika taabu zangu. Zaidi ya hayo, ninyi Wafilipi mnajua kwamba siku za kwanza nilipoanza kuhubiri Injili, nilipoondoka Makedonia, hakuna kundi lingine la waumini lililoshiriki nami katika masuala ya kutoa na kupokea isipokuwa ninyi. Kwa maana hata nilipokuwa huko Thesalonike, mliniletea msaada kwa ajili ya mahitaji yangu zaidi ya mara moja. Si kwamba natafuta sana yale matoleo, bali natafuta sana ile faida itakayozidi sana kwa upande wenu. Nimelipwa kikamilifu hata na zaidi; nimetoshelezwa kabisa sasa, kwa kuwa nimepokea kutoka kwa Epafrodito vile vitu mlivyonitumia, sadaka yenye harufu nzuri, dhabihu inayokubalika na ya kumpendeza Mungu. Naye Mungu wangu atawajaza ninyi na kila mnachohitaji kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu ndani ya Al-Masihi Isa. Mungu wetu aliye Baba yetu apewe utukufu milele na milele. Amen.