Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Wafilipi 4:1-23

Wafilipi 4:1-23 Biblia Habari Njema (BHN)

Kwa hiyo, ndugu zangu wapenzi, ninaotamani sana kuwaoneni, nyinyi mlio furaha yangu na taji ya ushindi wangu, ndivyo basi mnavyopaswa kukaa imara katika kuungana na Bwana, enyi wapenzi wangu. Euodia na Suntike, nawaombeni na kuwasihi mpatane kama ndugu katika Bwana. Nawe ndugu yangu mwaminifu, nakutaka uwasaidie akina mama hao, kwani wamefanya kazi ya kueneza Injili kwa bidii pamoja nami na Klementi na wafanyakazi wenzangu wengine wote ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uhai. Basi, furahini daima katika kuungana na Bwana! Nasema tena: Furahini! Upole wenu ujulikane kwa watu wote. Bwana yu karibu. Msiwe na wasiwasi juu ya kitu chochote, ila kwa kila hali, mwombeni Mungu katika sala juu ya mahitaji yenu, kwa shukrani. Nayo amani ya Mungu ipitayo akili zote za watu italinda salama mioyo na akili zenu katika kuungana na Kristo Yesu. Hatimaye, ndugu zangu, zingatieni mambo mema na yanayostahili kusifiwa; mambo ya kweli na bora; mambo ya haki, safi, ya kupendeza na ya heshima. Tekelezeni yale mliyojifunza na kupokea kutoka kwangu; mambo mliyosikia nimesema na kuona nimeyatenda. Naye Mungu anayetujalia amani atakuwa pamoja nanyi. Katika kuungana na Bwana nimepata furaha kubwa kwamba mwishoni mlipata tena fursa ya kuonesha kwamba mnanikumbuka. Kusema kweli mmekuwa mkinikumbuka daima ila tu hamkupata nafasi ya kuonesha jambo hilo. Sisemi hivyo sasa kwa sababu nahitaji kitu; maana nimejifunza kuridhika na vitu nilivyo navyo. Najua hali ya kutokuwa na vitu na hali ya kuwa na vingi. Nimejizoeza kuridhika katika kila hali na mahali; niwe nina cha kutosha au nina njaa; iwe nina ziada au nimepungukiwa. Naweza kuikabili kila hali kwani Kristo hunipa nguvu. Hata hivyo, nyinyi mlifanya vema kwa kushirikiana nami katika taabu zangu. Nyinyi Wafilipi mwafahamu wenyewe kwamba mwanzoni mwa kuhubiri Habari Njema, nilipokuwa naondoka Makedonia, nyinyi peke yenu ndio kanisa lililonisaidia; nyinyi peke yenu ndio mlioshirikiana nami katika kupokea na kuwapa wengine mahitaji. Nilipokuwa nahitaji msaada kule Thesalonike mliniletea, tena zaidi ya mara moja. Sio kwamba napenda tu kupokea zawadi; ninachotaka ni faida iongezwe katika hazina yenu. Basi, nimekwisha pokea vitu vyote mlivyonipa, tena ni zaidi kuliko nilivyohitaji. Nina kila kitu kwa vile sasa Epafrodito amekwisha niletea zawadi zenu. Zawadi hizi ni kama tambiko yenye harufu nzuri, sadaka inayokubaliwa na kumpendeza Mungu. Basi, Mungu wangu, kwa utajiri wake mkuu kwa njia ya Kristo, atawapeni mahitaji yenu yote. Utukufu uwe kwa Mungu wetu na Baba yetu, milele na milele. Amina. Nawasalimu watu wote wa Mungu walio wake Kristo Yesu. Ndugu walio pamoja nami hapa wanawasalimuni. Watu wote wa Mungu hapa, na hasa wale walio katika ikulu ya mfalme, wanawasalimuni. Nawatakieni nyote neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.

Shirikisha
Soma Wafilipi 4

Wafilipi 4:1-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi, ndugu zangu, wapendwa wangu, ninaowaonea shauku, furaha yangu, na taji langu, hivyo simameni imara katika Bwana, wapenzi wangu. Namsihi Euodia, namsihi na Sintike, wawe na nia moja katika Bwana. Naam, nataka na wewe pia, mtumwa mwenzangu wa kweli, uwasaidie wanawake hao; kwa maana waliishindania Injili pamoja nami, na Klementi naye, na wale wengine waliofanya kazi pamoja nami, ambao majina yao yamo katika kitabu cha uzima. Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema, Furahini. Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yuko karibu. Msijisumbue kwa neno lolote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu. Hatimaye, ndugu zangu, mambo yoyote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo ya heshima, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote yenye kupendeza, yoyote yenye sifa njema; ukiwapo wema wowote, ikiwapo sifa nzuri yoyote, yatafakarini hayo. Mambo mliyojifunza kwangu na kuyapokea, na kuyasikia na kuyaona kwangu, yatendeni hayo; na Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi. Nilifurahi sana katika Bwana, kwa kuwa sasa mwisho mmehuisha tena fikira zenu kwa ajili yangu, kama vile mlivyokuwa mkinifikiri hali yangu lakini hamkupata nafasi. Si kwamba nasema haya kwa kuwa nina mahitaji; maana nimejifunza kuwa radhi na hali yoyote niliyo nayo. Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yoyote, na katika mambo yoyote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa. Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu. Lakini mlifanya vema, mliposhiriki nami katika dhiki yangu. Nanyi pia, ninyi wenyewe mnajua, enyi Wafilipi, ya kuwa katika mwanzo wa Injili, nilipotoka Makedonia, hakuna kanisa lingine lililoshirikiana nami katika habari hii ya kutoa na kupokea, ila ninyi peke yenu. Kwa kuwa hata huko Thesalonike mliniletea msaada kwa mahitaji yangu, wala si mara moja. Si kwamba nakitamani kile kipawa, bali nayatamani mazao yanayozidi kuwa mengi, katika hesabu yenu. Lakini ninavyo vitu vyote na kuzidi, tena nimejaa tele; nimepokea kwa mkono wa Epafrodito vitu vile vilivyotoka kwenu, harufu ya manukato, sadaka yenye kibali, impendezayo Mungu. Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu. Sasa atukuzwe Mungu, Baba yetu, milele na milele. Amina. Mnisalimie kila mtakatifu katika Kristo Yesu. Ndugu walio pamoja nami wanawasalimu. Watakatifu wote wanawasalimu, hasa wao walio wa nyumbani mwa Kaisari. Neema ya Bwana Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu.

Shirikisha
Soma Wafilipi 4

Wafilipi 4:1-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi, ndugu zangu, wapendwa wangu, ninaowaonea shauku, furaha yangu, na taji yangu, hivyo simameni imara katika Bwana, wapenzi wangu. Namsihi Euodia, namsihi na Sintike, wawe na nia moja katika Bwana. Naam, nataka na wewe pia, mjoli wa kweli, uwasaidie wanawake hao; kwa maana waliishindania Injili pamoja nami, na Klementi naye, na wale wengine waliotenda kazi pamoja nami, ambao majina yao yamo katika kitabu cha uzima. Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema, Furahini. Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu. Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo. Mambo mliyojifunza kwangu na kuyapokea, na kuyasikia na kuyaona kwangu, yatendeni hayo; na Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi. Nalifurahi sana katika Bwana, kwa kuwa sasa mwisho mmehuisha tena fikira zenu kwa ajili yangu, kama vile mlivyokuwa mkinifikiri hali yangu lakini hamkupata nafasi. Si kwamba nasema haya kwa kuwa nina mahitaji; maana nimejifunza kuwa radhi na hali yo yote niliyo nayo. Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa. Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu. Lakini mlifanya vema, mliposhiriki nami katika dhiki yangu. Nanyi pia, ninyi wenyewe mnajua, enyi Wafilipi, ya kuwa katika mwanzo wa Injili, nilipotoka Makedonia, hakuna kanisa lingine lililoshirikiana nami katika habari hii ya kutoa na kupokea, ila ninyi peke yenu. Kwa kuwa hata huko Thesalonike mliniletea msaada kwa mahitaji yangu, wala si mara moja. Si kwamba nakitamani kile kipawa, bali nayatamani mazao yanayozidi kuwa mengi, katika hesabu yenu. Lakini ninavyo vitu vyote na kuzidi, tena nimejaa tele; nimepokea kwa mkono wa Epafrodito vitu vile vilivyotoka kwenu, harufu ya manukato, sadaka yenye kibali, impendezayo Mungu. Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu. Sasa atukuzwe Mungu, Baba yetu, milele na milele. Amina. Mnisalimie kila mtakatifu katika Kristo Yesu. Ndugu walio pamoja nami wawasalimu. Watakatifu wote wawasalimu, hasa wao walio wa nyumbani mwa Kaisari. Neema ya Bwana Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu.

Shirikisha
Soma Wafilipi 4

Wafilipi 4:1-23 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Kwa hiyo, ndugu zangu, ninaowapenda na ambao ninawaonea shauku, ninyi mlio furaha yangu na taji langu, hivi ndivyo iwapasavyo kusimama imara katika Bwana, ninyi wapendwa wangu. Nawasihi Euodia na Sintike wawe na nia moja katika Bwana. Naam, nakusihi wewe pia, mwenzangu mwaminifu, uwasaidie hawa wanawake, kwa sababu walijitaabisha katika kazi ya Injili pamoja nami bega kwa bega, wakiwa pamoja na Klementi na watendakazi wenzangu ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima. Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema furahini! Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu. Hatimaye, ndugu zangu, mambo yote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo na sifa njema, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote ya kupendeza, yoyote yenye staha, ukiwepo uzuri wowote, pakiwepo chochote kinachostahili kusifiwa, tafakarini mambo hayo. Mambo yote mliyojifunza au kuyapokea au kuyasikia kutoka kwangu, au kuyaona kwangu, yatendeni hayo. Naye Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi. Nina furaha kubwa katika Bwana kwamba hatimaye mmeanza upya kushughulika tena na maisha yangu. Kweli mmekuwa mkinifikiria lakini mlikuwa hamjapata nafasi ya kufanya hivyo. Sisemi hivyo kwa vile nina mahitaji, la! Kwa maana nimejifunza kuridhika katika hali yoyote. Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa. Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu. Lakini, mlifanya vyema kushiriki nami katika taabu zangu. Zaidi ya hayo, ninyi Wafilipi mnajua kwamba siku za kwanza nilipoanza kuhubiri Injili, nilipoondoka Makedonia, hakuna kanisa lingine lililoshiriki nami katika masuala ya kutoa na kupokea isipokuwa ninyi. Kwa maana hata nilipokuwa huko Thesalonike, mliniletea msaada kwa ajili ya mahitaji yangu zaidi ya mara moja. Si kwamba natafuta sana yale matoleo, bali natafuta sana ile faida itakayozidi sana kwa upande wenu. Nimelipwa kikamilifu hata na zaidi; nimetoshelezwa kabisa sasa, kwa kuwa nimepokea kutoka kwa Epafrodito vile vitu mlivyonitumia, sadaka yenye harufu nzuri, dhabihu inayokubalika na ya kumpendeza Mungu. Naye Mungu wangu atawajaza ninyi na kila mnachohitaji kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu ndani ya Kristo Yesu. Mungu wetu aliye Baba yetu apewe utukufu milele na milele. Amen. Msalimuni kila mtakatifu katika Kristo Yesu. Ndugu walio pamoja nami wanawasalimu. Watakatifu wote wanawasalimu, hasa wale watu wa nyumbani mwa Kaisari. Neema ya Bwana Yesu Kristo iwe pamoja na roho zenu. Amen.

Shirikisha
Soma Wafilipi 4