Wafilipi 2:1-30
Wafilipi 2:1-30 Biblia Habari Njema (BHN)
Je, maisha yenu katika Kristo yanawapeni nguvu? Je, upendo wake unawafarijini? Je, mnao umoja na Roho Mtakatifu na kuoneana huruma na kusikitikiana nyinyi kwa nyinyi? Basi, ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na fikira moja, upendo mmoja, moyo mmoja na nia moja. Msifanye chochote kwa moyo wa fitina au kwa majivuno ya bure; muwe na unyenyekevu nyinyi kwa nyinyi, na kila mmoja amwone mwenzake kuwa bora kuliko yeye mwenyewe. Pasiwe na mtu anayetafuta faida yake mwenyewe tu bali faida ya mwenzake. Muwe na msimamo uleule aliokuwa nao Kristo Yesu: Yeye, kwa asili alikuwa daima Mungu; lakini hakufikiri kwamba kule kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kungangania kwa nguvu. Bali, kwa hiari yake mwenyewe, aliachilia hayo yote, akajitwalia hali ya mtumishi, akawa sawa na wanadamu, akaonekana kama wanadamu. Alijinyenyekesha na kutii mpaka kufa, hata kufa msalabani. Kwa sababu hiyo Mungu alimkweza juu kabisa, akampa jina lililo kuu kuliko majina yote. Ili kwa heshima ya jina la Yesu, viumbe vyote mbinguni, duniani na kuzimu, vipige magoti mbele yake, na kila mtu akiri kwamba Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba. Wapenzi wangu, nilipokuwa nanyi mlinitii daima, na hata sasa niwapo mbali nanyi endeleeni kutii. Fanyeni kazi kwa hofu na tetemeko kwa ajili ya ukombozi wenu, kwani Mungu ndiye afanyaye kazi daima ndani yenu, na kuwapeni uwezo wa kutaka na kutekeleza mambo yanayopatana na mpango wake mwenyewe. Fanyeni kila kitu bila kunungunika na bila ubishi, ili mpate kuwa watu safi, wasio na lawama, kama watoto wanyofu wa Mungu wanaoishi katika ulimwengu mbaya na uliopotoka. Mtangara kati yao kama nyota zinavyoliangaza anga, mkishika imara ujumbe wa uhai. Na hapo ndipo nami nitakapokuwa na sababu ya kujivunia katika siku ile ya Kristo, kwani itaonekana dhahiri kwamba bidii yangu na kazi yangu havikupotea bure. Hata ikiwa nitatolewa mhanga pamoja na imani yenu iliyo tambiko kwa Mungu, basi, nafurahi sana na kuwashirikisha nyinyi nyote furaha hiyo. Hali kadhalika nanyi mnapaswa kufurahi na kunishirikisha mimi furaha yenu. Katika kuungana na Bwana Yesu ninalo tumaini kwamba nitaweza kumtuma Timotheo kwenu hivi karibuni, ili nitiwe moyo kwa kupata habari zenu. Sina mtu mwingine kama yeye ambaye anawashughulikieni kwa moyo. Wengine wanashughulikia tu mambo yao wenyewe badala ya kuyashughulikia mambo ya Yesu Kristo. Nyinyi wenyewe mwafahamu jinsi Timotheo alivyo thabiti; yeye na mimi, kama vile mtoto na baba yake, tumefanya kazi pamoja kwa ajili ya Injili. Kwa hiyo natumaini kumtuma kwenu mara nitakapojua jinsi mambo yatakavyoniendea. Na, ninatumaini katika Bwana kwamba nami pia nitaweza kuja kwenu karibuni. Nimeona sina budi kumtuma kwenu ndugu yetu Epafrodito, ambaye ni mwenzangu kazini na vitani na ambaye ni mjumbe wenu aliyenisaidia katika mahitaji yangu. Anayo hamu kubwa ya kuwaoneni nyinyi nyote, na amesikitika sana kwani nyinyi mmepata habari kwamba alikuwa mgonjwa. Naam, alikuwa mgonjwa hata karibu ya kufa. Lakini Mungu alimwonea huruma, na si yeye peke yake, ila na mimi pia ili nisipate uchungu zaidi. Basi, nataka sana kumtuma kwenu, ili mtakapomwona mpate kufurahi tena, nayo huzuni yangu itoweke. Mpokeeni, basi, kwa furaha yote kama ndugu katika Bwana. Mnapaswa kuwastahi watu walio kama yeye, kwani yeye alikuwa hata karibu ya kufa kwa ajili ya kazi ya Kristo, na kuhatarisha maisha yake ili aweze kunipa mimi msaada ule ambao hamkuweza kuuleta nyinyi wenyewe.
Wafilipi 2:1-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi ikiwako faraja yoyote katika Kristo, yakiwako matulizo yoyote ya mapenzi, ukiwako ushirika wowote wa Roho, ikiwako huruma yoyote na rehema, ijalizeni furaha yangu, ili muwe na nia moja, wenye mapenzi mamoja, wenye roho moja, mkiwaza mamoja. Msitende neno lolote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine. Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuko na namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba. Basi, wapendwa wangu, kama vile mlivyotii sikuzote, si wakati mimi nilipokuwapo tu, bali sasa zaidi sana mimi nisipokuwapo, utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka. Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema. Yatendeni mambo yote pasipo manung'uniko wala mashindano, mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu, mkishika neno la uzima; nipate sababu ya kuona fahari katika siku ya Kristo, ya kuwa sikupiga mbio bure wala sikujitaabisha bure. Naam, hata nikimiminwa juu ya dhabihu na ibada ya imani yenu, nafurahi; tena nafurahi pamoja nanyi nyote. Nanyi vivyo hivyo furahini, tena furahini pamoja nami. Lakini natumaini katika Bwana Yesu kumtuma Timotheo afike kwenu karibu, nifarijiwe na mimi, nikiijua hali yenu. Maana sina mtu mwingine mwenye nia moja nami, atakayeiangalia hali yenu kweli kweli. Maana wote wanatafuta vyao wenyewe, sivyo vya Kristo Yesu. Ila mwajua sifa yake, ya kuwa ametumika pamoja nami kwa ajili ya Injili, kama mwana na baba yake. Basi, natumaini kumtuma huyo mara, hapo nitakapojua yatakayonipata. Nami naamini katika Bwana ya kuwa nitakuja na mimi mwenyewe hivi karibuni. Lakini niliona imenilazimu kumtuma kwenu Epafrodito, ndugu yangu, mfanyakazi pamoja nami, askari pamoja nami; tena ni mtume wenu na mhudumu wa mahitaji yangu. Kwa kuwa alikuwa na shauku kwenu ninyi nyote, akahuzunika sana, kwa sababu mlisikia ya kwamba alikuwa mgonjwa. Kwa maana alikuwa mgonjwa sana, karibu kufa; lakini Mungu alimhurumia; wala si yeye peke yake, ila na mimi pia; nisiwe na huzuni juu ya huzuni. Kwa hiyo nimefanya bidii nyingi zaidi kumtuma, ili mtakapomwona tena mpate kufurahi, nami nipunguziwe huzuni yangu. Mpokeeni, basi, katika Bwana, kwa furaha yote, mkawahesabu watu kama huyu kuwa watu wa kuheshimiwa. Maana kwa ajili ya kazi ya Kristo alikaribia kufa akahatarisha roho yake ili kusudi aitimize huduma ambayo msingeweza kunitimizia.
Wafilipi 2:1-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi ikiwako faraja yo yote katika Kristo, yakiwako matulizo yo yote ya mapenzi, ukiwako ushirika wo wote wa Roho, ikiwako huruma yo yote na rehema, ijalizeni furaha yangu, ili mwe na nia moja, wenye mapenzi mamoja, wenye roho moja, mkinia mamoja. Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine. Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba. Basi, wapendwa wangu, kama vile mlivyotii sikuzote, si wakati mimi nilipokuwapo tu, bali sasa zaidi sana mimi nisipokuwapo, utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka. Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema. Yatendeni mambo yote pasipo manung’uniko wala mashindano, mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu, mkishika neno la uzima; nipate sababu ya kuona fahari katika siku ya Kristo, ya kuwa sikupiga mbio bure wala sikujitaabisha bure. Naam, hata nikimiminwa juu ya dhabihu na ibada ya imani yenu, nafurahi; tena nafurahi pamoja nanyi nyote. Nanyi vivyo hivyo furahini, tena furahini pamoja nami. Walakini natumaini katika Bwana Yesu kumtuma Timotheo afike kwenu karibu, nifarijiwe na mimi, nikiijua hali yenu. Maana sina mtu mwingine mwenye nia moja nami, atakayeiangalia hali yenu kweli kweli. Maana wote wanatafuta vyao wenyewe, sivyo vya Kristo Yesu. Ila mwajua sifa yake, ya kuwa ametumika pamoja nami kwa ajili ya Injili, kama mwana na baba yake. Basi, natumaini kumtuma huyo mara, hapo nitakapojua yatakayonipata. Nami naamini katika Bwana ya kuwa nitakuja na mimi mwenyewe hivi karibu. Lakini naliona imenilazimu kumtuma kwenu Epafrodito, ndugu yangu, mtenda kazi pamoja nami, askari pamoja nami; tena ni mtume wenu na mhudumu wa mahitaji yangu. Kwa kuwa alikuwa na shauku kwenu ninyi nyote, akahuzunika sana, kwa sababu mlisikia ya kwamba alikuwa hawezi. Kwa maana alikuwa hawezi kweli kweli, karibu na kufa; lakini Mungu alimhurumia; wala si yeye peke yake, ila na mimi pia; nisiwe na huzuni juu ya huzuni. Kwa hiyo nimefanya bidii nyingi zaidi kumtuma, ili mtakapomwona tena mpate kufurahi, nami nipunguziwe huzuni yangu. Mpokeeni, basi, katika Bwana, kwa furaha yote, mkawahesabu watu kama huyu kuwa watu wa kuheshimiwa. Maana kwa ajili ya kazi ya Kristo alikaribia kufa akaponza roho yake; ili kusudi ayatimize yaliyopungua katika huduma yenu kwangu.
Wafilipi 2:1-30 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kama kukiwa na jambo lolote la kutia moyo katika kuunganishwa na Kristo, kukiwa faraja yoyote katika upendo wake, kukiwa na ushirika wowote na Roho, kukiwa na wema wowote na huruma, basi ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia moja, mkiwa na upendo huo moja, mkiwa wa roho na kusudi moja. Msitende jambo lolote kwa nia ya kujitukuza wala kujivuna, bali kwa unyenyekevu kila mtu amhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake. Kila mmoja wenu asiangalie faida yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine. Kuweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Kristo Yesu: Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa, hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa kitu cha kushikilia, bali alijifanya si kitu, akachukua hali hasa ya mtumwa, naye akazaliwa katika umbo la mwanadamu. Naye akiwa na umbo la mwanadamu, alijinyenyekeza, akatii hata mauti: naam, mauti ya msalaba! Kwa hiyo, Mungu alimtukuza juu sana, na kumpa Jina lililo kuu kuliko kila jina, ili kwa Jina la Yesu, kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi, na kila ulimi ukiri kwamba Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba. Kwa hiyo, wapendwa wangu, kama vile mmekuwa mkitii siku zote, si tu wakati nikiwa pamoja nanyi, bali sasa zaidi sana nisipokuwepo, utimizeni wokovu wenu kwa kuogopa na kutetemeka, kwa maana Mungu ndiye atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu kwa kulitimiza kusudi lake jema. Fanyeni mambo yote bila kunungʼunika wala kushindana, ili msiwe na lawama wala hatia, bali mwe wana wa Mungu wasio na kasoro katika kizazi chenye ukaidi na kilichopotoka, ambacho ndani yake ninyi mnangʼaa kama mianga ulimwenguni. Mkilishika neno la uzima, ili nipate kuona fahari siku ya Kristo kwamba sikupiga mbio wala kujitaabisha bure. Lakini hata nikimiminwa kama sadaka ya kinywaji kwenye dhabihu na huduma inayotoka katika imani yenu, mimi ninafurahi na kushangilia pamoja nanyi nyote. Vivyo hivyo, ninyi nanyi imewapasa kufurahi na kushangilia pamoja nami. Natumaini katika Bwana Yesu kumtuma Timotheo hivi karibuni aje kwenu, ili nipate kufarijika moyo nitakapopata habari zenu. Sina mtu mwingine kama yeye, ambaye ataangalia hali yenu kwa halisi. Kwa maana kila mmoja anajishughulisha zaidi na mambo yake mwenyewe wala si yale ya Yesu Kristo. Lakini ninyi wenyewe mnajua jinsi Timotheo alivyojithibitisha mwenyewe, kwa maana ametumika pamoja nami kwa kazi ya Injili, kama vile mwana kwa baba yake. Kwa hiyo, ninatumaini kumtuma kwenu upesi mara nitakapojua mambo yangu yatakavyokuwa. Nami mwenyewe ninatumaini katika Bwana kwamba nitakuja kwenu hivi karibuni. Lakini nadhani ni muhimu kumtuma tena kwenu Epafrodito, ndugu yangu na mtendakazi pamoja nami, aliye askari mwenzangu, ambaye pia ni mjumbe wenu mliyemtuma ili ashughulike na mahitaji yangu. Kwa maana amekuwa akiwaonea sana shauku ninyi nyote, akiwa na wasiwasi kwa kuwa mlisikia kwamba alikuwa mgonjwa. Kweli alikuwa mgonjwa, tena karibu ya kufa. Lakini Mungu alimhurumia, wala si yeye tu, bali hata na mimi alinihurumia, nisipatwe na huzuni juu ya huzuni. Kwa hiyo mimi ninafanya bidii kumtuma kwenu ili mtakapomwona kwa mara nyingine, mpate kufurahi, nami wasiwasi wangu upungue. Kwa hiyo mpokeeni katika Bwana kwa furaha kubwa, nanyi wapeni heshima watu kama hawa, kwa sababu alikaribia kufa kwa ajili ya kazi ya Kristo, akihatarisha maisha yake ili aweze kunihudumia vile ninyi hamkuweza.