Wafilipi 2
BHN

Wafilipi 2

2
Unyenyekevu na ukuu wa Kristo
1Je, maisha yenu katika Kristo yanawapeni nguvu? Je, upendo wake unawafarijini? Je, mnao umoja na Roho Mtakatifu na kuoneana huruma na kusikitikiana nyinyi kwa nyinyi? 2Basi, ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na fikira moja, upendo mmoja, moyo mmoja na nia moja. 3Msifanye chochote kwa moyo wa fitina au kwa majivuno ya bure; muwe na unyenyekevu nyinyi kwa nyinyi, na kila mmoja amwone mwenzake kuwa bora kuliko yeye mwenyewe. 4Pasiwe na mtu anayetafuta faida yake mwenyewe tu bali faida ya mwenzake. 5Muwe na msimamo uleule aliokuwa nao Kristo Yesu:
6Yeye, kwa asili alikuwa daima Mungu;
lakini hakufikiri kwamba kule kuwa sawa na Mungu
ni kitu cha kungangania kwa nguvu.
7Bali, kwa hiari yake mwenyewe,
aliachilia hayo yote, akajitwalia hali ya mtumishi,
akawa sawa na wanadamu,
akaonekana kama wanadamu.
8Alijinyenyekesha na kutii mpaka kufa,
hata kufa msalabani.
9Kwa sababu hiyo Mungu alimkweza juu kabisa,
akampa jina lililo kuu kuliko majina yote.
10Ili kwa heshima ya jina la Yesu,
viumbe vyote mbinguni, duniani na kuzimu,
vipige magoti mbele yake,
11na kila mtu akiri kwamba Yesu Kristo ni Bwana,
kwa utukufu wa Mungu Baba.
Mwanga kwa ulimwengu
12Wapenzi wangu, nilipokuwa nanyi mlinitii daima, na hata sasa niwapo mbali nanyi endeleeni kutii. Fanyeni kazi kwa hofu na tetemeko kwa ajili ya ukombozi wenu, 13kwani Mungu ndiye afanyaye kazi daima ndani yenu, na kuwapeni uwezo wa kutaka na kutekeleza mambo yanayopatana na mpango wake mwenyewe.
14Fanyeni kila kitu bila kunungunika na bila ubishi, 15ili mpate kuwa watu safi, wasio na lawama, kama watoto wanyofu wa Mungu wanaoishi katika ulimwengu mbaya na uliopotoka. Mtangara kati yao kama nyota zinavyoliangaza anga, 16mkishika imara ujumbe wa uhai. Na hapo ndipo nami nitakapokuwa na sababu ya kujivunia katika siku ile ya Kristo, kwani itaonekana dhahiri kwamba bidii yangu na kazi yangu havikupotea bure.
17Hata ikiwa nitatolewa mhanga pamoja na imani yenu iliyo tambiko kwa Mungu, basi, nafurahi sana na kuwashirikisha nyinyi nyote furaha hiyo. 18Hali kadhalika nanyi mnapaswa kufurahi na kunishirikisha mimi furaha yenu.
Timotheo na Epafrodito
19Katika kuungana na Bwana Yesu ninalo tumaini kwamba nitaweza kumtuma Timotheo kwenu hivi karibuni, ili nitiwe moyo kwa kupata habari zenu. 20Sina mtu mwingine kama yeye ambaye anawashughulikieni kwa moyo. 21Wengine wanashughulikia tu mambo yao wenyewe badala ya kuyashughulikia mambo ya Yesu Kristo. 22Nyinyi wenyewe mwafahamu jinsi Timotheo alivyo thabiti; yeye na mimi, kama vile mtoto na baba yake, tumefanya kazi pamoja kwa ajili ya Injili. 23Kwa hiyo natumaini kumtuma kwenu mara nitakapojua jinsi mambo yatakavyoniendea. 24Na, ninatumaini katika Bwana kwamba nami pia nitaweza kuja kwenu karibuni.
25Nimeona sina budi kumtuma kwenu ndugu yetu Epafrodito, ambaye ni mwenzangu kazini na vitani na ambaye ni mjumbe wenu aliyenisaidia katika mahitaji yangu. 26Anayo hamu kubwa ya kuwaoneni nyinyi nyote, na amesikitika sana kwani nyinyi mmepata habari kwamba alikuwa mgonjwa. 27Naam, alikuwa mgonjwa hata karibu ya kufa. Lakini Mungu alimwonea huruma, na si yeye peke yake, ila na mimi pia ili nisipate uchungu zaidi. 28Basi, nataka sana kumtuma kwenu, ili mtakapomwona mpate kufurahi tena, nayo huzuni yangu itoweke. 29Mpokeeni, basi, kwa furaha yote kama ndugu katika Bwana. Mnapaswa kuwastahi watu walio kama yeye, 30kwani yeye alikuwa hata karibu ya kufa kwa ajili ya kazi ya Kristo, na kuhatarisha maisha yake ili aweze kunipa mimi msaada ule ambao hamkuweza kuuleta nyinyi wenyewe.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.


Jifunze Mengi Kuhusu Biblia Habari Njema

Encouraging and challenging you to seek intimacy with God every day.


YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy.