Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hesabu 22:21-41

Hesabu 22:21-41 Biblia Habari Njema (BHN)

Balaamu akaamka asubuhi, akatandika punda wake, akaenda pamoja na hao maofisa. Hasira ya Mungu iliwaka kwa sababu Balaamu alikuwa anakwenda; hivyo malaika wa Mwenyezi-Mungu akakabiliana naye njiani. Wakati huo Balaamu alikuwa amepanda punda wake akiwa na watumishi wake. Basi, punda alimwona malaika huyo wa Mwenyezi-Mungu amesimama njiani, ameshika upanga uliochomolewa alani mwake. Kwa hiyo aliiacha njia, akaenda pembeni. Balaamu akampiga huyo punda, akamrudisha njiani. Kisha malaika huyo wa Mwenyezi-Mungu akatangulia mbele, akasimama mahali penye njia nyembamba, kati ya mashamba ya mizabibu na kuta pande zote mbili. Punda alipomwona malaika huyo wa Mwenyezi-Mungu, akajisukumiza ukutani na kuubana mguu wa Balaamu hapo. Kwa hiyo Balaamu akampiga tena huyo punda. Kisha malaika akatangulia tena, akasimama mahali pembamba pasipo na nafasi ya kupita kulia wala kushoto. Punda alipomwona huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu, akalala chini. Balaamu akawaka hasira, akampiga kwa fimbo yake. Hapo Mwenyezi-Mungu akakifunua kinywa cha huyo punda, akamwambia Balaamu, “Nimekutendea nini hata ukanipiga mara hizi tatu?” Balaamu akamwambia punda, “Wewe umenidhihaki! Kama ningekuwa na upanga ningalikuulia mbali sasa hivi!” Punda akamwambia Balaamu, “Je, mimi si yuleyule punda wako aliyekubeba maisha yako yote hadi siku hii ya leo? Je, nimewahi kukutendea namna hii?” Balaamu akajibu, “La.” Hapo, Mwenyezi-Mungu akayafungua macho ya Balaamu, naye akamwona malaika wa Mwenyezi-Mungu amesimama njiani, ameshika upanga uliochomolewa alani mwake. Balaamu akajitupa chini kifudifudi. Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Balaamu, “Mbona umempiga punda wako mara hizi tatu? Nimekuja kukuzuia, kwa sababu njia yako ni mbaya. Punda wako ameniona akaniepa mara hizi tatu. Kama asingaligeuka mbali nami hakika ningalikuua wewe na kumwacha hai punda huyu.” Balaamu akamwambia malaika wa Mwenyezi-Mungu “Nimetenda dhambi maana sikujua kwamba umesimama njiani kunizuia. Sasa, kama haikupendezi niendelee na safari hii, basi nitarudi nyumbani.” Lakini malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Balaamu, “Nenda na watu hawa, lakini utasema tu kile nitakachokuambia.” Basi, Balaamu akaendelea na safari pamoja na viongozi wa Balaki. Balaki alipopata habari kwamba Balaamu anakuja, alitoka kwenda kumlaki mjini Ari, mji uliokuwa ukingoni mwa mto Arnoni kwenye mpaka wa Moabu. Balaki akamwambia Balaamu, “Kwa nini hukuja kwangu mara moja nilipokuita? Je, ulifikiri sitaweza kukutunukia heshima ya kutosha?” Balaamu akamjibu Balaki, “Sasa nimekuja! Lakini, je, nina mamlaka ya kusema chochote tu? Jambo atakaloniambia Mungu ndilo ninalopaswa kusema.” Basi, Balaamu akaenda pamoja na Balaki wakafika mjini Kiriath-husothi. Huko Balaki alitoa kafara ya ng'ombe na kondoo, akawagawia nyama Balaamu na maofisa waliokuwa pamoja naye. Kesho yake, Balaki alimchukua Balaamu, akapanda naye mpaka Bamoth-baali; kutoka huko, Balaamu aliweza kuwaona baadhi ya Waisraeli.

Shirikisha
Soma Hesabu 22

Hesabu 22:21-41 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Balaamu akaondoka asubuhi, akatandika punda wake, akaenda pamoja na wakuu wa Moabu. Hasira ya Mungu ikawaka kwa sababu alikwenda; malaika wa BWANA akajiweka njiani, ili kumpinga. Basi alikuwa amepanda punda wake, na watumishi wake wawili walikuwa pamoja naye. Na yule punda akamwona malaika wa BWANA amesimama njiani, na upanga wake mkononi mwake amekwisha kuufuta; punda akageuka upande ili kuiacha njia, akaingia shambani. Balaamu akampiga punda ili kumrejesha njiani. Kisha malaika wa BWANA akasimama mahali penye bonde, katikati ya mashamba ya mizabibu, tena penye kitalu upande huu na kitalu upande huu. Yule punda akamwona malaika wa BWANA, akajisukuma ukutani, akaubana mguu wake Balaamu, basi akampiga mara ya pili. Malaika wa BWANA akaenda mbele akasimama mahali pembamba sana, hapakuwa na nafasi ya kugeukia mkono wa kulia, wala mkono wa kushoto. Yule punda akamwona malaika wa BWANA, akajilaza chini ya Balaamu; hasira yake Balaamu ikawaka, akampiga punda kwa fimbo yake. BWANA akakifunua kinywa cha yule punda, naye akamwambia Balaamu, Nimekutenda nini, hata ukanipiga mara tatu hizi? Balaamu akamwambia punda; Kwa sababu umenidhihaki; laiti ningekuwa na upanga mkononi mwangu ningekuua sasa hivi. Yule punda akamwambia Balaamu, Je! Mimi si punda wako, nawe umenipanda maisha yako yote hata leo? Nimezoea kukutenda hayo? Akasema, La! Ndipo BWANA akafunua macho ya Balaamu akamwona malaika wa BWANA amesimama njiani, akiwa na upanga mkononi mwake, umekwisha kufutwa, naye akainamisha kichwa, akaanguka kifudifudi. Malaika wa BWANA akamwambia, Mbona umempiga punda wako mara tatu hizi? Tazama mimi nimekuja ili kukupinga, kwa sababu njia yako imepotoka mbele zangu, punda akaniona, akageuka upande mbele zangu mara tatu hizi; kama asingejiepusha nami, bila shaka ningalikuua wewe, nikamwacha yeye hai. Balaamu akamwambia malaika wa BWANA, Nimefanya dhambi; maana sikujua ya kuwa wewe umesimama njiani ili kunipinga; basi sasa, ikiwa umechukizwa, nitarudi tena. Malaika wa BWANA akamwambia Balaamu Nenda pamoja na watu hawa, lakini neno lile nitakalokuambia, ndilo utakalosema. Basi Balaamu akaenda pamoja na wakuu wa Balaki. Balaki aliposikia ya kuwa Balaamu amefika, akatoka kwenda kumlaki, mpaka Mji wa Moabu, ulioko katika mpaka wa Arnoni, ulioko katika upande wa mwisho wa mpaka huo. Balaki akamwambia Balaamu, Je! Mimi sikutuma watu kwako kwa bidii ili kukuita? Mbona hukunijia? Je! Siwezi mimi kukufanyizia heshima nyingi? Balaamu akamwambia Balaki, Tazama, nimekujia. Je! Mimi sasa nina uwezo wowote kusema neno lolote? Neno lile Mungu atakalolitia kinywani mwangu, ndilo nitakalolisema. Balaamu akaenda pamoja na Balaki wakafika Kiriath-husothi. Balaki akachinja ng'ombe, na kondoo, akampelekea Balaamu na wale wakuu waliokuwa pamoja naye. Ikawa asubuhi Balaki akamchukua Balaamu, akampandisha hadi Bamoth-baali; na kutoka huko aliweza kuwaona baadhi ya Waisraeli hadi pande zao za mwisho.

Shirikisha
Soma Hesabu 22

Hesabu 22:21-41 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Balaamu akaondoka asubuhi, akatandika punda wake, akaenda pamoja na wakuu wa Moabu. Hasira ya Mungu ikawaka kwa sababu alikwenda; malaika wa BWANA akajiweka njiani, ili kumpinga. Basi alikuwa amepanda punda wake, na watumishi wake wawili walikuwa pamoja naye. Na yule punda akamwona malaika wa BWANA amesimama njiani, na upanga wake mkononi mwake amekwisha kuufuta; punda akageuka upande ili kuiacha njia, akaingia shambani. Balaamu akampiga punda ili kumrejeza njiani. Kisha malaika wa BWANA akasimama mahali penye bonde, katikati ya mashamba ya mizabibu, tena penye kitalu upande huu na kitalu upande huu. Yule punda akamwona malaika wa BWANA, akajisonga ukutani, akamseta Balaamu mguu wake, basi akampiga mara ya pili. Malaika wa BWANA akaendelea mbele akasimama mahali pembamba sana, hapakuwa na nafasi ya kugeukia mkono wa kuume, wala mkono wa kushoto. Yule punda akamwona malaika wa BWANA, akajilaza chini ya Balaamu; hasira yake Balaamu ikawaka, akampiga punda kwa fimbo yake. BWANA akakifunua kinywa cha yule punda, naye akamwambia Balaamu, Nimekutenda nini, hata ukanipiga mara tatu hizi? Balaamu akamwambia punda; Kwa sababu umenidhihaki; laiti ningekuwa na upanga mkononi mwangu ningekuua sasa hivi. Yule punda akamwambia Balaamu, Je! Mimi si punda wako, nawe umenipanda maisha yako yote hata leo? Nimezoea kukutenda hayo? Akasema, La! Ndipo BWANA akafunua macho ya Balaamu akamwona malaika wa BWANA amesimama njiani, ana upanga mkononi mwake, umekwisha kufutwa naye akainama kichwa, akaanguka kifudifudi. Malaika wa BWANA akamwambia, Mbona umempiga punda wako mara tatu hizi? Tazama mimi nimekuja ili kukupinga, kwa sababu njia yako imepotoka mbele zangu, punda akaniona, akageuka upande mbele zangu mara tatu hizi; kama asingejiepusha nami, bila shaka ningalikuua wewe, nikamwacha yeye hai. Balaamu akamwambia malaika wa BWANA, Nimefanya dhambi; maana sikujua ya kuwa wewe umesimama njiani ili kunipinga; basi sasa, ikiwa umechukizwa, nitarudi tena. Malaika wa BWANA akamwambia Balaamu Enenda pamoja na watu hawa, lakini neno lile nitakalokuambia, ndilo utakalosema. Basi Balaamu akaenda pamoja na wakuu wa Balaki. Balaki aliposikia ya kuwa Balaamu amefika, akatoka kwenda kumlaki, mpaka Mji wa Moabu, ulioko katika mpaka wa Arnoni, ulioko katika upande wa mwisho wa mpaka huo. Balaki akamwambia Balaamu, Je! Mimi sikutuma watu kwako kwa bidii ili kukuita? Mbona hukunijia? Je! Siwezi mimi kukufanyizia heshima nyingi? Balaamu akamwambia Balaki, Tazama, nimekujia. Je! Mimi sasa nina uwezo wo wote kusema neno lo lote? Neno lile Mungu atakalolitia kinywani mwangu, ndilo nitakalolisema. Balaamu akaenda pamoja na Balaki wakafika Kiriath-husothi. Balaki akachinja ng’ombe, na kondoo, akampelekea Balaamu na wale wakuu waliokuwa pamoja naye. Ikawa asubuhi Balaki akamchukua Balaamu, akampandisha hata mahali pa juu pa Baali; na kutoka huko akawaona watu, hata pande zao za mwisho.

Shirikisha
Soma Hesabu 22

Hesabu 22:21-41 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Balaamu akaamka asubuhi, akatandika punda wake akaenda pamoja na wakuu wa Moabu. Lakini Mungu alikasirika sana alipoenda, naye malaika wa BWANA akasimama barabarani kumpinga. Balaamu alikuwa amepanda punda wake, na watumishi wake wawili walikuwa pamoja naye. Punda alipomwona malaika wa BWANA akiwa amesimama barabarani, na upanga ukiwa mkononi mwake, punda akageukia upande kuelekea shambani. Balaamu akampiga ili amrudishe barabarani. Ndipo malaika wa BWANA akasimama katika njia nyembamba iliyo kati ya mashamba mawili ya mizabibu, yakiwa na kuta pande zote mbili. Punda alipomwona malaika wa BWANA, alijisukumiza karibu na ukuta, na kugandamiza mguu wa Balaamu ukutani. Ndipo Balaamu akampiga tena punda. Kisha malaika wa BWANA akaendelea mbele na kusimama mahali pembamba ambapo hapakuwa na nafasi ya kugeuka mkono wa kulia wala wa kushoto. Punda alipomwona malaika wa BWANA, alilala chini Balaamu angali amempanda, naye Balaamu akakasirika na kumpiga kwa fimbo yake. Kisha BWANA akakifungua kinywa cha punda, akamwambia Balaamu, “Nimekutendea nini kinachokufanya unipige mara hizi tatu?” Balaamu akamjibu punda, “Umenifanya mjinga! Kama ningekuwa na upanga mkononi mwangu, ningekuua sasa hivi.” Punda akamwambia Balaamu, “Je, mimi si punda wako mwenyewe, ambaye umenipanda siku zote, hadi leo? Je, nimekuwa na tabia ya kufanya hivi kwako?” Akajibu, “Hapana.” Kisha BWANA akafungua macho ya Balaamu, naye akamwona malaika wa BWANA amesimama barabarani akiwa ameufuta upanga wake. Balaamu akainama, akaanguka kifudifudi. Malaika wa BWANA akamuuliza Balaamu, “Kwa nini umempiga punda wako mara tatu hizi? Nimekuja kukuzuia kwa sababu njia yako imepotoka mbele yangu. Punda aliniona na kunikwepa mara hizi tatu. Kama punda hangenikwepa, hakika ningekuwa nimeshakuua sasa, lakini ningemwacha punda hai.” Balaamu akamwambia malaika wa BWANA, “Nimetenda dhambi. Sikutambua kuwa umesimama barabarani kunizuia. Basi kama haikupendezi, nitarudi.” Malaika wa BWANA akamwambia Balaamu, “Uende na watu hao, lakini useme tu lile nikuambialo.” Kwa hiyo Balaamu akaenda na wale wakuu wa Balaki. Balaki aliposikia kuwa Balaamu anakuja, akatoka kumlaki katika mji wa Moabu, katika mpaka wa Mto Arnoni, ukingoni mwa nchi yake. Balaki akamwambia Balaamu, “Je, sikukupelekea jumbe za haraka? Kwa nini hukuja kwangu? Hivi kweli mimi siwezi kukulipa?” Balaamu akajibu, “Vema, sasa nimekuja kwako. Lakini kwani nina uwezo wa kusema tu chochote? Ni lazima niseme tu kile ambacho Mungu ataweka kinywani mwangu.” Kisha Balaamu alienda na Balaki hadi Kiriath-Husothi. Balaki akatoa dhabihu ya ngʼombe na kondoo; baadhi yake akampa Balaamu na wakuu waliokuwa pamoja naye. Asubuhi iliyofuata Balaki akamchukua Balaamu hadi Bamoth-Baali, na kutoka huko Balaamu akawaona baadhi ya watu.

Shirikisha
Soma Hesabu 22