Marko 10:2-16
Marko 10:2-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Mafarisayo wakamwendea, na kwa kumjaribu wakamwuliza, “Je, ni halali mume kumpa mkewe talaka?” Yesu akawajibu, “Mose aliwapa maagizo gani?” Nao wakasema, “Mose aliagiza mume kumpatia mkewe hati ya talaka na kumwacha.” Yesu akawaambia, “Mose aliwaandikia amri hiyo kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu. Lakini tangu kuumbwa ulimwengu, Mungu aliumba mwanamume na mwanamke. Hivyo mwanamume atawaacha baba yake na mama yake, ataungana na mke wake, nao wawili watakuwa mwili mmoja. Kwa hiyo, wao si wawili tena bali mwili mmoja. Basi, alichounganisha Mungu, binadamu asitenganishe.” Walipoingia tena ndani ya nyumba, wanafunzi wake walimwuliza juu ya jambo hilo. Naye akawaambia, “Anayemwacha mkewe na kuoa mwingine, anazini dhidi ya mkewe. Na mwanamke anayemwacha mumewe na kuolewa na mwingine anazini.” Watu walimletea Yesu watoto wadogo ili awaguse, lakini wanafunzi wakawakemea. Yesu alipoona hivyo, alikasirika akawaambia, “Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana ufalme wa Mungu ni kwa ajili ya watu walio kama watoto hawa. Nawaambieni kweli, mtu yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hataingia humo.” Kisha akawapokea watoto hao, akawawekea mikono, akawabariki.
Marko 10:2-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamwuliza, Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe? Huku wakimjaribu. Naye akajibu, akawaambia, Musa aliwaamuru nini? Wakasema, Musa alitoa ruhusa kuandika hati ya talaka na kumwacha. Yesu akawaambia, Kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu aliwaandikia amri hii. Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwaumba mwanamume na mwanamke. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja; hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe. Ndipo nyumbani tena wanafunzi wakamwuliza habari ya neno hilo. Akawaambia, Kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine azini juu yake; na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine, azini. Basi wakamletea watoto wadogo ili awaguse; wanafunzi wake wakawakemea. Ila Yesu alipoona alichukizwa sana, akawaambia, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao. Amin, nawaambieni, yeyote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa. Akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabariki.
Marko 10:2-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamwuliza, Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe? Huku wakimjaribu. Naye akajibu, akawaambia, Musa aliwaamuru nini? Wakasema, Musa alitoa ruhusa kuandika hati ya talaka na kumwacha. Yesu akawaambia, Kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu aliwaandikia amri hii. Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja; hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe. Hata nyumbani tena wanafunzi wakamwuliza habari ya neno hilo. Akawaambia, Kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine azini juu yake; na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine, azini. Basi wakamletea watoto wadogo ili awaguse; wanafunzi wake wakawakemea. Ila Yesu alipoona alichukizwa sana, akawaambia, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao. Amin, nawaambieni, Ye yote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa. Akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabarikia.
Marko 10:2-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Baadhi ya Mafarisayo wakaja ili kumjaribu kwa kumuuliza, “Je, ni halali mtu kumwacha mke wake?” Yesu akawajibu, “Je, Musa aliwaamuru nini?” Wakajibu, “Musa aliruhusu kwamba mume anaweza kumwandikia mkewe hati ya talaka na kumwacha.” Yesu akawaambia, “Musa aliwaandikia sheria hiyo kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu. Lakini tangu mwanzo wa uumbaji, ‘Mungu aliwaumba mwanaume na mwanamke’. ‘Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja.’ Kwa hiyo hawatakuwa wawili tena, bali mwili mmoja. Basi, alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.” Walipokuwa tena ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamuuliza kuhusu jambo hili. Akawajibu, “Mtu yeyote amwachaye mkewe na kuoa mke mwingine, anazini naye. Naye mwanamke amwachaye mumewe na kuolewa na mume mwingine, anazini.” Watu walikuwa wakimletea Yesu watoto wadogo ili awaguse, lakini wanafunzi wake wakawakemea. Yesu alipoona yaliyokuwa yakitukia, akachukizwa. Akawaambia wanafunzi wake, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana ufalme wa Mungu ni wa wale walio kama hawa. Amin, nawaambia, mtu yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hatauingia kamwe.” Akawachukua watoto mikononi mwake, akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabariki.