Mathayo 5:1-20
Mathayo 5:1-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu alipoyaona makundi ya watu, alipanda mlimani, akaketi. Wanafunzi wake wakamwendea, naye akaanza kuwafundisha: “Heri walio maskini rohoni, maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri walio na huzuni, maana watafarijiwa. Heri walio wapole, maana watairithi nchi. Heri wenye njaa na kiu ya kufanya atakavyo Mungu, maana watashibishwa. Heri walio na huruma, maana watahurumiwa. Heri wenye moyo safi, maana watamwona Mungu. Heri wenye kuleta amani, maana wataitwa watoto wa Mungu. Heri wanaoteswa kwa sababu ya kufanya atakavyo Mungu, maana ufalme wa mbinguni ni wao. “Heri yenu nyinyi watu wakiwatukana, wakiwadhulumu na kuwasingizia kila aina ya uovu kwa ajili yangu. Furahini na kushangilia maana tuzo lenu ni kubwa mbinguni. Hivyo ndivyo walivyowadhulumu manabii waliokuwako kabla yenu. “Nyinyi ni chumvi ya dunia. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake itakolezwa na nini? Haifai kitu tena, ila hutupwa nje na kukanyagwa na watu. “Nyinyi ni mwanga wa ulimwengu! Mji uliojengwa juu ya mlima hauwezi kufichika. Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa debe, ila huiweka juu ya kinara ili iwaangazie wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo, ni lazima mwanga wenu uangaze mbele ya watu, ili wayaone matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni. “Msidhani kuwa nimekuja kutangua sheria na mafundisho ya manabii. Sikuja kutangua bali kukamilisha. Kweli nawaambieni, mpaka hapo mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata nukta moja au sehemu ndogo kabisa ya sheria itakayoondolewa, mpaka yote yametimia. Basi, yeyote atakayevunja hata amri moja ndogo kuliko zote, na kuwafundisha wengine wafanye hivyo, huyo atakuwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni. Lakini yule atakayezishika na kuwafundisha wengine, huyo atakuwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni. Ndio maana nawaambieni, wema wenu usipozidi ule wa waalimu wa sheria na wa Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.
Mathayo 5:1-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye alipowaona makundi ya watu, alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjia; akafumbua kinywa chake, akawafundisha, akisema, Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri wenye huzuni; Maana hao watafarijika. Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi. Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa. Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema. Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu. Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu. Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu. Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikipoteza ladha yake, ladha hiyo itarudishwa vipi? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu. Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji ukiwa juu ya mlima hauwezi kusitirika. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni. Msidhani ya kuwa nilikuja kuitangua Torati au Manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie. Basi mtu yeyote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni. Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya Waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.
Mathayo 5:1-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye alipowaona makutano, alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjia; akafumbua kinywa chake, akawafundisha, akisema, Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri wenye huzuni; Maana hao watafarijika. Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi. Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa. Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema. Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu. Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu. Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu. Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu. Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni. Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie. Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni. Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.
Mathayo 5:1-20 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi Yesu alipoona makundi ya watu, alipanda mlimani akaketi chini, nao wanafunzi wake wakamjia. Ndipo akaanza kuwafundisha, akisema: “Heri walio maskini wa roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri wale wanaohuzunika, maana hao watafarijiwa. Heri walio wapole, maana hao watairithi nchi. Heri wenye njaa na kiu ya haki, maana hao watatoshelezwa. Heri wenye huruma, maana hao watapata rehema. Heri walio na moyo safi, maana hao watamwona Mungu. Heri walio wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu. Heri wanaoteswa kwa sababu ya haki, maana ufalme wa mbinguni ni wao. “Heri ninyi watu watakapowashutumu, na kuwatesa na kunena mabaya ya aina zote dhidi yenu kwa uongo kwa ajili yangu. Furahini na kushangilia kwa maana thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa kuwa hivyo ndivyo walivyowatesa manabii waliokuwa kabla yenu. “Ninyi ni chumvi ya ulimwengu. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake, yawezaje kurudishiwa ladha yake tena? Haifai tena kwa kitu chochote, ila kutupwa nje ikanyagwe na watu. “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji uliojengwa kilimani hauwezi kufichika. Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa bakuli. Badala yake, huiweka kwenye kinara chake, nayo hutoa mwanga kwa kila mtu aliye ndani ya ile nyumba. Vivyo hivyo, nuru yenu iangaze mbele ya watu, ili wapate kuona matendo yenu mema wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni. “Msidhani kwamba nimekuja kufuta Sheria au Manabii; sikuja kuondoa bali kutimiza. Kwa maana, amin nawaambia, hadi mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata herufi moja ndogo wala nukta itakayopotea kwa namna yoyote kutoka kwa Sheria, hadi kila kitu kiwe kimetimia. Kwa hiyo, yeyote atakayevunja mojawapo ya amri ndogo kuliko zote ya amri hizi, naye akawafundisha wengine kufanya hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni, lakini yeyote azitendaye na kuzifundisha hizi amri ataitwa mkuu katika ufalme wa mbinguni. Kwa maana nawaambia, haki yenu isipozidi haki ya Mafarisayo na walimu wa sheria, kamwe hamtaingia katika ufalme wa mbinguni.